July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ICC yamuweka kifungo cha miaka 25 mhalifu wa kivita Uganda

Dominic Ongwen akiwa katika mahakama ya ICC

Spread the love

 

MAHAKAMA ya Kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu (ICC), iliyopo mjini The Hague, nchini Uholanzi, imemuamuru Dominic Ongwen, kutumikia kifungo cha miaka 25 gerezani. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hukumu dhidi ya mbabe huyo wa kivita, imetolewa muda mfupi uliopita, leo Alhamisi, tarehe 6 Mei 2021. Mahakama imesema, mazingira ya utotoni ya Ongwen hayastahili kuhalalisha mateso kwa waathiriwa.

Ongwen aliingizwa kwenye kundi la uasi la Lord’s Resistance Army (LRA), lenye makao yake makuu nchini Uganda, baada ya kutekwa wakati akielekea shuleni, akiwa na mama yake.

Alikutwa na hatia katika mashitaka zaidi 60, yakiwemo mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watu katika hali ya utumwa.

Majaji wamesema, Ongwen binafsi alitoa amri kwa wapiganaji wake kuwauwa watu wapatao 130 katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2002 na 2005.

Mkuu wa jopo la majaji hao, Bertram Schmitt amesema, wamekabiliana na hali isiyo ya kawaida, kwa sababu mtuhumiwa mbele yao alikuwa mhanga na mhalifu kwa wakati mmoja.

Mawakili wake walitaka Ongwen kupewa adhabu ya kifungo cha miaka 20 gerezani, kwa hoja kuwa kutekwa kwake akiwa mwanafunzi na kuingizwa katika kundi kundi hilo la waasi, kunahalalisha kupunguziwa adhabu ambayo ingekuwa kifungo cha miaka 30 gerezani.

Kesi dhidi ya Ongwen ilijikita zaidi kwenye uhalifu uliotendwa kati ya mwaka 2002 hadi 2005, kipindi ambacho waendesha mashtaka walisema, LRA ilifanya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono, ndoa za kulazimisha, utesaji, uporaji na kuwasajili watoto chini ya umri wa miaka 15 kama wapiganaji.

Dominic Ongwen

Kesi hiyo, ilikuwa ya kwanza kwenye mahakama ya ICC ikihusisha mtuhumiwa ambaye pia ni muhanga wa uhalifu ule ule wa kivita uliofanywa na LRA, kwa sababu Ongwen mwenyewe alitekwa nyara na waasi akiwa mtoto alipokuwa njiani kwenda shule.

Aidha, Ongwen ambaye alipachiwa jina la utani la “siafu mweupe,” ni mpiganaji wa kwanza wa kundi hilo la waasi, kukabiliwa na mashtaka kwenye mahakama ya ICC au kwengineko kuhusiana na madhila na umwagaji damu uliyofanywa na kundi hilo katika mataifa manne ya Afrika.

Mbabe huyo wa kivita mwenyewe alijitetea “kwa jina la mwenyezi Mungu” kuwa hana hatia na mawakili wake walisema, mara kadhaa kwamba mashtaka dhidi yake sharti yaondolewe kwa sababu mtuhumiwa aliathiriwa kisaikolojia kwa kuchukuliwa mateka na waasi alipokuwa mtoto.

Katika kundi hilo, Ongwen alipanda ngazi hadi kufikia wadhifa wa naibu kamanda wa kundi hilo la waasi la LRA.

 

 

Mwaka 1975 katika kijiji cha Choorum wilayani Amuru, Kaskazini mwa Uganda.

Alitekwa nyara na kundi hilo linaloongozwa na Josephy Kony, akiwa mvulana mdogo wa miaka 14, wakati akielekea shule ya msingi Abili Koro 9 au 10.

Alibebwa katika safari yao hadi kwenye kambi ya LRA, kutokana na kutoweza kutembea.

Mama yake, Ogwen alipofahamishwa habari za kutekwa nyara kwa mtoto wake aliamuwa kuwafata wafuasi hao, na badaye watu walimkuta mama huyo amefariki pamoja na mumewe.

Baada ya muda akiwa na umri wa miaka 18, Ogwen alipewa cheo cha Brigadier wa kundi la waasi wa LRA na kuongoza kikosi cha Sinia.

Ogwen alishirika katika matukio mbalimbali ya uhalifu wa kivita mwezi wa Mei mwaka 2004 walishambulia kambi ya ndani ya Lukodi wilayani Gulu, nchini Uganda.

Ameshambulia pia kambi nyingine za ndani ikiwemo ya Pajule, Odeke na Abok na kushiriki mauaji mbalimbali ya wanchi wasiokuwa na hatia, ubakaji na unyanyasaji wa kigono.

error: Content is protected !!