Friday , 1 March 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Hili ndio chimbuko la uadui wa Israeel, Iran
Kimataifa

Hili ndio chimbuko la uadui wa Israeel, Iran

Spread the love

TANGU kufanyika kwa Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, ambapo viongozi wa kidini wenye msimamo mkali walichukua mamlaka na kumaliza utawala wa Kifalme wa Reza Shah Pahlavi, Iran imekuwa ikiitisha kuangamizwa kwa Israel. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Iran husema taifa la Israel halina haki zozote za kuwepo, kwa sababu liliundwa kwenye ardhi ambayo ilitekwa kutoka kwa Waislamu.

Israel hutazama Iran kama tishio kuu dhidi ya kuwepo kwake. Taifa hilo la Kiyahudi limekuwa likisisitiza kwamba, Iran haifai kuruhusiwa kuwa na silaha zozote za kinyuklia.

Viongozi wao wana wasiwasi kuhusu kuenea kwa ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati.

Israel imekuwa ikifuatilia matukio katika taifa jirani la Syria kwa wasiwasi tangu vita vilipozuka mwaka 2011. Israel imekuwa haishiriki katika vita hivyo kati ya serikali ya Bashar al-Assad na waasi.

Lakini Iran imeshiriki hasa katika vita hivyo ambapo imetuma maelfu ya wapiganaji na washauri wa kijeshi kusaidia wanajeshi wa Rais Assad.

Israel ina wasiwasi pia kwamba, Iran inajaribu kuwatuma wapiganaji na silaha kisiri nchini Lebanon – jirani wa Israel – ambayo pia huitishia Israel.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mara kwa mara amesisitiza kwamba, taifa lake halitairuhusu Iran ijenge kambi Syria ambazo zinaweza kutumiwa dhidi ya Israel.

Kwa hivyo, kadiri Iran ilivyoendelea kujiimarisha nchini Syria ndivyo Israel ilinavyozidisha mashambulio dhidi ya kambi na wanajeshi wa Iran huko.

Hapa. Iran kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono makundi yanayoishambulia Israel – kwa mfano Hezbollah wa Lebanon na kundi la Hamas la Palestina.

Lakini mataifa hayo mawili hayajawahi kupigana moja kwa moja na inakadiriwa kwamba, vita kama hivyo vinaweza kusababisha uharibifu mkubwa.

Iran ina shehena kubwa ya makombora ya masafa marefu na ina washirika walio na silaha kali pia wanaopakana na Israel.

Israel nayo ina jeshi lenye nguvu sana na inadaiwa kuwa na silaha za nyuklia. Aidha, Israel huungwa mkono kikamilifu na Marekani. Mataifa haya mawili yanachagizwa zaidi na maono tofauti kuhusu taifa la Palestina.

Palestina na Israel

Kumekuwepo na mzozo wa muda mrefu kuhusu udhibiti wa Mji wa Jerusalem kati ya Waisraeli na Wapalestina. Mji huo kwa sasa umegawanywa mara mbili, Jerusalem Mashariki na Jerusalem Magharibi.

Jerusalem ya Magharibi hutazamwa na Israel kama mji wake mkuu nayo Jerusalem Mashariki hutazamwa kuwa mji mkuu wa taifa la Wapalestina (litakapoundwa), ingawa eneo hilo bado kwa kiwango kikubwa limetawaliwa na Israel tangu vita vya 1967.

Tangu wakati wa vita hivyo, Israel imejengwa nyumba za walowezi wa Kiyahudi takriban 200,000 ambao huishi Jerusalem Mashariki, hatua iliyoshutumiwa na jamii ya kimataifa. Eneo hilo huishi Wapalestina takriban 370,000.

Israel ilitangaza 1980 Jerusalem yote kuwa mji wake mkuu wa milele, lakini nchi nyingi duniani hazikubali azimio hilo.

Hivyo basi, balozi za nchi za kigeni katika Israel ziko nje ya Jerusalem, katika Mji wa Tel Aviv isipokuwa Marekan kwa sasa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuutambua mji huo kama Mji Mkuu wa Israel.

Lakini ni kwa nini mji huu huzozaniwa hivyo? Dini tatu

Mji huu una umuhimu mkubwa kwa dini tatu kuu – Uislamu, Ukristo na Uyahudi. Dini zote tatu humuangazia Nabii Ibrahim anayetajwa kwenye Biblia na Qur’an kama mmoja wa waanzilishi au mababu wa imani.

Ni mji ambao umedhibitiwa na dini hizo kwa vipindi mbalimbali katika historia.

Kwa Kiebrania, mji wa Jerusalem hufahamika kama Yerushalayim na kwa Kiarabu al-Quds. Kwa Kiswahili, jina lake halisi ni Yerusalemu. Mji huo ni miongoni mwa miji ya kale zaidi ambayo ipo hadi sasa duniani.

Ni mji ambao umetekwa, ukabomolewa na kuharibiwa na kisha kujengwa tena. Kila sehemu ya ardhi yake ukichimba kwenda chini hufichua enzi fulani katika historia yake.

