BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imeahidi kutoa fedha za mikopo kwa wanafunzi waliobadilisha kozi, kesho tarehe 18 Desemba 2019. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 16 Desemba 2019 na Abdul-Razaq Badru, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, kwenye kikao cha menejimenti ya bodi hiyo na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na wawakilishi wa wanafunzi wa chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Badru amesema HESLB inakamilisha malipo ya fedha, kwenye orodha ya wanafunzi waliobadilisha kozi, iliyopokea kutoka kwa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), mwishoni mwa wiki.
“Kuna wanafunzi waliobadilisha kozi wakiwa vyuoni na taarifa hizo zilikua hazijatufikia, tumezipokea mwishoni mwa wiki, na tunakamilisha malipo ambayo yatawafikia siku mbili zijazo,” amesema Badru.
Wakati huo huo, Badru amesema HESLB itakamilisha malipo ya Sh. 11 bilioni, kwa ajili ya vitabu na viandikwa kwa wanafunzi, siku ya Jumamosi ya tarehe 21 Desemba mwaka huu.
Maelezo ya bodi hiyo yamekuja siku moja baada ya Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM (DARUSO), kutoa saa 72 kwa HESLB kuwapangia mikopo wanafunzi ambao rufaa zao zilipingwa, pamoja na kurudisha fedha za mikopo ya wanafunzi, ilizokata.
Leave a comment