January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hii Tume inanishangaza

Spread the love

NAUVAA ujasiri. Nilipokuwa nabashiri kabla ya kuchagua, watakuwepo watu laki wanadai haki kortini ya kuchagua, nilikuwa nahimiza ufanisi wa kazi. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Zilikuwepo dalili nyingi kazi ingefujika. Kweli mfumo wa uandikishaji wa kielektroniki – Biometric Voters Register (BVR), ulileta shida. Watendaji wazito kama sio wavivu, hata kudhaniwa walitumwa.

Kazi ya uhakiki ilihofiwa kwenda kombo. Ah, wacha bwana, nimerudisha imani kiasi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Wananishangaza kwa ninayoyashuhudia.

Tume iliita waandishi kituo cha uhakiki Relwe Gerezani wajionee uhakiki unavyofanywa. Ikatolewa orodha, angalau kwa idadi tu, ya walioandikisha zaidi ya mara moja. Wakakabidhiwa Polisi kuwashitaki. Tukio hili lilioneshwa hewani.

Uhakiki ukatengewa muda kuliko ilivyopangwa awali, Tume ikitaja Na. *152*00# ya kutumika mtu kujihakiki kabla ya kulazimika kufika kituoni iwapo taarifa hazijakaa sawasawa.

Haya nadra kwa siasa za Tanzania, kwa Zanzibar ndio usiseme.

Nikaisoma siku ya uteuzi wa wagombea urais, Babu Lubuva, mkuu wa Tume, anataka kila kitu hadharani.

Uteuzi wa wagombea urais hewani. Tukaona walioamua wakaidhinishwa, waliotania kumbo puu. Sijayaona tangu 1995.

Wakati maajabu yakitokea, kila siku unasoma taarifa mpya za jambo la maana kwa kujenga imani wananchi.

Kama si Babu Lubuva, itakuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey, au Mkurugenzi wa Idara ya Dafatari la Wapigakura, Sisty Kariah, si hao itakuwa Mama Fatuma Mkanguzi, mtaalamu wa TEHAMA wa Tume.

Tayari tunajua wachapishaji karatasi za kura – Uniprint wa Bondeni kwa Madiba.

Hayo tisa. Hii khabari ya siku tatu za kuonesha mfano wa Oktoba 25, ndio kumi. Tume wanasema wananchi watashuhudia laivu mfano wa kupiga kura (eleksheni demo) mpaka utangazaji matokeo.

Tutaona foleni, mtu kuingia chumba cha uchaguzi, kuhojiwa na msimamizi huku akitoa kadi ya kuandikishwa naye, akishathibitishwa si mamluki, akipewa karatasi tatu za kura; kwa mpigakura wa Zanzibar, na kura za Rais wa Zanzibar, mwakilishi na diwani. Ndio tuna kura saba siku hii.

Mpigakura ataelekezwa kupigakura, kuzikunja na kuzitia sandukuni. Atachovya kidole wino maalum. Yote haya, isipokuwa anapozungumza na muumba wake, pale anapomuua mnyama, yanafanyika kila mhusika chumbani akiona.

Dah, Babu Lubuva yukoje? Anaahidi kutangaza matokeo siku tatu au nne kutoka saba za Sheria ya Uchaguzi, 1985. Mazoea yetu hata wiki, leo anafuta ajizi. Huyu babu nae!

Msikilize, “…taratibu nyingine ziendelee, wananchi wakajenge taifa, waachane na khabari za uchaguzi.”

Anaamini kurefusha muda, unajichongea na kualika maharamia kuchakachua – ada Tanzania na Afrika.

Anakataa “utaratibu tuliojiwekea.” Haogopi lawama za watemi wanaosubiri kushinda kwa “goli la mkono,” alivosema kinda wa Sisiem.

Babu akili nyingi kumzidi Samwel Kivuitu, ambaye chini yake Wakenya walichapana kwa kuhisi aliacha ushindi wa upinzani uhujumiwe Disemba 2007.

Anakwepa janga na ICC ya Mama Bensouda aliyetanguliza maajenti tayari. Ndio naamini wasemavyo waomjuao Babu, Pitalo rekodi tupu za maamuzi yasiyotegemea harufu ya KK (Kitu Kidogo). Yeye sheria basi! Sijui ataweza; kazi ndo inaanza. Akitaka sawa, asitake pia sawa, si tutayaona?

error: Content is protected !!