October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hivi ndivyo Trump anavyoiua Palestina

Spread the love

RAIS wa Marekani, Donald Trump anataka dunia itambue, kwamba anashughulika kutatua mgogoro kati ya Israel na Palestina. Anaandika Mwandishi Wetu… (endelea).

Harakati na juhudi zake zinakinzana wazi na kile anachokitambulisha kwenye uso wa dunia, anataka amani asubuhi, jioni anapinduka na kukaa uapande mmoja dhidi ya upande mwingine.

Bila shaka, Trump mpaka atapoondoka madarakani, atakuwa ametengeneza zaidi mgogoro kati ya Israel na Palestina kuliko kuutatua, ni kwa kuwa analenga kuikandamiza Palestina na kuinawisirisha Israel.

Hatua anazochukua Trump zinadhishirsha dhamira yake ya kuiangamiza Palestina; Novemba 2017, Trump akiongozana na mkwewe, Jared Kushner waliandaa kile kilichoitwa ‘Mpango wa Amani’ wa kumaliza mzozo uliopo kwenye mataifa hayo.

Hakuna chochote kilichoibua matumaini kwenye mpango huo, na badala yake Desemba 2017, utawala wa Trump uliongeza mgogoro kwa kuutambua Mji wa Yerusalemu kama Mji Mkuu wa Israeli. Hili lilikuwa pigo kubwa kwa Palestina na wapenda Amani.

Katika kuonesha dhamira hiyo, Marekani ilihamishia ubalozi wake mjini humo. Trump hakujali kwamba, anachokifanya ni kinyume na sheria za kimataifa.

Trump akasonga mbele, uongozi wake ukafunga ofisi za uwakilishi za Palestina zilizokuwepo jijini Washington. Hatua hiyo haikumtosha, Trump akashinikiza kukata misaada yote iliyokua ikitoa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).

Trump na dhamira yake ya kuimarisha Israel, Machi 2019 aliamua kuitambua milima ya Golan (mali ya Syria) iliyoporwa na Israel 1967, kwamba sasa ni ardhi ya Israel.

Safari ya Trump kuidhoofisha Palestina imeendelea ambapo Novemba 2019, serikali yake ilieleza kutambua makazi haramu ya Israeli katika mjini West Bank.

Ardhi hiyo kabla ya kuvamiwa, ilikuwa chini ya mamlaka ya Wapalestina. Utambuzi huo unakinzana na sheria za kimataifa.

Januari 2020, Trump akaibuka na mpango mwingine wa amani, ambao umegomewa na Wapalestina na nchi za kiarabu.

Mji Yerusalemu

Mji wa Yerusalemu, ni mji mtakatibu katika Imani tatu za kidini; Uislam, Ukristo na Uyahudi. Mji huu unagombaniwa kutoka na historia yake kwenye imani ya dini hizo.

Kutokana na mzozo kumea, Palestina ilikubali Yerusalemu igawanywe, hivyo taifa hilo lingekuwa na mji mkuu wake mashariki mwa Yerusalemu.

Lakini mpango wa Trump unasema, mji wote na maeneo yote matakatifu na nyumba za Wapalestina (zaidi ya 300,000), ni mali katika mji mkuu wa Israeli.

Mpango huu wa Trump unawataka Wapalestina kuunda mji wao mkuu nje ya mji wa Yerusalemu, na kuamua kuuita jina lolote ikiwa ni pamoja na Al Quds, yaani Yerusalemu.

Msikiti wa Al-Aqsa, ni mahali wanapofanya ibada Waislam. Katika Imani ya dini hiyo, pale Aqsa ndio mahali penye nafasi ya tatu kwa utakatifu.

Mwaka 1967, Israeli na nchi ya Yordani, walisaini makubaliano yaliyoiweka Yordani kama ‘msimamizi’ rasmi wa Msikiti wa Al-Aqsa.

Pamoja na hivyo, Israeli imejaribu kubadilisha hali ya msikiti huo kwa kuuvamia mara kwa mara huku wakisindikizwa na polisi. Uvamizi huo umeenda sambamba na kufanya swala za kiyahui kwenye msikiti huo kimabavu.

