November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Haya yafanyike kuvutia wawekeza sekta ya habari

Spread the love

 

NI ukweli usiopingika  kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa nchi, ambao una mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya taifa na wananchi wake.

Licha ya jukumu zito ililonalo vyombo vya habari, lakini baadhi yake vinashindwa kulitekeleza kwa ufanisi,  kutokana na ukata wa fedha za uendeshaji.Hususan za kulipia gharama za uchapishaji kwa vyombo vinavyomiliki magazeti.

Pia, gharama za kulipia leseni kila mwaka, bili za  intaneti, umeme, kutuma waandishi wake wa habari kushuka chini kwa  wananchi hususan wa maeneo ya vijijini, kwa ajili ya kuibua changamoto zinazowakabili ili Serikali izifahamu na kuzitafutia suluhisho na gharama nyinginezo.

Gharama inazokutana nazo vyombo vya habari kwa upande wa magazeti, hazijaachana sana na gharama za uendeshaji wa vyombo vya kielektroniki, kama redio na televisheni, licha ya kwamba vyenyewe hukabiliwa na gharama nyingine zaidi za ununuzi wa vifaa na mitambo ya kuviendesha kama redio na televisheni.

Licha ya vyombo hivyo vya habari kuwa na fursa za kujiingizia kipato kupitia njia mbalimbali ikiwemo matangazo na mauzo, si vyote vinavyopata fedha za kutosha kujiendesha sambamba na kulipa stahiki za wafanyakazi wao, kutokana na ukosefu wa matangazo ya kutosha na mauzo ya maudhui yao.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Idara ya Habari Maelezo, magazeti na majarida yaliyosajiliwa ni 257, wakati vituo vya redio vilivyosajiliwa ni 210, televisheni (56), redio za mtandaoni (24), televisheni za mtandaoni (663), tovuti na mitandao ya habari zaidi ya 200.

Kutokana na changamoto hizo, ni ukweli usiopingika ya kwamba, inahitajika jitihada za kisera na kisheria zitakazosaidia kuinua uchumi wa vyombo vya habari, sambamba na kuwavutia wawekezaji ili waweke mitaji ya kutosha kujiendesha kwa ufanisi.

Hivi karibuni, wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya wahariri juu ya mikakati ya uchechemuzi kuhusu marekebisho ya sheria zinazosimamia  habari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliiomba Serikali iondoe vifungu vya sheria vinavyokimbiza wawekezaji ndani ya sekta hiyo.

Balile aliishauri Serikali iondoe kifungu cha sita cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, kinachoelekea vyombo hivyo kukata leseni kila mwaka, kwani kinawatia hofu watu wanaotaka kuwekeza wakihofia vyombo vyao kunyimwa leseni. Lakini pia, kukabiliwa na gharama za kulipia leseni kila mwaka.

Mwenyekiti huyo wa TEF alishauri vyombo vya habari vipewe leseni ya kudumu au ya muda mrefu kama inavyofanyika katika sekta ya mawasiliano, ambapo kampuni za simu hupewa leseni ya muda wa miaka 15.

“Kampuni za simu leseni zake ni miaka 15 ndiyo maana unaona wawekezaji hawana wasiwasi kuwekeza katika eneo hilo, sisi tunaona huku kwenye sekta ya habari nako leseni isiwe inahuishwa kila mwaka,” alisema Balile.

Licha ya kifungu hicho cha 6 cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, wadau wa tasnia hiyo wameanisha vifungu vyake kadhaa ambavyo wanasema vinadhorotesha uchumi wa vyombo vya habari, huku wakipendekeza virekebishwe kupitia mchakato wa marekebisho ya sheria unaotekelezwa sasa na Serikali.

Wanapendekeza kifungu cha 53 (4) cha sheria hiyo, kinachoelekeza mmiliki wa kiwanda kitakachochapisha habari za uchochezi kuchukuliwa hatua, kirekebishwe ili mmiliki asiwajibishwe, kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kuanzisha viwanda hivyo kwa wingi ili kupunguza gharama za uchapishaji zinazowakabili wamiliki wa magazeti.

Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa vyombo vya habari kupitia TEF na taasisi nyingine binafsi zinazosimamia sekta hiyo, wamependekeza marekebisho dhidi ya kifungu cha 4 (1) (b) cha Kanuni za sheria hiyo zilizotolewa 2017, kinachoelekeza raia wa kigeni kuwa na hisa asilimia 49 kwenye vyombo vya habari.

Wanapendekeza kifungu hicho kirekebishwe ili kutoa nafasi kwa raia wa kigeni kuwa na hisa nyingi, kitendo kitakachofanya vyombo vya habari kupata mitaji na teknolojia za kisasa kutoka nje ya nchi, kama inavyofanyika katika nchi nyingine.

Pia, wadau hao wanapendekeza vifungu vinavyompa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuratibu matangazo ya Serikali, kifutwe badala yake kiwepo kifungu kinachotoa uhuru kwa watoa matangazo, kufanya kazi na vyombo vya habari inavyotaka, ili kuepusha mwanya wa vitendo vya rushwa na upendeleo.

Hali kadhalika, wanapendekeza sheria ziweke mazingira mazuri kwa waandishi wa habari kuandika habari za kiuchunguzi, ili kuvutia wasomaji au wasikilizaji wengi, kitendo kitakachotanua wigo wa kupata fedha za kutosha za matangazo.

Makala hii imeandaliwa na Regina Mkonde … (endelea).

error: Content is protected !!