August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hekaheka za EFDs zaanza

Spread the love

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara wasio na mashine za kodi (EFDs) na wale walio nazo lakini hawazitumii, wazinunue na kuanza kuzitumia, anaandika Christina Haule.

Imeeleza kuwa, walionazo lakini hawazitumii pia wasiokuwa nazo watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi zilizokaziwa na agizo la Rais John Magufuli.

Wito huo umetolewa leo na Kabula Mwemezi, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Mwemezi alizungumza hayo kufuatia kuepo kwa malalamiko ya wananchi wa manispaa hiyo kupewa bidhaa kwenye maduka makubwa bila stakabadhi licha ya kudai.

Meneja huyo amefafanua kuwa, wafanyabiashara hao wakubwa ni wale wenye mitaji mikubwa yenye kuingiza mauzo ya zaidi ya Sh. 20 mil kwa mwaka.

“Wafanyabiashara wakubwa watambue kuwa, wanapaswa kununua mashine hizo wenyewe na sio kusubiria kuwa TRA inaweza kuwapa bure.

“Wanaopaswa kupewa bure mashine hizo ni wale wafanyabiashara kundi la kati wenye mauzo ya chini ya Sh. mil 20,” amesema.

Amesema kuwa, lengo la TRA ni kuwataka wafanyabiashara wote nchini kutunza vizuri kumbukumbu zao na kufikia malengo waliyokusudia.

Hata hivyo, amefafanua kuwa kundi la mwisho la wafanyabiashara ni wale wenye mauzo ya chini ya Sh. 14 mil kwa mwaka ambao hawawajibiki kutumia mashine hizo bali wataendelea kutumia vitabu.

Aidha, Mwemezi amesisitiza wafanyabiashara wote kutambua kuwa, wanahaki ya kuuza na kutoa stakabadhi kwa wateja wao ili kuongeza mapato kwa taifa.

error: Content is protected !!