September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Hisabati’ za Simba na Yanga kuelekea Oktoba Mosi

Spread the love

 

KUELEKEA mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga katika Ligi Kuu soka Tanzania Bara, siku ya Oktoba Mosi mwaka huu utakaofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hizi ni dondoo fupi za kihistoria katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, anaandika Kelvin Mwaipungu.

Timu hizi mbili zenye upinzani mkubwa tangu zilipoanzishwa katika miaka ya 1935 kwa Yanga na Simba iliyoanzishwa mwaka 1936, zimejizolea mashabiki wengi ndani na nje ya nchi huku pambano baina yao likiwekwa katika orodha ya mapambano ya kuvutia zaidi kwa timu za Mji mmoja barani Afrika (derby).

Kuelekea pambano hili, Simba ina kumbukumbu ya kupata ushindi wa 4-0 katika mchezo wake wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Majimaji, na kufanya kuongoza wakiwa na alama 16, na Yanga wakiwa na alama 10 baada ya kupata kipigo cha 1-0 kutoka kwa Stand United ya Shinyanga

Hata hivyo Yanga ina mchezo mmoja mkononi.

Ushindi mkubwa zaidi ambao Simba imewahi kuupata dhidi ya Yanga ni mabao 6-0 mnamo mwaka 1977 ambapo kipigo kingine kizito zaidi ilichokitoa kwa Yanga ni 5-0, mnamo tarehe 6 Mei, 2012 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa.

Simba mara nyingi imekuwa ikitumia vyema madhaifu ya wapinzani wao, hasa wanapokuwa hawapo vizuri tofauti na Yanga, mathalani Oktoba 20, 2013 Yanga ingeweza kuifunga Simba mabao mengi katika baada ya kuongoza kwa mabao matatu katika kipindi cha kwanza lakini baadaye Simba walifanikiwa kusawazisha yote, na kufanya mchezo huo umalizika kwa sare.

Kwa miaka mitano iliyopita, timu hizi zimekutana mara 11 ikewemo katika mechi za ligi pamoja na michuano mingine. Simba imeibuka na ushindi mara nne huku Yanga ikishinda mara tatu na mara nne timu hizo zikienda sare.

Rekodi nzuri ya ambayo Yanga wanaweza kujivunia kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba ni ushindi ambao wamekuwa wakiupata kila timu hizo zinapokutana katika mwezi Oktoba.

Tarehe 16 Oktoba, 2010 Yanga iliifunga Simba bao 1-0 kwa bao la mshambuliaji Jeryson Tegete katika dakika ya 70. Ilikuwa katika mchezo wa ligi kuu uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Yanga ilifanya hivyo tena 29 Oktoba, 2011 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kwa kuifunga Simba bao 1-0 mfungaji akiwa ni Davis Mwape, katika dakika ya 75.

Oktoba 3, 2012 Simba ililazimisha sare ya bao 1-1, goli la Simba likifungwa na Amri Kiemba katika dakika ya tatu ya mchezo huo huku bao la kusawazisha la Yanga likifungwa na Said Bahanuzi katika dakika ya 64 kwa njia ya adhabu ya Penati.

Ushindi pekee walioupata Simba walipocheza na Yanga ndani ya mwezi Oktoba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ilikuwa ni Oktoba, 2013 ambapo iliifunga Yanga bao 1-0 lililofungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ katika dakika ya 26 ya mchezo huo.

Rekodi hizi kila Simba na Yanga zinapokutana katika mwezi Oktoba, zinaongeza mvuto katika mchezo huo wa watani wa jadi unaotarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi ya wiki hii (Oktoba Mosi).

 

error: Content is protected !!