Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hoja 5 zilizofanya Bunge limpongeze Spika Ndugai
Habari za Siasa

Hoja 5 zilizofanya Bunge limpongeze Spika Ndugai

Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge Tanzania
Spread the love

CHARLES Kitwanga, Mbunge wa Misungwi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewasilisha bungeni azimio la kumpongeza Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea)

Azimio hilo limesomwa leo Jumatatu tarehe 8 Juni 2020 bungeni jijini Dodoma na Kitwanga ikiwa ni siku chache zimebaki kuhitimishwa kwa Bunge hilo la 11 lililozinduliwa tarehe 20 Nobemba 2015 na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Kwa mujibu wa ritiba, Bunge hilo litahitimishwa tarehe 19 Juni 2020. Ndugai alikuwa Spika akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Anne Makinda.

Wakati azimio hilo lililosomwa na Kitwanga, kiti cha Spika kilikuwa kimekaliwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson. Azimio hilo ni hili hapa;

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 54 (1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha Bunge la Kumi na Moja kupata mafanikio tunayojivunia sisi sote.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kukushuru kwa kunipatia fursa hii adhimu ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu hoja hii inayotambua weledi, maarifa, ubunifu, uzalendo na juhudi zako zilizopelekea Bunge la Kumi na Moja kupata mafanikio tunayojivunia sisi sote.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie dakika moja kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano aliotupatia sisi Wabunge katika kutekeleza majukumu yetu lakini pia kwa uongozi wake thabiti na wenye maono uliowezesha kupata mafanikio tunayojivunia kama nchi.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiofichika kwamba huwezi kuelezea mafanikio tuliyoyapata kama nchi bila kumtaja Jemedari wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia ni ukweli usiofichika kwamba huwezi kuzungumzia mafanikio hayo bila kutaja mchango wa Bunge lako Tukufu. Hali kadhalika, huwezi kutaja mafanikio hayo bila kutaja jina la Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema nimewiwa kuwasilisha Azimio hili kwa sababu kubwa moja. Sababu yenyewe ni kutambua mchango wako katika maendeleo ya Taifa hili yaliyopatikana katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano hatuwezi kuacha kuzungumzia mchango wako wa kuliongoza Bunge hili kupitisha Miswada ya Sheria mbalimbali na Bajeti za Serikali zilizopelekea kupata mafanikio tunayojivunia leo.

Mheshimiwa Spika, nani asiyejua kwamba Bajeti za kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo kama vile Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge kotoka Dar es salaam hadi Dodoma zilipitishwa na Bunge lako Tukufu.

Nani asiyejua Bajeti ya kujenga Vituo vya Afya kila Kata na Hospitali za Wilaya 67 nchi nzima ilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Vile vile, nani asiyejua kama Bajeti ya mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa zaidi ya Megawatts 2,115 la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilipitishwa na Bunge lako Tukufu.

Kama vile haitoshi nani asiyejua Bajeti za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara, maji, bandari, meli, madarasa, maabara n.k zilipitishwa na Bunge lako Tukufu. Lakini kubwa zaidi nani asiyejua kuwa Sheria ya kuitamka Dodoma kuwa Makuu ya Nchi pamoja na Bajeti ya kugharamia ujenzi wa miundombinu na Ofisi mbalimbali za Serikali na kuwezesha Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma ilipitishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba Bunge lako Tukufu limefanya mambo mengi ya kujivunia katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano. Bila utayari na ushirikiano wa Bunge lako Tukufu kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pengine mafanikio tunayojivunia leo ingekuwa vigumu kuyafikia.

Mheshimiwa Spika, mbali ya kufanikisha matokeo hayo ya Serikali ya Awamu ya Tano, pia umekuwa kiongozi mwenye maono, ubunifu, weledi, msimamo na ushawishi wa hali ya juu katika kuongoza uendeshaji wa Bunge letu Tukufu. Katika kipindi chako tumeshuhudia mabadiliko mengi ya kifalsafa, kimiundombinu na kiteknolojia, ambayo yamewezesha Bunge la Kumi na Moja kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, mambo uliyoyafanya katika kipindi chako ni mengi sana lakini naomba nitaje machache ambayo yamenifanya niwiwe kuwasilisha Azimio hili.

