July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Hofu ya vurugu 100%

Spread the love

TAIFA lipo njiapanda. Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ‘kuasisi’ mvutano usio wa lazima, anaandika Dany Tibason.

Pande mbili zinaumana; moja ikiwa ni serikali inayoendeshwa na CCM ambapo upande wa pili ni vyama pinzani. Busara isipotumika, mwisho wake ni vurugu.

Serikali inaweka mashatri makali yaliyo nje ya Katiba kudhibiti harakati za kisiasa nchini, vyama vya upinzani vinagomea mashatri hayo. Hapo ndipo panapoibua mgogoro.

Kauli ya Rais John Magufuli ya kuwataka wabunge na madiwani wafanye mikutano ya kisiasa katika majimbo yao, imepingwa kila kukicha, wanaopinga wanaonya kwamba, vurugu na hata mauaji yanaweza kutokea.

Wapo wanaosema kinachomtesa Rais Magufuli ni woga, kupenda kusifiwa bila kukosolewa na wengine wanaeleza kwamba ‘si mwanasiasa’.

Akizungumza na mtandao huu katika mahojiano maalumu Kayumbo Kabutali, Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) amesema, Rais Magufuli anatoa kauli za kupotosha ukweli juu ya uwepo wa vyama vingi vya siasa.

Mbali na upotoshaji huo amesema Rais Magufuli ni muoga “kitendo cha Rais Magufuli kuzuia mikutano ya siasa ni dalili za uoga.”

“Nafananisha na kitendo cha mtu mlevi anapotembea usiku hutishwa na visiki ambavyo huonekana kama mtu huku akichimba mkwara kwa visiki hivyo bila kujua kuwa, kiski hakiwezi kumfanya jambo lolote,” amesema na kuongeza;

“Siyo sahihi kudai kuwa, kila mbunge afanye mikutano katika jimbo lake au diwani afanye kazi katika kata yake bali matakwa ya kisheria ya mfumo wa vyama vingi, yanaruhusu shughuli za mikutano ya siasa na maandamano kufanywa na vyama vya siasa husika.

Amesema kuwa, lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola au kutetea dola na ili kiweze kushika dola, ni lazima kifanye mikutano ya kisiasa kwa lengo la kutoa ushawishi na kueleza mikakati na malengo ya chama husika.

“Sasa tujiulize, kama siasa zitazuiliwa, itakuwaje kwa vyama hivyo na wanachama wataongezekaje” amehoji na kuongeza;

“Pia Rais Magufuli arejee kauli yake katika Mkutano Mkuu wa CCM ambapo alisema kwamba, CCM inatakiwa kuongeza wanachama kufikia milioni nane. Je, wanachama hao atawaongezaje kama siyo kufanya mikutano ya kisiasa?”

Poul Loisulie, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma amesema, kitendo cha Rais Magufuli kuzuia mikutano na kuruhusu mikutano ya majimbo na kata ni kutaka kuligawa taifa kwa misingi ya ukabila.

Amesema, kutokana na kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, ni vyema Rais Magufuli awaache wanasiasa wafanye mikutano na wananchi wenyewe watafanya uchambuzi wa kisiasa.

Loisulie amesema, kauli ya Rais Magufuli inaweza kusababisha kuwepo kwa machafuko nchini na kutengeneza vita ya kikabila na mwisho wa siku, itafikia hatua kuwa mwana CCM na mwanachama wa chama kingine cha upinzani hawatashirikiana katika shughuli za maendeleo.

“Katiba inasema wazi kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi na kazi pekee ni kunadi sera zao leo hii ukizuia uwepo wa vyama vya siasa ni wazi kuwa vyama hivyo vitakufa.

“Ikumbukwe kuwa, kulikuwepo na malalamiko kuwa vyama vingi vinaibuka wakati wa uchaguzi lakini cha kushangaza leo hii wanasiasa wakitaka kuimarisha vyama hivyo, wanazuiwa. Kimsingi jambo hilo si sahihi na wala rais hatakiwi kutumia nguvu nyingi,” amesema.

 

error: Content is protected !!