Thursday , 7 December 2023
Home Kitengo Maisha Elimu HESLB yatoa bil.100 mikopo ya wanafunzi
Elimu

HESLB yatoa bil.100 mikopo ya wanafunzi

Mkurugenzi wa Bodi MIkopo ya Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru
Spread the love

BODI ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania, imetoa fedha za mikopo zaidi ya Sh. 100 bilioni, kwa wanafunzi 132,119, wanaotarajia kurejea vyuoni kuanzia tarehe 1 Juni 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo amesema Abdul-Razaq Badru, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, leo Ijumaa tarehe 29 Mei 2020 jijini Dodoma, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu hatua zilizochukuliwa na bodi hiyo, katika kuhakikisha wanafunzi wanufaika wa mikopo, wanaipata kwa wakati.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania, John Magufuli, la kuwataka mikopo itoke kwa wakati na kusitokee usumbufu mara vyuo hivyo vitakapofunguliwa.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo tarehe 21 Mei 2020, alipotangaza kufunguliwa kwa vyuo vikuu na wanafunzi wa kidato cha sita kuanzia tarehe 1 Juni, 2020 baada ya kuwa vimefungwa kuanzia tarehe 18 Machi 2020, kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Akichanganua matumizi ya fedha hizo, Badru amesema Sh. 63.7 bilioni, zimetolewa kwa ajili ya malipo ya chakula na malazi, katika kipindi cha muhula wa tatu.

“Sh. 63.7 bilioni ni kwa ajili ya muhula wa tatu, kwa wanafunzi 132,119, kwa ajili ya kulipia malipo ya mhula wa tatu wa chakula na maradhi kwa wanafunzi wenye mikopo, kutoka vyuo na taasisi 81, kwa muda wa siku 60, watakazokuwa wanasoma mhula wa tatu,” amesema Badru.

Badru amesema, fedha za  malipo kwa ajili ya muhula wa nne, bodi yake imeshakabidhiwa na serikali na kwamba zitatolewa baadae.

Badru amesema, kiasi cha Sh. 59.1 bilioni, zimetolewa kwa ajili ya malipo ya ada za maosmo kwa muhula wa pili.

“Malipo ya ada ambayo yanafanyika mara mbili kwa mwaka, baadhi ya wanafunzi wanastahili ya ada za masomo, muhula  wa kwanza imeshalipwa, na sasa hivi tunalipa ya muhula wa pili, ambayo ni Sh. 59.1 bilioni, na hizi zinalipwa pale ambapo chuo kinaleta ankara kulingana na idadi ya wanafunzi wake,” amesema Badru.

Badru amesema, fedha hizo zimeshapelekwa katika vyuo 62, na kwamba, hadi kufikia mwisho wa wiki hii, vilivyobakia zitapewa fedha hizo.

Wakati huo huo, Badru amesema kuanzia leo hadi tarehe 7 Juni 2020, HESLB itapeleka maafisa wake katika vyuo, ili kuhakikisha changamoto za mikopo zinatatuliwa kwa haraka.

“Ili kuhakikisha tunakwenda sambamba na vyuo, tumekubaliana tutafanya kazi pamoja, bodi inapeleka watu katika vyuo vyote. Ambao watakuwa wanashirikiana na watumishi kuhakikisha mikopo inalipwa kwa wakati na panapokuwepo changamoto zinatatuliwa mara moja,” amesema Badru.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuHabari Mchanganyiko

CEO NMB awataka vijana kunoa ujuzi wao

Spread the loveAfisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amewashauri...

Elimu

150 wahitimu Shahada ya Udaktari HKMU

Spread the loveCHUO Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), kimeiomba serikali...

Elimu

Aliyehitimu udaktari HKMU na miaka 21 atoa siri

Spread the love MHITIMU wa fani ya udaktari ambaye ni mdogo kuwahi...

Elimu

Janeth Mbene apongeza HKMU, ataka wahitimu wajiajiri

Spread the loveWAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), ...

error: Content is protected !!