HUKUMU ya kesi ya Jinai Na. 36/2020, inayomkabili kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, imepigwa kalenda. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).
Hukumu hiyo ilipangwa kusomwa leo Jumatatu, tarehe 14 Juni 2021, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Zawadi Laizer, lakini imeahirishwa hadi tarehe 28 Juni mwaka huu.
Hakimu Laizer alisema, ameahirisha kusoma hukumu hiyo, kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, Wakili wa Mdude, Faraji Mangula, amesema hukumu hiyo haijasomwa leo, kwa kuwa haikuwa tayari.
“Hukumu ya kesi ya Jinai Na. 36/2020, imepangwa kutolewa tarehe 28 Juni 2021. Imeahirishwa kwa sababu hukumu haijawa tayari, hakimu amesema haijawa tayari kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake, hivyo hawezi kuisoma,” amesema Wakili Mangula.
Awali, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, aliongoza wafuasi wa chama hicho, akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.
Kada huyo wa Chadema anayesota rumande tangu Mei 2020, anakabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin, zenye uzito wa gramu 23.4.
Mdude alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, tarehe 10 Mei 2021, baada ya kufanyiwa upekuzi katika hoteli moja jijini humo, alikokuwa amepanga, na kudaiwa kukutwa na dawa hizo.
Leave a comment