May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hospitali ya Rorya kuanza upasuaji Desemba 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Festo Dugange

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imesema, Hospitali ya Halmashauri ya Rorya mkoani Mara, inatarajiwa kuanza kazi rasmi mwezi Desemba 2021. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 31 Mei 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Festo Dugange, akimjibu Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege, aliyehoji lini hospitali hiyo itaanza kutoa huduma.

Akijibu swali hilo, Dk. Dugange amesema hospitali hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma za upasuaji wa dharula na kulaza wagonjwa, ifikapo Desemba 2021, baada ya ujenzi wa majengo yanayotoa huduma hizo kukamilika.

“Hospitali ya Halamashauri ya Rorya, inatarajiwa kuanza kutoa huduma za upasuaji wa dharula na kulaza wagonjwa, ifikapoDisemba 2021,” amesema Dk. Dugange.

Dk. Dugange amesema, Serikali inaendelea na ujenzi wa majengo hayo, ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, imetenga Sh. 800 milioni, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wake.

Pia, Dk. Dugange amesema, kwa mwaka wa fedha wa 2020/21, Serikali ilitoa Sh. 500 milioni , kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya hospitali hiyo.

“Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/21 Serikali imetenga Sh. 500 milioni, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imetenga Sh. 800 milioni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi,” amesema Dk. Dugange.

Dk. Dugange amesema, kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma ya wagonjwa wa nje, baada ya majengo saba kati ya tisa yaliyokuwa yanajengwa, kukamilika Juni 2020.

“Serikali imeendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, ambapo kati ya mwaka wa fedha 2018/2019 hadi 2020/2021, Serikali imeipatia Sh. 2.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa wodi tisa,” amesema Dk. Dugange na kuongeza:

“Na shughuli za ujenzi zinaendelea, ambapo ujenzi wa majengo saba ya awali umekamilika na tangu Juni 2020, inatoa huduma ya wagonjwa wa nje,” amesema Dk. Dugange.

error: Content is protected !!