Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Hawatatukana watafufua makaburi
Makala & UchambuziTangulizi

Hawatatukana watafufua makaburi

Spread the love

 

VYAMA vya siasa nchini Tanzania vimefunguliwa kutoka katika kifungo cha takribani miaka sita baada ya katazo lisilo la kikatiba wala kisheria la kufanya mikutano ya hadhara. Kwa kipindi chote hicho ni kama walifungwa midomo na hawakupata fursa ya kusema kwa uwazi mengi yaliyotokea katika Serikali ya awamu ya tano ya Hayati John Magufuli. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).

Januari 4 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati anatoa ruhusa ya mikutano ya hadhara alihadharisha matumizi ya lugha lakini pia namna nzuri ya kukosoa. Ni wazi wapinzani hawataacha kukosoa.

Vyama vyote vya upinzani vinaeleza kuwa lengo lao kuu ni kushika dola na ili vishike dola vieleze udhifu wa chama kilichopo madarakani ambacho ni Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kila chama kina utamaduni wake kwenye uwasilishaji wake wa hoja kwa wananchi mathalan uwasilishaji wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huwa ni wakikakamavu, wakufoka, wakikamanda wenye kuashiria wapo kwenye uwanja wa mapambano, uwasilishaji huo unawajaza wananchi matamanio ya mapambano lakini unakosoa kwa lugha ambazo wengine huona kuwa sio za kiungwana.

Mfano Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara akiwa anakosoa huwa ana sauti ya kukemea huku akichukua tahadhari kubwa ya kuhakikisha havunji sheria :- Siku ile aliposema Rais ni Dikteta Uchwara, Jamhuri ilipoamua kumfungulia mashtaka walijikuta wapo kwenye mtego wa kisheria kwa kuwa hakubainisha ni Rais yupi aliyemlenga ilhali kuna Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF).

Zitto Kabwe

Lissu ni miongoni mwa wanasiasa walionja joto ya jiwe kipindi cha serikali ya awamu ya Tano baada ya kushambuliwa kwa risasi 16 alipokuwa akitoka kwenye ukumbi wa Bunge na kurejea nyumbani kwake area ‘D’ jijini Dodoma eneo ambalo linalindwa ndio eneo wanaloishi viongozi na wabunge.

Lissu akisimama jukwaani hatokaa kimya bila kuzungumzia tukio hilo na bila kuihusisha serikali ya awamu ya tano. Hatoacha kusema jinsi alivyonyimwa stahiki zake za ubunge ambazo hatimaye alipata suluhu kwenye serikali ya awamu ya sita.

Lissu atakuwa na mengi ambayo hataweza kuyakalia kimya halikadhalika kwa Godbless Lema Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema akipanda kwenye jukwaa atazungumza kilichomuondosha nchini ambapo lazima ataigusa kwa namna mbaya serikali ya awamu ya tano na pengine kuihusisha na iliyopo sasa.

Vilevile kwa Mbowe atalikumbuka jengo la Billcanas , ataikumbuka hukumu iliyompeleka gerezani, atakumbuka uchaguzi mkuu wa 2020 atamkumbuka msaidizi wake Ben Saanane, atakumbuka yote ya miaka sita iliyopita.

Nao Chama cha ACT-Wazalendo na Kiongozi wake Zitto Kabwe, atakumbuka kesi yake Na.327 ya mwaka 2018 ya uchochezi alipozungumzia tukio la Mpeta kwenye mkutano wa vyombo vya habari ambapo alikamatwa na kushtakiwa kwa uchochezi.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Chama hicho kitakumbuka katazo la mikutano ya hadhara lakini kipekee kitambuka maswahibu ya uchaguzi wa mwaka 2020 uliosababisha wanachama wake kule Visiwani Zanzibar kupoteza maisha, kuteswa na kusababishiwa ulemavu wa kudumu.

ACT kimejijengea utamaduni wake wa kukosoa huku wakionyesha njia ya ufumbuzi wa hilo tatizo hivyo ukosoaji wao ni wa kujenga zaidi.

Halikadhalika Chama cha Wananchi CUF kitaeleza namna walivyofumbwa midomo kuwaambia wananchi yanayoendelea lakini pia kuendelea kukieneza chama chao.
Kimsingi hawatatukana lakini watazungumza yale ambayo pengine chama fulani hakitapenda kuyasikia kwa kuwa mengi ni lawama kwa Serikali ya chama hicho.

Masikio ya watanzania yatakuwa kwenye mikutano hiyo kuwasikiliza wanasiasa kwa mara ya kwanza tangu kufunguliwa ili kuona watazungumza nini.

Mkutano wa kwanza utakuwa wa Chama cha Wananchi CUF unatarajiwa kufanywa kesho tarehe 6 Januari Manzese jijini Dar es Salaam huku Chadema ikitarajiwa kuzindua mikutano yake ya hadhara kitaifa tarehe 21 Januari mwaka huu na kuendelea na kanda zote nchi nzima.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!