Mosi, Kubuni wazo la Bunge Mtandao (e-Parliament)

Mheshimiwa Spika, ni katika kipindi chako Wabunge tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa Bunge letu Tukufu. Umetutoa kwenye ujima wa Bunge analogia (analogy) na kutuleta katika 3 utandawazi wa Bunge Mtandao. Umetuwezesha Wabunge kupata vishikwambi (Tablets) ambazo tunatumia katika shughuli mbalimbali za kibunge.

Sasa Wabunge ni mwendo wa kubofya tu, hakuna tena makaratasi. Jambo la kushangaza na la kujivunia zaidi ni kwamba Mfumo wa Bunge Mtandao (e-parliament) umebuniwa na watumishi wa Bunge na kupata msaada wa kiufundi kutoka kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba matumizi ya Bunge Mtandao yatapunguza sana gharama za manunuzi ya karatasi na wino wa kuchapisha nyaraka mbalimbali za Bunge zinazozalishwa na Ofisi ya Bunge, Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya shughuli za Bunge.

Mathalani nimeelezwa kuwa Ofisi ya Bunge inatarajia kuokoa zaidi Shilingi Bilioni 4 kwa mwaka baada ya kuanza kutumia Bunge Mtandao.

Aidha, nimeelezwa kwamba inakadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zinatarajiwa kuokolewa kutoka kwenye matumizi ya Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kutokana na matumizi ya Bunge Mtandao ambapo sasa Wizara na Taasisi za Serikali zimepunguza matumizi hayo kwa zaidi ya 90% ya uzalishaji wa nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa Bungeni badala yake wanawasilisha nakala mango (hard copies) chache kwa ajili kumbukumbu na nakala tete (soft copy) kwa ajili ya matumizi ya Waheshimiwa Wabunge na Sekretarieti ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, mbali ya faida zitakazopatikana kwa kutumia Bunge Mtandao, lakini pia umetufanya wabunge tuwe wa kisasa zaidi na kufikiri kisasa zaidi.

Pili, Kupunguza matumizi yasiyo ya lazima

Mheshimiwa Spika, katika kumsaidia Rais wetu kutimiza ndoto yake ya kuleta maendeleo ya kweli katika nchi yetu, Bunge lako Tukufu likiongozwa na wewe Mheshimiwa Spika lilikubali kubana matumizi yake kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama vile kupunguza safari zisizo za lazima nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kuthibitisha hilo, nimefanya utafiti mdogo na kubaini kuwa Bajeti ya mwisho ya Bunge la Kumi yaani Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/2016 ilikuwa takribani Shilingi Bilioni 173.77 wakati Bajeti ya Mwisho ya Bunge la Kumi na Moja unaloliongoza wewe Mheshimiwa Spika yaani Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/2021 ni Shilingi Bilioni 121.79.

Kwa takwimu hizo utagundua kwamba Bunge lako Tukufu limeweza kubana matumizi na kuokoa fedha za umma takribani Shilingi Bilioni 51.98 kila mwaka ambazo zimekwenda kutumika kugharamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya tano.

Tatu, Kuongezeka kwa Ofisi na Kumbi za Mikutano

Mheshimiwa Spika, kabla ya Bunge hili la Kumi na Moja, Ofisi ya Bunge imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa Kumbi za kufanyia vikao vya Kamati na vyumba vya ofisi za watumishi wa Ofisi ya Bunge.

Kwa sasa changamoto hiyo imekuwa historia kwa sababu ubunifu na jitihada zako zimewezesha ofisi ya Bunge kukamilisha ujenzi wa Jengo la Utawala Annex ambalo lina kumbi tisa (9) za mikutano zinazotumiwa na Kamati za Kudumu za Bunge, vyumba vya ofisi vinavyotumiwa na watumishi wa Idara ya Kamati za Bunge, Sehemu ya Milki na Majengo na Sehemu ya Uchapishaji.

