January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Huu ni ushauri wangu kwa meya Silaa

Meya Jerry Silaa

Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa

Spread the love

MEYA wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ameshindwa kuendesha manispaa hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam. Je, ataweza ubunge alioonesha nia ya kugombea katika uchaguzi mkuu mwaka ujao? Tusubiri.

Vyovyote iwavyo, ashinde ubunge au ashindwe, ameweka historia. Huyu ni kijana wa kwanza katika historia ya Manispaa ya Ilala kuwa meya mwenye umri mdogo kuwahi kuongoza manispaa iliyo katikati ya jiji na ambayo ina shughuli nyingi za kiuchumi ambako hata Ikulu ya Magogoni iko ndani yake.

Katika historia ya majiji, duniani kote madiwani wanaitwa City Fathers yaani Wazee wa Jiji; watu wazito kwa vyeo, waliostaafu au wenye shughuli zao kubwa kubwa, mabwanyenye wenye majumba yao maeneo husika.

Kwa Silaa imekuwa tofauti, yeye ameingia kwenye uongozi wa udiwani akiwa anasoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa hata hajaoa, hivyo alivunja utamaduni kwamba meya lazima awe mzee mwenye umri mkubwa na mwenye shughuli kubwa kubwa.

Huko nyuma ilizoeleka kuona mameya kama Kitwana Kondo, Abdulwahid Sykes, Adam Kimbisa na Abuu Jumaa, majina mazito yenye sifa nyingi na historia ndefu. Lakini kwa Silaa haikuwa hivyo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 Silaa alichaguliwa tena kuwa diwani kisha akaomba nafasi kuwa Meya wa Manispaa ya Ilala. Chama chake CCM kilimpitisha kuwania nafasi hiyo baada ya kuwashinda meya wa muda mrefu, Abuu Juma, na Bisalala Salum

Katika uchaguzi wa CCM mwaka 2012 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) vyombo vya chama vinavyofanya maamuzi makubwa ya nchi kwa ujumla.

Katika hali ya kawaida na kwa mtu yeyote, kwa kadri anavyopanda juu kwa kupata vyeo vingi ndivyo anavyozidi ‘kujitenga’ na wananchi wa kawaida na matatizo yao maana anakuwa amepanda daraja yuko ngazi nyingine ya uongozi.

Zamani hatukuwahi kumsikia Silaa kwenda mikoa mingine kufanyia kampeni wagombea wa chama chake wawe wa ubunge au udiwani, lakini kwenye uchaguzi wa Kalenga tulimwona akimfanyia kampeni Godfrey Mgimwa ambaye sasa ni mbunge. Alikwenda Kalenga kwa nafasi yake kama mjumbe wa NEC na CC hivyo ana majukumu na wajibu mkubwa zaidi ya udiwani aliokuwa nao kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.

Kama Msitahiki Meya wa Ilala ana watu wengi wanaohitaji huduma yake. Kila mtu anahitaji msaada fulani kutoka kwake kama wa kupewa viwanja au maeneo ya kufanyia biashara katikati ya mji.

Siku moja nilikutana naye kwenye sherehe nyumbani kwa Balozi wa Marekani jijini Dar es Salaam. Nilizungumza naye kama mwananchi wake mkazi wa mtaa wa Ugombolwa, kata ya Segerea. Baada ya muda mfupi watu wakubwa walikuja wakaondoka naye.

Kama meya, Silaa anakabiliwa na changamoto nyingi za kiutendaji. Mfano, mvua zilizonyesha mwaka huu jijini Dar es Salaam na nchi nzima zilikuwa nyingi sana na zilileta uharibifu na maafa makubwa.

Mvua hizi zimeharibu barabara kadhaa na kuvunja baadhi ya madaraja. Barabara kadhaa za Ilala, ikiwemo ya Uhuru ziliharibiwa. Wiki kadhaa baada ya mvua kukoma, barabara ziko vilevile, tofauti na Manispaa ya Kinondoni, inayoongozwa na meya mwingine kijana Yusuf Mwenda.

Kinondoni kuna kazi zinafanyika, Ilala kimya. Sababu rahisi inayotolewa na watu mbalimbali eti ni kwamba huko kuna wabunge na madiwani wa upinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaotoa changamoto kwenye baraza la madiwani tofauti na Ilala.

Ilitarajiwa meya ambaye katika hali ambayo hakuna upinzani mkubwa ndani ya baraza, ndiye angefanya kazi vizuri, lakini imekuwa tofauti.

Barabara ya Uhuru karibu na mzunguko wa Msimbazi na kuelekea Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) hadi Buguruni ni balaa, kwani kuna mahandaki kama si mashimo. Barabara ya Lindi kuelekea Mtaa wa Shaurimoyo kuanzia Shule ya Uhuru pia haifai.

Suala jingine ni uchafu katika manispaa. Mitaa mbalimbali ni michafu, takataka haziondolewi kwa wakati, mitaa inanuka harufu kali, hasa maeneo ya Kariakoo. Hapa sijazungumzia Uswahilini, uchafu ni sehemu ya maisha ya watu huku jiji likikusanya kodi zinazotumika kulipia umeme wa viyoyozi ofisini.

Hii haina maana Silaa hajafanya lolote, la hasha. Ilala wamefanya mengi na kwa kweli ndiyo kazi waliyoomba kwetu kama kugawa madawati; kujenga barabara na shule. Ninachosema hapa Silaa ameshindwa kufukia mahandaki kwenye barabara hizi angalau kubwa na zilizopo usoni pa manispaa.

Maana kama kazi hizi zinamshinda, vipi ubunge ambao ameonesha nia ya kugombea? Silaa hajasema jimbo gani, lakini wengi wanadhani angegombea Jimbo la Ukonga linaloshikiliwa na Eugine Mwaiposa. Hii ni kwa sababu, Silaa amekuwa diwani wa kata ya Gongo la Mboto kwa kipindi cha pili sasa – mwaka 2005 hadi 2015.

Hata hivyo, anataka kugombea ubunge katika Jimbo la Segerea. Alianza kampeni za kutafuta jimbo hili tangu alipochaguliwa kuwa meya wa Manispaa ya Ilala na mjumbe wa CC na NEC.

Anawania jimbo hilo linaloongozwa na Makongoro Mahanga, ambaye ni naibu waziri wa Kazi, na wala siyo jimbo la Ilala linaloongozwa na Azan Zungu ambaye pia ni mwenyekiti wa bunge.

Kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Mheshimiwa huyu anataka kumng’oa Mahanga. Uchunguzi unaonesha katika kipindi cha mwaka 2011 na 2013 amefanya kazi kubwa za kisiasa Segerea kuliko mahali pengine katika wilaya ya Ilala. Huko ndiko amefungua vizimba vingi sana vya wakereketwa wa CCM.

Nina ushauri mdogo na wa bure kwa Silaa. Aanze kazi ya kufukia mashimo na mahandaki kwenye mabarabara zilizoharibiwa na mvua, kuzoa takataka zote kabla hazijaleta madhara makubwa kwa binadamu ili watu wasije kumhukumu kwa kazi isiyoridhisha ya miaka mitano ya umeya.

Ajue anaweza kukimbia watu wanaomfuata kutaka kuzungumza naye lakini hawezi kukwepa matatizo kwa kuwakimbia watu wanaomfahamu vizuri.

*Mwandishi wa makala hii, Hebron Mwakagenda ni mkazi wa Manispaa ya Ilala, msomaji wa gazeti la Mawio na mwanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii anapatikana kupitia: 0713612681 barua pepe:mwakagendah@yahoo.com

error: Content is protected !!