YUDA Thaddaeus Ruwa’ichi, Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam nchini Tanzania, amewaomba waumini kuchukua tahadhari juu ya maambukizo ya virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Askofu Mkuu Ruwa’ichi ametoa ushauri huo hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kumbukumbu ya Wafia Dini katika Kituo cha Hija Pungu, jijini Dar es Salaam.
“Tusali na tujiombee sisi wenyewe, atulinde na janga la COVID-19. Hapa niseme kwamba COVID haijaisha…,kwa hiyo tusiende holela, tuwe makini na tujilinde,” alisema Askofu Ruwa’ichi na kuongeza:
“Ule utamaduni wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni uendelee, utamaduni wa barakoa tuliouacha wote, tuurudie tena, tujijali, tujipende, tujitunze, tushirikiane na Mungu katika kujilinda na tuendelee kuomba ulinzi kwa ajili yetu sote.”
Askofu Ruwa’ichi anaungana na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Aman aliyetoa andishi la kurasa mbili kwenda kwa mapadre, watawa na waamini walei akizungumzia janga la corona.
Katika andishi hilo alilolituma na kuagiza kusomwa Jumapili iliyopita ya tarehe 24 Januari 2021, Askofu Amani alisema, “…tusimjaribu Mungu kwa kufanya uzembe na maisha yetu. Turejee tahadhari za kuzuia maambukizi bila ya kuwa na hofu.”

Waraka wa Askofu Amani aliupa kichwa cha maneno kisemacho, “Kutembea Pekupeku Juu ya Mbigili.”
Amesema, watu wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa ugonjwa huo upo na unatesa mataifa mengi duniani.
“Maji ya kunawa kanisani yameondolewa, na pengine yapo lakini watu hawanawi tena kwa imani kwamba hakuna corona. Hata ile tahadhari ya kutoshikana mikono watu wamejiondolea wenyewe kwa imani kwamba, hakuna corona,” ameeleza.
Amesema, taifa linalazimika kutengeneza utamaduni mpya, huku akitahadharisha jamii inapaswa kutafakari upya kwa kuwa “mwenendo wake wa sasa, unatia mashaka.”
Askofu huyo amewataka mapadri na watawa kuchukua tahadhari, huku akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuchukua tahadhari kwa manufaa yake na wengine.
Jana Jumanne tarehe 26 Januari 2021, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga aliwaandikia barua Mwadhama, Mpelekwa wa Baba Mtakatifu, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Maaskofu Wastaafu akiwataka kuchukua tahadhari ya maambukizi mapya ya corona.

Nyaisonga ambaye ni Jimbo Kuu anasema, kuna wimbi jipya la maambukizo ya corona kufuatia nchi kadhaa kuthibitisha kupita kwenye kipindi kigumu cha kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.
Amesema “hatuna budi kujihami, kuchukua tahadhari na kumlilia Mungu kwa nguvu zaidi, ili janga hili lisitukumbe.”
Rais wa TEC, anazidi kueleza maaskofu wenzake, kwamba “kwa uhalisia huo, tusiache kuwashauri, kuwahimiza na kuwaongoza Taifa la Mungu katika mapambano haya dhidi ya virusi vya Korona.”
Leave a comment