October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Hospitali ya Manipal yaanzisha teknolojia mpya ya matibabu, Tamwa yapongeza

Spread the love

 

HOSPITALI ya Manipal kutoka nchini India kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), wameendesha mafunzo kwa wanahabari kuhusu teknolojia mpya ya mionzi ya matibabu ya saratani (Radixact System with Synchrony Technology). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mafunzo hayo yamefanyika hivi karibuni kwa njia ya mtandao na kuhudhuriwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Afrika ikiwemo Tanzania na wataalamu wa Hospitali za Manipal.

Mshauri wa Masuala ya Matibabu ya Magonjwa ya Saratani kwa kutumia mionzi, kutoka Hospitali za Manipal, Dk. Vadhiraja B M, alisema teknolojia hiyo mpya inasaidia kutibu watu wenye saratani ya kichwa, shingo, matiti, kibofu, kongosho na mapafu.

“Hospitali za Manipal zimekuwa zikijikita kuwapa matibabau bora zaidi wagonjwa, zinazopatikana ulimwenguni. Teknolojia hii inatarajia kuleta mabadiliko kwenye matibabu ya saratani kwa kupunguza usumbufu wanaoupata wagonjwa,” alisema Dk. Vadhiraja.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben

Dk. Vadhiraja alisema, timu ya wataalamu wa matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi ya hospitali hiyo, wamemtibu mgonjwa wa kwanza nchini India, aliyekuwa na uvimbe kwenye mapafu kwa kutumia teknolojia na mfumo huo mpya.

Alisema, teknolojia hiyo ina uwezo wa kufuatilia uvimbe katika mapafu kwa haraka, ambao huondoka wakati mgonjwa anapumua.

Alisema teknolojia hiyo mpya inapunguza matumizi ya mionzi kwenye mapafu, pamoja na kuharibu seli za saratani. Pia, teknolojia hiyo inapunguza muda wa matibabu, ikilinganishwa na matibabu ya mionzi ya zamani.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben aliishukuru hospitali hiyo kwa kuanzisha teknolojia hiyo, ambayo ni sahihi kwa wagonjwa wa saratani.

“Teknolojia hii itatumika kuendesha ubunifu na kuboresha maisha ya wagonjwa wa saratani. Teknolojia ya mfumo wa Radixact ni ya kwanza na ya aina yake nchini India,” alisema Rose.

error: Content is protected !!