Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Huyu ndiye John Magufuli aliyetutoka 1959-2021
Habari za SiasaTangulizi

Huyu ndiye John Magufuli aliyetutoka 1959-2021

Hayati John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania
Spread the love

 

DK. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amehitimisha safari ya miaka 61 ya maisha yake hapa duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Magufuli, amehitimisha safari hiyo jana Jumatano saa 12:00 jioni, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho, mkoani Dar es Salaam.

Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, alilitangazia Taifa juu ya kifo hicho akisema, Rais Magufuli amefikwa na mauti kutokana na tatizo la maradhi ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mama Samia ambaye sasa anasubiri kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, alitangaza siku 14 za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.

John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 huko wilayani Chato Mkoani Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya mkoa mpya wa Geita).

Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974.

Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo, mkoani Kagera ambako alisoma kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 – 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza alikosoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 – 1978.

Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981.

Halafu alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 1981 – 1982.

Alipopata stashahada yake, moja kwa moja alikwenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.

Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983.

Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai – Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).

Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.

Mwaka 1989 – 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.

Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari.

Safari yake kwenye siasa

Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36.

Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu.

Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.

Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili.

Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika mwaka 2005.

Mwaka 2005 aliendelea kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge kwa kipindi cha tatu.

Akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa.

Lakini safari hii, Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne.

Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.

Katika uchaguzi ule, alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema.

Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, aliyohudumu hadi mwisho mwaka 2015.

Ajitosa kwenye mbio za urais

Dk Magufuli alikuwa miongoni mwa wana CCM 42 waliojitosa kuchukua fomu za kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Idadi hiyo ya makada wa CCM, haikuwahi kufikiwa tangu kuanzia kwa mafumo wa vyama vingi mwaka 1992 na mwisho wa mchakato wa ndani, Dk. Magufuli alipitishwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, uliokuwa na mchuano mkali kutoka kwa vyama vya upinzani ambavyo vyama vinne, vilishirikiana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge na udiwani.

Ushirikiano huo, ulipewa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukihusisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF ambapo, Edward Lowassa, ndiye alipitishwa kuwa mgombea urais.

Lowassa aliyewahi kuwa waziri mkuu, alijiunga na Chadema tarehe 28 Julai mwaka 2015, akitoka CCM ambako hakuridhika na mchakato wa kumpata mgombea urais, hivyo kuamua kutafuta fursa upinzani.

Rais John Magufuli

Hata hivyo, uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza Dk. Magufuli kuwa mshindi kwa kupata kura milioni nane sawa na asilimia 58.46.

Lowassa alijipatia kura milioni sita sawa na asilimia 39.97. Hata hivyo, si Lowasa au Ukawa waliokubali matokeo hayo.

Dk. Magufuli, alitafuta tena fursa ya Watanzania, katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba mwaka 2020, ambapo alitetea nafasi hiyo baada ya kupata kura milioni 12.5 sawa na asilimia 84 ya kura zote milioni 15.9 huku mshindani wake wa karibu kutoka Chadema, Tundu Lissu, akiambulia kura milioni 1.9 sawa na asilimia 13.

Tarehe 5 Novemba 2020, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, kumalizia ungwe ya pili ya miaka mitano na tayari alikuwa amekaa madarakani takribani miezi minne.

Kama ambavyo yeye mwenyewe amekuwa akinukuliwa, enzi za uhai wake, alisema siku akifikwa na mauti basi akazikwe nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Dk. Magufuli, ameacha watoto na Mjane Mama Janeth.

Nenda Salama, Safari umeiimaliza.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!