MKURUGENZI wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Said, amesema watoto wadogo hawaathiriki sana na Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), kwa sababu wamepewa chanjo nyingi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Kanali Said amesema hayo leo Jumamosi, tarehe 7 Agosti 2021, akifungua warsha ya kuwajengea uwezo watetezi wa haki za binadamu, katika kukabiliana na maafa na majanga, mkoani Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Mkurugenzi huyo wa maafa amesema, mtoto hadi anafikisha umri wa miaka mitano, anakuwa amepata chanjo za aina tisa, ambazo zinamsaidia kutengeneza kinga za kukabiliana na magonjwa ikiwemo UVIKO-19.
“Wenzetu kina mama wakienda kujifungua wanapiga chanjo nyingi sana na watoto wakifika miaka mitano inatakiwa wapate chanjo tisa, ndiyo maana wana immunite (kinga) sana. Korona inaweza ikampata asitingishike. Atashika nini lakini mikono iko salama. Sababu amechanjwa chanjo ya kutosha,” amesema Kanali Said.
Kanali Saidi amesema, watu wazima kuanzia miaka 40 na kuendelea, wako katika hatari ya kuathirika na ugonjwa huo, kwa kuwa kinga zao za utotoni zinakuwa zimeisha nguvu.
“Kuanzia miaka 40 kwenda juu huko, wako katika hatari sababu chanjo ulizopata zimeisha nguvu,” amesema Kanali Said.
Kanali Said amewaomba Watanzania wapate chanjo ya ugonjwa wa Korona, ili wajikinge na maambukizi yake.
“Wimbi la sasa sio kama la mwanzo, ukasikia mtu anapiga chafya unamkwepa. Sasa hivi unaweza tembea kumbe una Korona, hujisikii kifua wala kukoa lakini wadudu unao wanaingia aidha kwa kutumia mdomo au kupumua hata kwa macho. Wakiingia wanapita kwenye mdomo na koo, wanajijenga wanashuka kwenye mapafu. Kwa nini usubiri mpaka ufike kote? Pata chanjo,” amesema Kanali Said.
Leave a comment