Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari Hofu yatanda Ngorongoro, madiwani wahojiwa CCM
HabariTangulizi

Hofu yatanda Ngorongoro, madiwani wahojiwa CCM

Baraza la Madiwani Ngorongoro
Spread the love

 

HOFU imetanda kwa madiwani na watetezi wa haki za binadamu waishio kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, baada ya baadhi ya madiwani kuhojiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na Polisi, kwa tuhuma za kuhamasisha wananchi wasiondoke hifadhini hapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Leopold Mosha iliyotolewa jana Jumatano, tarehe 23 Machi 2022, watetezi wa haki za binadamu na madiwani wa Kata ya Sale na Loliondo, wanasakwa na Jeshi la Polisi, kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma hizo.

Taarifa ya Mosha imedai kuwa, Diwani wa Kata ya Malambo, Joel Clemence na wa Kata ya Arash, Mathew Siloma, jana wamehojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM Wilaya ya Ngorongoro, kwa tuhuma za kutetea wananchi wa kata zao kutohamishwa katikahifadhi hiyo.

Mbali na madai ya madiwani hao kuhojiwa, taarifa ya Mosha imedai, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wafugaji waishio Ngorongoro, Robert Kamakia na Mfanyakazi wa Shirika la Kutetea Haki za Jamii ya Watu Asilia wilayani humo, waliitwa kuhojiwa katika Kituo cha Polisi cha Kati Arusha.

“Mtandao unatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufuata taratibu zilizopo kisheria endapo kuna uhitaji wa watetezi wa haki za binadamu kukamatwa na sio utaratibu unaotumika sasa wa kuwasaka,” imesema taarifa ya Mosha.

Kufuatia taarifa hizo, MwanaHALISI Online imemtafuta kwa simu Clemence kwa ajili ya kuthibitisha, ambaye amekiri kwamba yeye na wenzake wawili, walihojiwa jana na kamati hiyo ya CCM wilaya ya Ngorongoro.

Amedai, alihojiwa kufuatia kauli zinazodaiwa kuwa alizitoa kwenye mkutano wa wananchi uliofanyika tarehe 19 Machi mwaka huu, ikiwemo iliyosema “Serikali haichukui ardhi yetu hata siku moja na wala haitachukua uhai wetu”

Kauli nyingine ni “hatuhami kuelekea kwenye wilaya nyingine yoyote. Hatutaruhusu kuweko bikoni mahali popote na itakapowekwa tunang’oa muda huo huo. Tunamwambia Waziri Mkuu hatuna makosa yoyote.

“Tulihojiwa kwa tuhuma za kuhamasisha wananchi wasihame, lakini hizi kauli tulizitoa baada ya wananchi wetu kutuuliza je mlienda kukubaliana na Waziri Mkuu kuweka bikoni, sisi tukawaambia wananchi hatujakubaliana imesemwa uongo,” amesema Clemence.

Diwani huyo amedai, maagizo ya wao kuhojiwa yalitoka kwa Katibu Mkuu wa CCM Arusha, Mussa Matoroka.

Aidha, Clemence amedai, diwani mwenzake, Siloma, baada ya kuhojiwa na CCM, alikamatwa na Jeshi la Polisi Loliondo, kisha akahamishiwa Kituo cha Polisi cha Kati Arusha, ambako anashikiliwa hadi leo.

“Bado yuko ndani na mimi walinitafuta jana wakanikosa. Ila suala la mwenzetu bado linashughulikiwa,” amesema Clemence.

Mtandao huu ulimtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Arusha, ACP Justine Masejo, kwa ajili ya ufafanuzi wa tuhuma za kumshikilia diwani huyo, ambapo simu yake iliita bila kupokewa.

Alipotafutwa Matoroka, kwa ajili ya ufafanuzi wa taarifa za chama chake kuwahoji madiwani hao alijibu akidai hana taarifa hizo.

“Mimi sina hizo taarifa kama walihojiwa na kamati ya maadili ya wilaya, sababu mimi niko mkoa. Ungewauliza wenyewe watu wa Ngorongoro,” amesema Matoroka.

MwanaHALISI Online ilimtafuta kwa simu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, kwa ajili ya ufafanuzi huo tangu majira ya asubuhi, alijibu akisema yuko kwenye kikao.

Tangu sakata hilo liibuke, Mongella alisema Serikali haitatumia nguvu kuwaondoa wananchi katika hifadhi hiyo, huku akiahidi kwamba mtu atakayetumia nguvu kuwalazimisha wananchi kuchukua hatua hiyo, atachukuliwa hatua.

Mongella alisema, Serikali itafuata misingi ya kisheria na utawala bora, katika kuwahamisha wananchi hao, ambapo imeshaanda mazingira ya kuwahamisha wanaotaka kuhama kwa hiari.

1 Comment

  • Wanangorongoro kwakweli hatupo tayari kuganyishwa Kwa umoja wetu iliyotamalaki kila ukoo itapotea Mara moja tu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Mo Dewji achomoza bilionea pekee Afrika Mashariki

Spread the loveMAZINGIRA mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania yamezidi kuleta matunda baada...

Habari MchanganyikoTangulizi

Bilioni 213 za miradi ya DMDP zaistawisha Temeke

Spread the loveJUMLA ya Sh bilioni 213 zimetumika kuboresha sekta ya afya,...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Bashiru aibuka na bei za vyakula, “Njaa inadhalilisha nchi”

Spread the loveMBUNGE wa kuteuliwa na Rais, Dk. Bashiru Ally, ameitaka Serikali...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ahoji fedha za Plea-Bargaining

Spread the love  RAIS Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya kuangalia namna...

error: Content is protected !!