Vile vile, Jengo hilo lina sehemu ya kutolea huduma ya chakula (Canteen), huduma za kibenki (Tawi la Benki ya NMB na CRDB), huduma za afya (Kituo cha Afya cha Bunge). Huduma hizo ni muhimu na zimerahisisha sana maisha ya waheshimiwa wabunge wanapokuwa hapa Bungeni.

Halikadhalika, umefanikisha kupatikana kwa kumbi nyingine mbili katika Jengo la Msekwa (Msekwa D na Msekwa C) na Kumbi mbili katika Jengo kuu la Utawala (Ukumbi na 9 na 231).

Aidha, tunaona kuna ujenzi unaoendelea katika Jengo kuu la Utawala ambapo nimeelezwa kuwa inaongezwa Sakafu ya tano (5 th Floor) ambayo itakuwa na Ukumbi mkubwa mmoja wenye uwezo wa kubeba watu 200 kwa wakati mmoja, kumbi ndogo nne na vyumba vya ofisi sita.

Mheshimiwa Spika, ongezeko la kumbi za mikutano ndani ya maeneo ya Bunge limesaidia kuondoa kabisa gharama ambazo zilikuwa zinatumika kukodi kumbi za mikutano wakati wa vikao vya Kamati.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi Milioni 120 kila mwaka sawa na Shilingi Milioni 600 kwa miaka mitano zimeokolewa baada ya Bunge kuanza kutumia kumbi zilizopo katika majengo niliyoyataja.

Nne, Maboresho ya Miundombinu

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo sisi kama Bunge tunajivunia ni maboresho ya miundombinu mbalimbali ya Ofisi ya Bunge. Katika kipindi cha Bunge la Kumi na Moja tumeshuhudia ujenzi wa Lift katika Jengo Kuu la Utawala na Jengo la Utawala Annex.

Ujenzi wa Lift hizo umeondoa adha ya waheshimiwa Wabunge na kupata na kuwawezesha huduma za kiofisi kwa urahisi zaidi.

Huko nyuma Mbunge alikuwa analazimika kupanda ngazi hadi ghorofa ya nne jengo la Utawala jambo ambalo lilikuwa ni adha kubwa kwa wabunge na wageni wanaotembelea ofisi ya Bunge. Lakini sasa aaaah mambo safi hakuna tena kupanda ngazi ni mwendo wa kuteleza tu.

Tano, Kulinda hadhi, staha na taswira ya Bunge

Mheshimiwa Spika, Bunge la Kumi na Moja ndo Bunge lenye idadi kubwa ya wabunge vijana na wabunge kutoka vyama vya upinzani kuliko kipindi chochote cha historia ya nchi yetu.

Hivyo, kwa vyovyote vile uendeshaji wa Bunge lenye mchanganyiko wa namna hiyo unahitaji kiongozi shupavu, msimamo thabiti, hekima, busara, maono, msikivu na mwenye kufanya maamuzi magumu.

Mheshimiwa Spika, bila kumung’unya maneno kiongozi wa Bunge mwenye sifa hizo ni wewe, kwa sababu katika kipindi chako tumeshuhudia namna ambavyo umepambana kulinda hadhi, staha na taswira ya Bunge.

Kwa kipindi chote umesimamia nidhamu na utulivu wa Bunge na kuhakikisha kuwa Bunge linatekeleza majukumu yake kwa kufuata demokrasia, uwazi na uzalendo kwa nchi yetu.

Wote waliojaribu kudharau mamlaka ya Bunge na kushusha hadhi ya Bunge ulishughulika nao kikamilifu.

Hivi sasa tunaelekea kumaliza kipindi cha uhai wa Bunge, tukiliacha Bunge letu likiwa na hadhi na heshma, inayostahili. Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Bunge la Kumi na Moja ni mengi sana siwezi kuyasema yote.

