July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Huduma zarejea Kliniki ya Foreplan

Sehemu ya dawa katika kiliniki ya ForePlan

Spread the love

MENEJIMENTI ya Kliniki ya Foreplan imelazimika kutoa huduma bila malipo kwa wateja ambao walishaanza kutumia dawa wakati serikali ilipoifunga.

“Kliniki ilipofungwa ilisababisha wagojwa kukatiza dozi. Sasa baada ya kufunguliwa tumelazimika kuwaanzishia matibabu upya bila malipo wale waliokuwa wanaendelea na dozi,” anasema Dk. Juma Mwaka.

Anasema gharama hizo zinabebwa na kliniki badala ya kuwabebesha wagonjwa mzigo wa gharama kwa kuwa baadhi yao hawawezi tena kugharamia kutokana na kipato duni.

Kauli hiyo inakuja wakati kliniki ikiwa imeanza tena huduma kama kawaida baada ya Mahakama ya Wilaya kuondoa amri iliyowekwa na Baraza la Tiba Mbadala 28 Novemba.

Baraza hilo kupitia kwa Msajili wake, Mboni Bakari, lilifunga kliniki hiyo kwa madai kuwa inatoa huduma kinyume cha taratibu za kisheria. Kliniki ipo Bungoni Ilala, ikihudumia zaidi wanawake wanaohangikia kupata uzazi.

Akieleza hasara iliyopatikana kutokana na uamuzi huo, Dk. Mwaka anasema wakati kliniki inafungwa tarehe 6 Novemba, kulikuwa na wagonjwa waliokuwa wanatumia dawa lakini ikashindikana kuendelea na dozi.

“Wakati wanafunga kituo, kulikuwa na shehena ya madawa ndani, dawa hizi zingeweza kusaidia wagonjwa lakini nyingi zimeharibika. Haziwezi kutumika tena,” anasema katika mahojiano na MwanaHALISI Online.

Hasara zaidi kwa kliniki hiyo kufungwa ilitokana na kuwalipa wafanyakazi 40 wakati wakiwa hawafanyi kazi kwa muda wote huo.

“Tuliwalipa posho wafanyakazi licha ya kituo kufungwa. Halikuwa kosa lao wafanyakazi na hatukuona kama ni haki kutowalipa. Wametuonesha imani kubwa na tukaona wapate faraja,” anasema.

Lakini madhara ya kufungwa kwa Kliniki ya Foreplan yalifika mbali. Mfanyakazi mmoja aliyekuwa na ujauzito mchanga, aliugua kwa mshtuko hadi mimba yake ikaharibika.

Analalamika kuwa namna wale wafanyakazi wa Baraza la Tiba Mbadala walivyowasili na kutimiza lengo lao, ilimtia hofu mtumishi huyo ambaye ameomba asitajwe kwa jina.

“Nilikuwa na ujauzito wa miezi mitatu na hali yangu ya afya haikuwa nzuri. Watu wale walianza kufunga milango ya ofisi. Nilihamaki, woga ukanishika. Mapigo ya moyo yakabadilika. Nikasikia kizunguzungu na kushindwa kusimama,” anasimulia.

Kwa hali aliyonayo, aliomba kutoka nje ya chumba, lakini alizuiwa na waliokwenda na amri ya kufunga kliniki, kitendo kilichosababisha hali yake kuwa mbaya.

“Ilipofika tarehe 7 Novemba, nikaenda hospitali ya Burhan iliyopo Posta, nikalazwa lakini ilipofika usiku nilitokwa na damu nyingi, hali iliyoashiria mimba yangu kuharibika,” anasema.

“Niliumia sana roho kwa kauli ya Daktari ambaye aliniambia kuwa mimba imepungua hivyo isingeweza kuendelea kukua,” anasema.

“Inaniuma sana, leo mimba ile ingekuwa kubwa. Ilitoka kwa sababu ya mshituko niliopata wakati kituo kilipovamiwa na kufungwa moja kwa moja kwa sababu sikujua hatma ya ajira yangu,” anasema.

Kliniki ya Foreplan hupokea zaidi ya wagonjwa 200 kwa siku. Watu wanaofika kupata huduma hapo

wengine wanatoka mikoani nchi nzima.

Kama yapo mafunzo muhimu ambayo Dk. Mwaka alipata, basi ile hali ya wateja kuendelea kufika kituoni wakiwa na matumaini ya huduma kurudi haraka, ilimshtua kiasi cha kujizuia kutokeza kituoni.

“Kumbe Watanzania wananikubali. Awali sikulijua hili. Watu wengi walinifariji kwa kilichotokea , kama wanasema ukipatwa na tatizo ndio utajua rafiki yako wa kweli, nimeamini.

Mtu mmoja kiongozi mkubwa nchini alinipigia kunifariji na akaniambia mama yake naye alikuwa anapata matibabu kwetu. Jambo la kutia moyo sana,” alisema.

Anasema amezidi kupata moyo kwamba tiba mbadala ni tiba inayotegemewa na watu wengi nchini hasa wakati huu ambao hospitali zilizopo hazitoshi.

Dk. Mwaka haachi kugusia mkasa uliotokea kwa kuwa pamoja na kuamua kuitumia mahakama kutafuta haki yake, kulikuwa na ukaidi wa jeuri kwa waliofunga kliniki kutekeleza amri ya mahakama kufungua kliniki.

“Mpaka sasa ninaamini hakuna yeyote aliye juu ya sheria, lakini inasikitisha Mahakama inatoa amri halafu watumishi wa serikali wanakaidi amri hiyo,” alisema.

error: Content is protected !!