December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Huduma za tiba masikitiko matupu

Waziri wa Afya, Dr. Seif Rashid

Spread the love

HUDUMA za afya nchini zinazogharamiwa na serikali, zinasikitisha. Kwa sehemu kubwa zimekumbwa na tatizo kubwa la uhaba wa dawa na vifaa tiba kiasi cha viongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuamua kuongeza gharama za huduma.

Hospitali hiyo inayotegemewa kusaidia wagonjwa wanaoshindikana kwenye hospitali za rufaa mikoani na zile za manispaa tatu jijini Dar es Salaam, inakabiliwa na madeni na hivyo hazipewi dawa kutoka bohari kuu.

Matokeo yake, zimeanza kushurutisha kwa wiki mbili  sasa, kwamba kila mgonjwa anayelazwa kwenye wodi za hospitali hiyo, achangie Sh. 5,000 kwa siku na Sh. 2,000 kwa chakula.

Sharti hilo ambalo tayari limeanza kuwaumiza wananchi wasiokuwa na uwezo kifedha na wametoa malalamiko yao kwa MwanaHALISI Online, ni jipya, kwa kuwa hapo kabla, mgonjwa alitakiwa kulipa Sh. 20,000 kwa muda wote anaolazwa Muhimbili, akihakikishiwa kupata chakula na malazi.

Uongozi wa Muhimbili umetangaza kwamba umelazimika kuongeza gharama za huduma kwa wagonjwa, kutokana na kukabiliwa na deni la Sh. 102 bilioni na Bohari Kuu ya Madawa nchini – Medical Store Department (MSD), asasi ya serikali inayoendeshwa kwa fedha za umma.

Ukosefu wa dawa kwa sababu Bohari Kuu haitoi tena dawa kwa Muhimbili mpaka kwanza ilipwe deni hilo, unazidisha tatizo la uduni wa huduma za tiba nchini.

Awali, uhaba wa dawa umekuwa ukiendana na ukosefu wa vifaa tiba muhimu, kama vile vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa, pamoja na watenda kazi.

Kutokana na tatizo hilo, linaloathiri sana maendeleo ya wanawake na watoto nchini, asasi ya SIKIKA inayopigania huduma bora za jamii, hususan afya, imekuja juu ikitaka serikali ichukuwe hatua za haraka kurekebisha tatizo liliopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa SIKIKA, Irenei Kiria amesema ni muhimu serikali ikatimiza ahadi yake ya kibajeti ya kutoa Sh. 70.5 bilioni ili kuondoa tatizo.

“Serikali iliahidi katika bajeti kutoa Sh. 70.5 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Lakini takwimu zinazonesha ni Sh. 45 bilioni tu ndizo ilizotoa kwa Wizara ya Afya. Tatizo zaidi ni kwamba Wizara ya Afya ilishindwa kusimamia ununuzi wa dawa ndio maana ni Sh. 7 bilioni tu kati ya hizo zilizotolewa, zilitumika kweli kwenye ununuzi wa dawa,” amesema mtendaji wa SIKIKA.

Amesema kwamba lipo tatizo kubwa la matumizi mabaya ya fedha za umma zinazokusudiwa kununulia dawa na vifaa tiba.

“Bajeti ya afya ni finyu, wakati mahitaji halisi ya mwaka wa fedha ni Sh. 500 bilioni, serikali ilipanga kutoa Sh. 70.5 bilioni kwa mwaka 2013/14, lakini hata hizo hazikutolewa kamili… kuna ubadhirifu unaolelewa na serikali kwa sababu lazima ieleweke fedha nyingine zimekwenda wapi?”

Akielezea matokeo ya uchunguzi walioufanya SIKIKA, Kiria amesema Wizara pekee inadaiwa Sh. 102 bilioni na Bohari Kuu ya Madawa, deni linalotokana na gharama ya ugomboaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba.

Sehemu ya deni ni la vituo vya afya nchini kote pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenyewe inayodaiwa peke yake Sh. 8 bilioni. SIKIKA inasema Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ambako wana mradi wa ufuatiliaji ubora wa huduma, inadaiwa Sh. 38 milioni.

Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesh ambaye ameibuka baada ya malalamiko kutokea dhidi ya hatua ya uongozi kuongeza gharama za huduma, amesema hakuna njia nyingine ya kuwezesha hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma isipokuwa kuongeza gharama ili ipate uwezo wa kulipa deni.

Deni la Bohari Kuu ya Madawa limewazindua viongozi wa Wizara ya Fedha ambako Waziri Saada Mkuya anasema tatizo hilo limechangiwa sana na ubadhirifu ndani ya Wizara ya Afya.

Japokuwa ameahidi serikali kuchukuwa hatua kupata ufumbuzi, Waziri Saada alisema deni litalipwa kwa awamu, na siyo kama inavyofikiriwa.

Suala hilo pia limemsukuma kutoa kauli Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akisema, “Kabla hawajaja kuomba fedha nyingine, watupe mchanganuo wa matumizi yaliyopita. Tunazo taarifa kuwa fedha zimetumika tofauti na lengo na kuzidisha tatizo hili.”

Ongezeko la gharama za huduma Muhimbili limeathiri zaidi wananchi wasiokuwemo katika mfumo wa bima za afya na hata waliomo lakini wakishiriki kwa viwango vidogo vya fedha wanazokatwa kwenye mishahara yao kila mwezi.

MwanaHALISI Online limeelezwa na mkazi wa jijini Mwanza, aliyeleta mgonjwa wake Muhimbili, kwamba “Mgonjwa wangu hana bima kwa hivyo imekuwa shida. Sioni dalili ya kutoka leo wala kesho maana hata ndugu sina.”

error: Content is protected !!