MUDA mfupi baada ya kuwasili Tanzania akitokea uhamishoni nchini Canada, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, amezindua matawi matatu ya chama hicho, yaliyoko mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Lema amezindua matawi hayo leo tarehe 1 Machi 2023, akiwa njiani kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuelekea mkoani Arusha kwa ajili ya kushiriki mkutano wa hadhara wa Chadema.
Matawi ya Chadema yaliyozinduliwa na Lema ni, Tawi la Njia Panda ya KIA, Tawi la King’ori na Siha, mkoani Kilimanjaro.
Baada ya kuzindua matawi hayo Lema aliwaaga wanachama wa Chadema walioshiriki tukio hilo kwamba analekea Arusha kwa ajili ya mkutano wa hadhara.
“Wapiganaji mimi hapa sikai, naomba kuzindua rasmi tawi hili kwa heshima ya wanachama wa Siha, ninakwenda kufanya mkutano wa hadhara,” amesema Lema.
Kwa sasa Lema ameshawasili mkoani Arusha, na yuko katika uwanja ulioandaliwa na Chadema kwa ajili ya mkutano huo. Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Leave a comment