Ingawa umekuwa chanzo cha ubishi na mzozano kati ya dini mbalimbali, dini zote huungana kwa pamoja kuungama kwamba ni eneo takatifu.

Ndani yake kuna Mji Mkongwe, ambao una njia nyembamba, vichochoro na nyumba za kale. Kuna maeneo manne makuu na kila eneo, majengo huwa tofauti. Kuna eneo la Waislamu, Wakristo, Wayahudi na Waarmenia.

Eneo hilo huzungukwa na ukuta mkubwa wa mawe. hapo, kunapatikana baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa matakatifu zaidi duniani. Kila eneo kati ya maeneo hayo manne (unaweza kuyaita mitaa) huishi watu wa aina moja.

Wakristo wana maeneo mawili, kwa sababu Waarmenia pia ni Wakristo. Eneo lililotengewa Waarmenia, ambalo ndilo ndogo zaidi kati ya hao manne, lina vituo vya kale zaidi vya Waarmenia duniani.

Jamii ya Waarmenia imehifadhi utamaduni wake wa kipekee ndani ya Kanisa la St James na nyumba kubwa ya utawala. Maeneo hayo mawili yamechukua sehemu kubwa ya mtaa huo wa Waarmenia.

Msikiti
Mtaa wa Waislamu ndio mkubwa zaidi kati ya maeneo hayo manne na ndani yake kunapatikana madhabahu ya Dome of Rock (Kuba ya Mwamba) na Msikiti wa al-Aqsa kwenye eneo linalofahamika na Waislamu kama Haram al-Sharif, au Mahali/Hekalu Patakatifu.

Msikiti huo ndio eneo la tatu kwa utakatifu katika dini ya Kiislamu na husimamiwa na wakfu wa Kiislamu ambao hufahamika kwa Kiarabu kama Waqf.

Waislamu huamini kwamba, Mtume Muhammad (S.A.W) alisafiri kutoka hapo hadi Makka usiku na aliomba pamoja na roho za manabii wengine wote.

Hatua chache kutoka hapo kunapatikana Dome of the Rock (Kuba ya Mwamba) ambapo kuna jiwe la msingi. Waislamu huamini kwamba, ni kutoka hapo ambapo Mtume Muhammad S.A.W alipaa mbinguni.

Waislamu hutembelea eneo hilo takatifu kila wakati katika mwaka, lakini kila Ijumaa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, mamia ya malelfu ya Waislamu hufika kuomba kwenye msikiti huo.

Kanisa

Ndani ya mtaa wa Wakristo, kuna Kanisa Kuu la Kaburi na Ufufuo wa Yesu Kristo, ambalo ni muhimu sana kwa Wakristo kote duniani.

Hupatikana katika eneo ambalo lina umuhimu mkubwa katika kisa cha kusulubiwa, kufariki na kufufuka kwa Yesu.

Kwa mujibu wa utamaduni wa Kikristo, Yesu alisulubiwa hapo, katika Golgotha, au mlima wa Calvary. Kaburi lake linapatikana ndani ya kanisa hilo la kaburi na inaaminika kwamba hapo ndipo alipofufuka. Kanisa hilo husimamiwa kwa pamoja na madhehebu mbalimbali ya Kikristo.

Kuna pia wahuudmu kutoka Kanisa la Waothodoksi kutoka Ethiopia, Coptic na Syria. Ni eneo ambalo mamilioni ya mahujaji wa Kikristo husafiri kila mwaka kwenda kuliona kaburi wazi la Yesu na kutafuta ufunuo na kuomba katika eneo hilo.

Ukuta
Katika mtaa wa Wayahudi, kunapatikana Kotel, au Ukuta wa Magharibi ambao ni masalio ya ukuta wa nje uliozunguka lililokuwa Hekalu Takatifu.

Ndani ya hetalu hilo kulikuwa na Patakatifu, eneo takatifu zaidi katika Dini ya Kiyahudi. Wayahudi huamini kwamba, hapo ndipo kulikuwa na jiwe la msingi ambapo kutoka kwake dunia iliumbwa.

Kadhalika, wanaamini ni hapo ambapo Abraham alikuwa amejiandaa kumtoa kafara mwanawe Ismail. Wayahudi wengi huamini kwamba Dome of the Rock ndipo lilipokuwa eneo takatifu zaidi ndani ya hekalu lililofahamika kama Patakatifu. Makala haya kwa msaada wa BBC.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Wanajeshi Ukraine waishiwa risasi, 31,000 wauawa

Spread the loveRais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema zaidi ya wanajeshi 31,000...

Kimataifa

Waziri mkuu Palestina ajiuzulu

Spread the loveWaziri Mkuu wa Palestina, Mohammed Shtayyeh ametangaza kujiuzulu pamoja na...

Kimataifa

Rais mstaafu ahukumiwa miaka 4 jela

Spread the loveMahakama ya mjini Tunis imemhukumu rais wa zamani wa Tunisia,...

Kimataifa

Malawi yaondoa vikwazo vya viza kwa nchi 79 ikiwamo TZ

Spread the loveWaziri wa usalama wa ndani nchini Malawi, Ken Zikhałe ametangaza...

error: Content is protected !!