July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hawakatai katiba CCM, ukweli hawataki mabadiliko

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda

Spread the love

KILA nikitafakari matamshi yanayotolewa na wakubwa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ninapata picha moja tu iliyo kubwa: hawataki katiba mpya kwa mwelekeo ulioletwa.

Mwelekeo ulioletwa katika kuendeleza utaratibu wa kuipatia jamhuri yetu katiba mpya inayoendana na wakati tuliopo, ni wa mabadiliko.

Tena, yaliyojengwa kwa muktadha huo, ni mabadiliko makubwa. Hatua ya kufumua mfumo wa uendeshaji wa serikali katika jamhuri, kwa mshabaha wa kuimarisha Muungano ulioasisiwa mwaka 1964, ni mabadiliko makubwa.

Hebu niliweke sawa hili mapema. Ni hivi, katika kuyachekecha kitaalamu maoni ya Watanzania walioeleza hisia zao kuhusu mwelekeo wa Katiba ijayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imekuja na rasimu inayofuta mfumo wa serikali mbili na kupendekeza mfumo wa serikali tatu badala ya wa mbili, unaong’ang’aniwa na CCM.

Mabadiliko hayo, aliyoyawasilisha kwa hoja na Mwenyekiti wa Tume, Joseph Warioba, yanataka ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali upunguzwe; na madaraka ya Rais wa jamhuri, yapunguzwe.

Ukubwa wa Bunge upunguzwe kwa kuwepo wabunge 75. Maana yake ule utitiri wa wabunge mpaka wasiojadili kitu bungeni zaidi ya kusinzia wakati wa mijadala, hautakuwepo. Hapo, inapatikana faida nyingine. Kupunguza mabilioni ya shilingi yanayotumika kugharamia mikutano ya bunge na posho za wabunge.

Tume imependekeza kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba, kuwa baraza la mawaziri la serikali ya jamhuri, liwe na wajumbe wasiozidi 15. Hapa napo maana yake katiba ijayo inaweka idadi ya mawaziri. Hili ni jambo jipya na zuri katika kupunguza matumizi.

Niseme zaidi kidogo. Kwa kupunguza idadi ya mawaziri, maana yake ule utamaduni wa Watanzania kuteuliwa baraza la mawaziri lenye hata watu wasiojua jamhuri ya Tanganyika iliungana na nchi gani mwaka 1964, na kuundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utakufa.

Pia hatutaona mawaziri wanaothubutu kutoa kauli za uchochezi wa kidini, kati ya Waislam na Wakristo, wakiendelea kuongoza. Hawa ikitokea, watupwe jela baada ya kuthibitishwa wamechochea fujo.

Katika baraza la mawaziri liliopo, wapo mawaziri watuhumiwa wa rushwa, ujangili, uzinzi, ushirikina, ushoga, ufisadi uchafu usiotakiwa. Lakini, kwa sababu wengi wao waliteuliwa ili kuhakikisha kila kipembe cha nchi kimepata mwakilishi, mteuzi hajali kumfukuza hata mmoja.

Sizui nikisema kuwa mawaziri waovu wanalindwa, licha ya machafu yao hayo kutangazwa waziwazi na vyombo vya habari. Ni kwa kuwa wakikosa uwaziri, watakusanyaje utajiri na kukisaidia chama dola kustawi zaidi ili na mwakani utapokuja uchaguzi mkuu, kishike tena madaraka?

Rasimu inataka Rais wa Jamhuri apunguziwe nguvu za kimungu alizopewa na Katiba ya 1977. Yeye ni Rais, Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa Nchi, na bado anateua kila ofisa wa serikali wa ngazi husika.

Ubaya ni pale anapopewa mamlaka ya kuteua hata wakuu wa taasisi mhimili wa dola kama ile anayoiongoza – Serikali. Rais anamteua Jaji Mkuu wa kuongoza Mahakama ambayo ni mhimili wa dola.

Rais hamteui Spika, anayeongoza Bunge ambayo nayo ni taasisi mhimili wa dola, bali mbali na kuwa mwenyewe ni sehemu ya Bunge, anateua anayeitwa Katibu wa Bunge.

Anateua wakuu wa asasi za serikali zinazofanya kazi ya ufuatiliaji wa masuala yanayohusu ulinzi, usalama na zinazosimamia mwenendo wa utawala bora.

Hizi ni Polisi, Usalama wa Taifa (TISS), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali – Controller and Auditor General (CAG) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi – National Electoral Commission (NEC).

