July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Huyu ndiye Rais Pohamba mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim

RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba

Spread the love

RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba (79), ameingia kwenye historia ya washindi wa tuzo ya dola milioni tano ya Mo Ibrahimu ya uongozi wa Afrika.

Rais huyo ambaye anatarajiwa kumkabidhi madaraka yake kwa rais mteule, Hage Geingob, anakuwa kiongozi wan ne kukwaa tuzo hiyo, akitanguliwa na Joachim Chissano wa Msumbiji (2007), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Pedro Pires wa Cape Verde (2011).

Tuzo hiyo ya dola milioni 5 hutuzwa kiongozi wa Kiafrika aliyechaguliwa na anayeongoza kwa njia bora na kuinua maisha ya watu na kuondoka madarakani.

Rais mtaafu wa Msumbiji mwaka 2005, Chissano ndiye alikuwa wa kwanza kutunukiwa tuzo hii ya heshima mwaka 2007, huku miaka mingine ikipita bila kupata mshindi kutokana ugumu wa vigezo.

Salim Ahmed Salim- Mwenyekiti wa kamati inayotafuta mshindi wa tuzo hiyo iliyotolewa Nairobi nchini Kenya, anasema Namibia chini ya Pohamba imeweza kuwa na utawala mzuri na kujiletea heshima. Anaongeza kuwa Namibia chini ya Pohamba ina demokrasia ya kweli, imekuwa imara na inayoheshimu uhuru wa habari na haki za binadamu,

Tuzo hii ni malipo ya awali ya dola za Marekani milioni 5 (sawa sh. bilioni 8.3) zinazotolewa kwa awamu kwa kipindi cha miaka kumi, zaidi ya malipo haya Pohamba atapewa dola laki 2 kwa kila mwaka kwa maisha yake yote.

Pia tuzo hii inaaminika kuwa kubwa na yenye thamani zaidi duniani ikiipiku Tuzo ya Nobeli ya Amani (Nobel Peace Prize) kwa zaidi ya mara tatu na nusu. Mshindi wa Tuzo ya Nobel anapewa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.3.

Tuzo ya Mo Ibrahim inatolewa kwa Rais aliyemaliza muda wake Afrika na mchakato wa kumpata unafanywa na kamati maalumu ya watu mashuhuri; kamati hii pia inajumuisha watu wengine wawili waliowahi kupata tuzo ya Nobel.

[pullquote]

WASHINDI

2007-Joachim Chissano (Msumbiji)

2008-Festus Mogae (Botswana)

2009- Hamna tuzo iliyotolewa

2010- Hamna tuzo iliyotolewa

2011-Pedro Pires (Cape Verde)

2012-Hamna tuzo iliyotolewa

2013-Hamna tuzo iliyotolewa

2014- Hifikepunye Pohamba (Namibia)

[/pullquote]

Tuzo hii inatolewa ili kutambua na kusherehekea viongozi wa Afrika waliotumia uwezo wao kuzijenga nchi zao kwa kuimarisha uchumi na huduma za kijamii na waliofanya juhudi za kupunguza umaskini na uimarishaji wa maendeleo endelevu yenye usawa kwa wote.

Utolewaji wa tuzo hii unaifanya Afrika iendelee kufaidika na uzoefu na weledi wa marais waliomaliza muda wao wa kutawala. Tuzo hii inawawezesha kuendelea kufanya shughuli nyingine za kijamii wanapomaliza muda wao wa kutawala.

Vigezo vinavyotumika katika kutafuta mshindi ni pamoja na Rais aliyemaliza muda wake katika nchi mojawapo ya Afrika; awe ameng’atuka madarakani sio zaidi ya miaka mitatu iliyopita; aliyechaguliwa kidemokrasia; aliyetumikia muda wake kwa mujibu wa katiba na aliyeonyesha kwa vitendo kuwa na sifa za pekee za uongozi.

Pohamba ni nani?

Huyu amezaliwa mwaka 1935 huko Namibia ya Kaskazini, eneo lililokuja kuwa ngombe ya harakati za SWAPO- Chama ambacho tangu uhuru 1990 kimekuwa kikitawala na kushinda chaguzi kwa ushindi wa kishindo.

Pohamba alipata elimu yake kwa wamisionari na akaajiriwa na mgodi wa Shaba akiwa kijana. Ni mwenza wa uanzilishi wa SWAPO na rafiki yake Sam Nujoma, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Namibia.

Aliwahi kufungwa kwa sababu za harakati na utawala uliosaidiwa na makaburu. Amekuwa Waziri wa Ardhi baada ya uhuru, aliyeleta mabadiliko kwenye sekta ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuigawa kwa wananchi.

Pohamba alipendekezwa na Nujoma kurithi mikoba ya urais mwaka 2004 na sasa mikoba hiyo anamwachia Hage Geingob.

Tuzo hii inafadhiliwa na Mo Ibrahim mzaliwa wa Sudan lakini ana uraia wa Uingereza; ni mjasiriamali na bilionea anayemiliki biashara ya mawasiliano ya simu kwakuwekeza katika nchi za Afrika.

Tuzo hii inatolewa kila mwaka lakini tangu 2007 ilipoanza ni marais watatu tu walizawadia, huku Nelson Mandera akizawadia kwa heshima.

 

error: Content is protected !!