Lakini Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuzungumzia hayo yote bila kutambua mchango wa Naibu Spika wako na Sekretarieti ya Ofisi ya Bunge ikiongozwa na Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai ambayo imewezesha Bunge kupata mafanikio hayo chini ya uongozi wako.

Hakika tunajivunia kuwa na Sekretarieti makini, yenye weledi, maarifa, ubunifu, uzalendo na juhudi ya kufanya kazi kama hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa niwasilishe Azimio la Bunge la kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mafanikio ya Bunge hili la Kumi na Moja:-

KWA KUWA, Bunge chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano,

NA KWA KUWA, Bunge la Kumi na Moja limeendeshwa kwa ubunifu na viwango vya hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika uendeshaji wa Shughuli zake,

NA KWA KUWA, Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) amechangia kubuni wazo la kubadilisha mfumo wa uendeshaji Bunge kutoka Bunge analogia (analogy) na kwenda kwenye mfumo wa Bunge Mtandao (e-parliament),

NA KWA KUWA, mfumo huo utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa Bunge na Serikali kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kwa mwaka na kurahisisha uendeshaji wa Shughuli za Bunge;

NA KWA KUWA, katika kumsaidia Rais wetu kutimiza ndoto yake ya kuleta maendeleo ya kweli katika nchi yetu, Bunge la Kumi na Moja likiongozwa na Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb), lilikubali kubana matumizi yake kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama vile kupunguza safari zisizo za lazima nje ya nchi kwa Wabunge na Watumishi wa Bunge;

NA KWA KUWA, hatua hiyo imesaidia kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 50 kila mwaka fedha ambazo zimeekelezwa kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano;

NA KWA KUWA, Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) amechangia sana kukamilika kwa ujenzi wa Jengo la Utawala Annex na kuanzisha Ujenzi wa Sakafu ya tano (5 th Floor) katika jengo Kuu la Utawala hatua ambayo imesaidia kuongeza kumbi za mikutano ndani ya maeneo ya Bunge.

NA KWA KUWA, ongezeko la Kumbi limesaidia kuondoa kabisa gharama ambazo zilikuwa zinatumika kukodi kumbi za mikutano wakati wa vikao vya Kamati.

NA KWA KUWA, inakadiriwa kuwa ziadi ya Shilingi Milioni 120 kila mwaka sawa na Shilingi Milioni 600 kwa miaka mitano zimeokolewa baada ya Bunge kuanza kutumia kumbi zake zilizopo katika majengo niliyoyataja.

NA KWA KUWA, Katika kipindi cha Bunge la Kumi na Moja tumeshuhudia ujenzi wa Lift katika Jengo Kuu la Utawala na Jengo la Utawala Annex zimeondoa adha ya Waheshimiwa Wabunge na kuwawezesha kupata huduma za kiofisi kwa urahisi zaidi,

NA KWA KUWA, kwa kipindi chote Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) amesimamia nidhamu na utulivu wa Bunge na kuhakikisha kuwa Bunge linatekeleza majukumu yake kwa kufuata demokrasia, uwazi na uzalendo kwa nchi yetu,

NA KWA KUWA, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai amefanikisha kulinda hadhi na heshma ya Bunge letu kwa wivu na kulifanya kubaki na hadhi linayostahili,

KWA HIYO BASI, katika kutambua jitihada, ubunifu, uzalendo na mchango wa Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwezesha Bunge na Taifa kupata mafanikio niliyoyaeleza ikiwa ni pamoja na kubuni na kuanzisha mfumo wa Bunge mtandao (e-parliament), kufanikisha ujenzi wa kumbi za mikutano ya Kamati, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Bunge, kuboresha miundombinu kama vile kuweka Lift katika majengo ya utawala na kulinda na kuhifadhi hadhi na heshima ya Bunge, Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wake wa Kumi na Tisa Kikao cha Arobaini cha tarehe 8 Juni, 2020 linaazimia kumpongeza Spika Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb) kwa mchango wake katika Mafanikio ya Bunge la Kumi na Moja. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!