Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Heche, Zitto waivuruga serikali
Habari za SiasaTangulizi

Heche, Zitto waivuruga serikali

Spread the love

MBUNGE wa Tarime Vijijini (CHADEMA/UKAWA), John Heche, amezua tafrani bungeni, kufuatia hatua yake ya kuituhumu serikali kuwa imejifunga kwenye mkataba wa kitapeli na kampuni ya Arab Contractors. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Akizungumza wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati, Heche alisema, kampuni hiyo kutoka nchini Misri haina uwezo wa kufanya kazi iliyopewa na serikali.

Alisema, “kaampuni hii ya Arab Contractors iliyopewa kazi ya kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye Mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s Gorge, haina uwezo wa kufanya kazi hiyo. Haijawahi kufanya hiyo kazi na haina uwezo wa kuifanya.”

Kwa mujibu wa Heche ambaye ni mjumbe wa kamati ya nishati, “Arab Contractors, ni kampuni inayojishughulisha na kazi za ujenzi wa majumba, siyo ujenzi wa mabwawa ya umeme.”

Alisema, “hawa watu hawana uwezo wa kujenga bwawa la umeme. Kwa sababu, hiyo sio kazi yao. Kazi ya Arab Contractor, ni kujenga majumba. Siyo mabwawa. Ndio maana baada ya kupata kazi hii, imetafuta mtalaamu wa kujenga hilo bwawa.”

Mara baada ya Heche kuibua madai hayo mazito, haraka naibu waziri wa nishati, Subira Mgalu, alisimama na kutoa taarifa bungeni kuwa mbunge aliyekuwa anachangia (Heche), amelidanganya Bunge.

Akitumia Kanuni ya 64 (e) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inayokataza mbunge kusema uwongo bungeni, Mgalu alisema, maelezo ya Heche kuwa “kampuni hiyo ni feki” hayana ukweli. Alisema, yeye kama naibu waziri mwenye dhamana ya nishati anaweza kulithibitishia Bunge kuwa mbunge Heche amedanganya Bunge.

“Mheshimiwa Heche amelidanganya Bunge. Kampuni ya Arab Contactor ina uwezo mkubwa wa kujenga bwawa hili na haijatafuta mbia kama ambavyo yeye aameeleza. Nimeuona mkataba wao na hilo naweza kulithibitisha,” alieleza Mgalu kwa sauti ya hasira.

Akamtaka Heche kuthibitisha anachokisema, vinginevyo akamuomba Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson Mwansasu, kutumia madaraka yake kumuamuru kufuta madai yake.

Akijibu mwongozo wa naibu waziri huyo, Naibu Spika Tulia alisema, kwa kuwa mkataba huo uko mikononi mwa serikali na yeye hajawahi kuuona, anaagiza uletwe bungeni ili ijulikane nani mkweli kati ya Heche na serikali.

Alisema, “mkataba ukifika bungeni ndipo nitakapomtaka mheshimiwa Heche kuthibitisha madai yake. Lakini kwa sasa, naamuru kusimamisha mjadala juu ya suala la Stiegler’s Gorge.”

Aliongeza, “kwa msingi huo, ninakuelekeza mheshimiwa Heche utaendelea na mchango wake katika maeneo mengine bila kutaja suala la mkataba kati ya serikali (Tanesco) na kampuni hiyo iliyoshinda zabuni.”

Maamuzi hayo ya Dk. Tulia yalipokewa kwa shangwe na upande wa upinzani, huku Zitto Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), akisimama katikati ya mjadala huku akisema, “mimi niko tayari kumsaidia Heche kuthibitisha.”

Kampuni ya Arab Contractors ilijifunga kwenye mkataba na serikali kupitia Shirika la umeme la taifa (Tanesco), kwa lengo la kujenga bwawa la kisasa la kuzalisha  megawati 2100 za umeme katika mto Rufiji. Mkataba kati ya pande hizo mbili, ulisainiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Desemba mwaka jana.

Katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Rais wa Jamhuri, John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly, walikuwa miongoni mwa mashuda wa tukio hilo linaloitwa na serikali ya Tanzania kuwa la “kihistoria.”

Wengine walioshuhudia, ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu; Waziri Mkuu wa Jamhuri, Kassim Majaliwa; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Waziri wa Nishati, Medard Kalemani; Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Dk. Tito Mwinuka na mwanasheria wa shirika hilo, Isdori Nkindi.

Wapo pia baadhi ya mawaziri, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, madhehebu ya kidini na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Arab Contractors – kampuni inayomilikiwa na serikali ya Misri – ilitangazwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano, kushinda zabuni ya kubuni/kusanifu na kujenga bwawa la Stiegler’s Gorge katika maporomoko ya mto Rufiji, kwa gharama zinazokadiriwa kufikia dola za Kimarekani 2.9 billion (sawa na Sh. 6.5 trilioni).

Fedha za kutekeleza mradi huu, ni mkopo uliotolewa na benki moja ya kibiashara nchini humo.

Kampuni ya Misri itajenga mradi huo katika hatua nne, ambazo ni ujenzi wa ukuta, ujenzi wa tuta lenye uwezo wa kutunza mita za ujazo 35.2 bilioni za maji, ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wenye mashine (turbines) 9 na kujenga vituo (sub-stations) za kufua umeme wa KV 400.

Hata hivyo, ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge unapingwa vikali na nchi wahisani, wakiwamo hasa Ujerumani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Wanasema, utekelezaji wa mradi huo, unahatarisha mazingira, wanyama na viumbe vingine asili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!