August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Haya ndiyo mashitaka yaliyowasotesha ‘mahabusu wa Ukuta’

Spread the love

WAFUASI watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakishitakiwa kwa makosa ya kimtandao pamoja na kuunga mkono harakati za Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), anaandika Faki Sosi.

Washtakiwa hao ambao pia wamepata dhamana ni Denis Mtegwa, Dennis Temu, Shakira Ndevu, Juma Mtatuu na Suleiman Nassoro walikuwa wakitetewa na jopo la wanasheria wakiongozwa na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Nassoro alisomewa shitaka la kusambaza taarifa za uongo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi ambapo alidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 25 Agosti, mwaka huu maeneo ya Kigogo Dar es Salaam alitumia mtandao wa Facebook kwa kusambaza taarifa hizo.

Anadaiwa kuandika, Safi sana aisee naona wangekufa kama 20 hivi, halafu Simon Sirro tumuulize mazoezi wanafanya kwa ajili ya wake zao.”

Mshtakiwa huyo alikana mashitaka yake huku akifanikiwa kupata dhamana baada ya wadhamini wawili kusaini bondi ya Sh. 500,000/- na kesi ikiahirishwa mpaka tarehe 27 Septemba, mwaka huu.

Mtegwa alisomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Yohana Yongolo na Bereck Mwakatubi, Wakili wa Serikali akidaiwa kufanya udhalilishaji kupitia mtandao wa WhatsAp mnamo 24 Agosti, mwaka huu.

“JPM Sijui anawaza nini kichwani hata samahani hajui au nilikosea hajui nchi imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua kujilipua ufahamu wake,

Huyu bwana ‘Misimamo’ ambayo ameisema, msinijaribu ilihali kajaribiwa na ubwabwa wa Jubilee, ….ajifunze kushindana kwa hoja sio mitutu ya bunduki na mazoezi ya Polisi yasiyo na kichwa wala miguu.

Watuhumiwa Makame na Mtatuu walisomewa mashtaka yao mbele ya, Respicius Mwijage Hakimu Mkazi Mkuu ambapo wakidaiwa tarehe 24 Agosti,  mwaka huu kwa nyakati tofauti kati Tegeta na Ocean Road jijini Dar es Salaam  walisambaza taarifa za kudhalilisha Jeshi la Polisi kupitia WhatsApp.

Makame anadaiwa kulidhalilisha jeshi hilo kwa kuandika;

“Wakati wao wanajiandaa na Ukuta, wengine wanajiandaaa na ujambazi safi sana Majambazi.”

Mtuhumiwa huyo alikana shItaka hilo na kudhaminiwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh. 2 milioni, ambapo shauri hilo litatajwa tena tarehe 4 Oktoba, mwaka huu.

Kwa upande wake Mtatuu anadaiwa kuandika ujumbe wenye lengo la kulichafua jeshi la polisi, akiandika “Huyu hata akifa hataenda peponi na kufanya mazoezini kote kule wamekufa Mbagala, Mimi nitakuwa wa kwanza kuandamana kule Kahama Septemba mosi kwa ajili ya Ukuta, nitakuwa namba moja kushika bendera ya Ukuta.

Kifo kipo tu usiogope kwani Mawe na Mapanga yameisha?”

Mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kudhaminiwa kwa bondi ya Sh. 2 milioni iliyosainiwa na mdhamini mmoja. Kesi yake imeahirishwa hadi tarehe 27 Oktoba  mwaka huu.

Watuhumiwa wote watano kwa jumla, wameachiwa huru baada ya kusota rumande wa zaidi ya siku 14 ilihali sheria inataka mtuhumiwa asishikiliwe kwa zaidi ya masaa 24 bila kufikishwa mahakamani.

Jumamosi iliyopita Lissu aliahidi kulichukulia hatua Jeshi la Polisi iwapo lingeendelea kuwashikilia watu hao pamoja na wengine watano ambao nao wamerejeshwa mikoani na kusomewa mashitaka yao huku wakipata dhamana.

error: Content is protected !!