Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari Huyu ndiye Mama Samia, Rais wa kwanza mwanamke Tanzania
HabariTangulizi

Huyu ndiye Mama Samia, Rais wa kwanza mwanamke Tanzania

Spread the love

 

MAMA Samia Suluhu Hassan, ameapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu, jijini Dar es Salaam. Anaandika Regina Mkonde…(endelea).

Ni baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, kilichotokea Jumatano tarehe 17 Machi mwaka huu, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho, mkoani Dar es Salaam.

Mama Samia (61), anaweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa rais pia kuwa Rais wa Tanzania.

Mama Samia, ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na marais wastaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Ally Hassan Mwinyi wa Tanzania na Abeid Amani Karume wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Mara baada ya kuapishwa katika moja ya ukumbi wa Ikulu, Rais Samia alikwenda kukagua gwaride maalum la vikosi vua ulinzi na usalama ikiwemo kupigiwa wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki huku mizinginga 21 ikipigwa.

Marais waliotangulia ni Hayati Julius Kambarage Nyerere (1964-1985), Alhaji Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Hayati Benjamin Willim Mkapa (1995-2005), Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (2005-2015) na Hayati Dk. John Pombe Magufuli 2015- Machi 2021.

Pia, anakuwa Rais wa Pili wa Tanzania kutokea Zanzibar akitanguliwa na Mzee Mwinyi.

Mama Samia atashikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia za zaidi ya miaka mine na nusu cha muhula wa urais (2020-2025).

Mama Samia alizaliwa tarehe 27 Januari 1960 visiwani Zanzibar.

Alisomea Shule za Msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) kati ya 1966 na 1972 na kisha akasomea masomo ya upili Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja mwaka 1976.

Mama Samia alisomea kozi mbalimbali na kupata Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Aliajiriwa kama mchapishaji katika Serikali ya Zanzibar mwaka 1977 na kupanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango serikalini (1987 – 1988).

Alihudumu pia kama meneja wa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama Meneja Mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGO 1998 hadi 1999.

Mama Samia, ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Mama Samia alijiunga na siasa mwaka wa 2000, wakati huo akiwa Mjumbe Maalum wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Haikuchukua muda mrefu nyota yake ikaanza kung’aa na akateuliwa kuwa Waziri na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, akipewa wadhifa wa Waziri wa Leba, Jinsia na Watoto.

Alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2005, alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri, wakati huu akipewa Wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji visiwani humo.

Mwaka 2010, Mama Samia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi.

Punde tu akateuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Kikwete kuwa Waziri wa Maswala ya Muungano katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Wakati wa Bunge Maalum la Katiba, Machi 2014, Mama Samia aliwania na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, mjini Dodoma.

Alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Amina Abdalla Amour ambaye alipata kura 126 sawa na asilimia 24.

Mama Samia akawa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo wakati Hayati Samuel Sitta akiwa mwenyekiti. Baada ya Dk. Magufuli kushinda nafasi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Julai 2015, alimchagua Mama Samia kuwa mgombea wake mwenza.

Tarehe 5 Novemba 2015, kwa pamoja Dk. Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Mama Samia, akiapishwa kuwa mgombea mwenza.

Mama Samia alichaguliwa pia na Dk. Magufuli kuwa mgombea wake mwenza, mwaka jana na waliposhinda uchaguzi mkuu, waliapishwa tena kwa pmaoja tarehe 5 Novemba 2020 kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Mama Samia ni mke wa Hafidh Ameir waliooana mwaka 1978 na kuwajaalia kupata watoto wanne akiwemo Wanu ambaye ni mbunge wa viti maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tunamtakia kila la kheri katika kuwatumikia wananchi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!