Mpango wa Trump unaruhusu Wayahudi kutumia msikiti wa Al-Aqsa kinyume na makubaliano ya mwaka 1967, na pia umeweka vizuizi vya Waislamu kusali katika msikiti huo.

Mpango wa amani wa Trump pia unaruhusu dini nyingine kuingia katika msikiti huo, na kufanya ibada kulingana na imani nje ya Uislam.

Mipaka na uhuru

Mpango wa amani wa Trump unaipa Israeli udhibiti juu ya mipaka yote, hata juu ya mipaka ya nchi mpya ya Palestina.

Mpango huu umeangalia zaidi upande wa Israeli na kusema kwamba, haya yote ni kuhakikisha usalama kwa Israeli.

Kulingana na mpango huo, mipaka yote ikijumlisha viwanja vya ndege, bonde la Yordani, mtandao wa barabara katika nchi pendekezwa ya Palestina na hata njia itakayounganisha Palestina na Yordani, itakua chini ya udhibiti na uangalizi wa Israeli.

Mpango huo unaitaka Palestina kusimamisha hatua zote za mashtaka yake juu ya makosa ya Israeli, kwenye mahakama ya makosa ya jinai (ICC), kuhakikisha usalama wa raia wa Israeli na raia wa Marekani.

Kunyang’anya ardhi ya Paletina

Trump kwenye mpango wake, anaipa Israeli ishara ya kijani kunyang’anya archi zaidi kwenye maeneo ya Wapalestina pamoja na mjini West Bank, Bonde la Yordani (Jordan valley).

Pia kutangaza uhuru juu ya makazi haramu yote yaliyoko mjini humo, ambayo pia yatakua ndani ya nchi pendekezi ya Paletina.

Pia Israeli itakua na mamlaka ya kuingia na kutoka Palestina, na vile vile haki ya kuharibu chombo chochote ambacho kitatishia usalama wa nchi ya Israeli pamoja na wakazi wake.

Pia mpango umeeleza kwamba, makazi haramu ya Israel ambayo yatakuwa ndani ya nchi mpya pendekezwa (Palestina), yatakuwa chini ya usalama wa Israeli na hivyo basi, kuashiria uwepo wa vikosi vya Israeli katika Palestina.

Swala la Wakimbizi

Sheria ya kimataifa imeweka haki ya wakimbizi wa Palestina wanakadiriwa kuwa 6,000,000 kurejea kwenye maeneo yao ya asili waliofukuzwa na Israel (right to return), lakini mpango wa Trump umepinga haki hiyo.

Mpango wake (Trump) umeeleza, wakimbizi wachache wataingia Palestina, huku wengine watafyonzwa (watabaki) kwenye nchi walizopo sasa hivi, mfano Jordan lakini hawataruhusiwa kurudi kwenye makazi yao yanayokaliwa na Israel kimabavu.

Kwanini Palestina imegoma?

Shida kwenye mpango huo haipo tu katika maelezo, lakini pia katika dhana na misingi ambayo imejengwa juu yake ikiwemo ushabiki na ubaguzi wa Trump.

Mpango huo unaipendelea Israel, unachukua simulizi za Israeli na kuharibu tumaini la Wapalestina kuwa na nchi huru ndani ya mipaka ya mwaka 1967, huku Yerusalemu Mashariki ikiwa mji wake mkuu.

Mpango huu umeandaliwa na kufikiwa bila ushiriki katika ngazi yoyote ya upande wa Palestina. Mpango huu wa amani unaua ahadi zote za sheria za kimataifa kuhusiana na mgogoro wa Palestina na Israeli, pia maazimio ya Umoja wa Mataifa na wa Jumuiya ya Kimataifa.

Mpango huu pia hauna masharti makali ya utekelezaji kwa upande wa Israel, bali upande wa Palestina umepewa masharti magumu yasiyofikirika.

mpango huo pia hautambui watu wa Palestina kama taifa badala yake, inakataa utambulisho wa kitaifa wa Palestina na inapuuza haki za Wapalestina zinazotambuliwa kimataifa.

error: Content is protected !!