Fikiria rais akishawateua wakuu hawa, si anawapa amri? Wataitekeleza, hakika wanatekeleza hata amri haramu. Hii ni kasoro kwa sababu baadhi ya amri zinamwelekeo wa kuumiza wananchi isivyo halali kisheria.

Amri nyingine zinaumiza taifa na kulipa taswira mbaya kwa walimwengu.

Mfano mzuri ni athari za Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuzuiwa au hata kuhofia kuchunguza watu wanaotuhumiwa kwa rushwa, hususan wale anaowajua kuwa wana uhusiano wa karibu na Rais, mteuzi wake.

Mwaka 2012, Edward Hoseah, mkuu wa asasi hii, alimwambia mhariri wa WikiLeaks, kuwa hawawezi kuchunguza baadhi ya wakubwa kwa kuwa wanamyong’onyesha mheshimiwa rais.

Kutowafuatilia wakubwa wanaokula rushwa ili kugawa zabuni kiupendeleo, wakubwa wanaohongwa ili kunyonga haki za watu, ili kupora ardhi wanazotumia wananchi kuzalisha mali, ni uharamia unaodhoofisha heshima ya serikali na Watanzania.

Ni kwamba manufaa yanayopatikana kutokana na madaraka makubwa aliyonayo Rais wa Jamhuri yetu, na matumizi makubwa yasiyohitajika yanayotafuna fedha za wananchi, na amri haramu zinazowaumiza wananchi, ni miongoni mwa manufaa yanayowaangukia wakubwa wanaopewa vyeo na rais.

Kuleta katiba inayokataza utamaduni huu wa kunufaishana kibinafsi, si jambo linalowapendeza wakubwa na mawakala wa CCM. Kupitia mfumo regevu kimaamuzi, ndipo zinapatikana fedha ambazo faida yake huifikia CCM ikaendesha siasa zake za kuchumia tumbo.

Ukweli upo hapa kwamba wakubwa wa CCM hawaitaki katiba mpya inayotokana na Rasimu ya Pili kwa kuwa itawavuruga wao na chama chao. Wanaogopa katiba mpya ijayo, kwa ilivyo rasimu, itafunga mirija yao ya kuchuma. Itapunguza mapato haramu na hivyo kuwazuia kufanya matanuzi hata wakati wa kazi. Itabidi wapunguze nyumba.

Hata angekuwa nani, asingeikubali rasimu ya katiba inayomhakikishia kukosa ulaji haramu anaoupata kwa miaka kadhaa. Wanayo mishahara halali, kuna fedha za juu (za michongo au mishemishe) watakosa. Hawapo tayari kuepuka kuhongwa.

Kwa sababu wakubwa CCM hawajakubali kwenda na wakati, hawakubali ukweli kuwa Watanzania walio wengi wamechagua mabadiliko. Hawakubali kwamba wapo tayari kugharamia serikali tatu, maana ni ndogo tu kuliko serikali mbili zilizojaa mawaziri na watendaji.

Basi kwa kuwa rasimu inaleta mabadiliko, ambayo wao hawayataki, wanagoma wakiamini hasa kuwa wanayo haki maana hii jamhuri ni yao peke yao. Watanzania walio nje ya wigo wa CCM, hawana chao.

Kiasi wakubwa wa CCM watamke hata leo kuwa wala “hatujui sababu zilizowatoa UKAWA bunge la katiba.” Kwani hamjui kwamba mlevi wa madaraka hawezi kujishughulisha na kutambua haki za anaowangoza?

Hawa ni walevi wa madaraka, na kwa sababu wanayatumia kuchuma mali, hawakubali kuruhusu mali wanayokula igawanwe na Watanzania wengine.

Kwa hiyo basi, tunaotaka mabadiliko tuvumilie kuwasikia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Nchi (Bunge), William Lukuvi, Asha Bakari Makame, Vuai Ali Vuai na Waride Bakari Jabu kusema UKAWA warudi bungeni ndiko kunapatikana katiba ya wananchi.

Hata kwa nukta, tusiwatarajie wakubwa hawa na wenzao wa kiwango chao kuridhia ukweli kwamba UKAWA walikataa ujahili na ulaghai. CCM ni chama ambacho kwa sasa, macho yake ni vipi kitabakia madarakani.

Hayo tu. Mengine yote, na hasa yale yanayoelekea kukiondoa kwa njia ya demokrasia, hayana maana yoyote kwao. Ndo maana wanasema “Mapinduziiiii, Daimaaaaa!”

error: Content is protected !!