Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Hawa ndio wanawake wanaotikisa, wanaoigusa jamii ya Watanzania
Makala & Uchambuzi

Hawa ndio wanawake wanaotikisa, wanaoigusa jamii ya Watanzania

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

MACHI 8 kila mwaka Siku ya Kimataifa ya Wanawake duniani ambayo huadhimishwa kwa lengo kuongeza chachu katika harakati za mapambano ya kuleta usawa wa kijinsia kwa wanawake na wanaume kwenye jamii.

Siku hii ilianza kuadhimishwa tarehe 8 Machi 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuridhia siku hii kutumika kama siku rasmi ya kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Abel&Fernandes, Fatma Fernandes

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake mwaka 2023, ambayo nchini yalianza Machi 1 na kufikia kilele leo Machi 8, ni ” Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia”.

Hata hivyo, wakati tukifikia kilele cha kwenye maadhimisho hayo, si vibaya kuwachambua baadhi ya wanawake ambao wamekuwa vinara katika kuigusa au kuinufaisha jamii kwa namna mbalimbali kutokana na uwepo wao hapa nchini.

RAIS DK. SAMIA

Baadhi ya wanawake hao walioigusa jamii kisiasa, kijamii, kiuchumi na nyanja nyingine, wa kwanza ni Rais wa sita wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Dk. Samia ambaye historia yake ni ya kipekee ikiwa imesheheni mambo mbalimbali, ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa ya urais nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki. Dk. Samia pia ndiye kiongozi wa kwanza mwanamke anayeongoza chama tawala cha CCM tangu kuasisiwa kwake.

Aidha, Dk. Samia ambaye mwaka 1977, alianza kazi ya ukatibu muhtasi alifanikiwa kujiendeleza kimasomo hadi kufikia kuwa mjumbe maalumu wa Baraza la wawakilishi la Zanzibar mwaka 2000 kazi ambayo ni kama aliendeleza majukumu ya kuwatetea wananchi kwani hapo kabla alikuwa kwenye taasisi binafsi zinazotetea jamii kwenye nyanja mbalimbali.

Baada ya kupenya kwenye Baraza la Mawaziri Tanzania  mwaka 2010, nyota yake ilizidi kung’aa baada ya kufanikiwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dk. John Magufuli mwaka huu 2015.

Hata hivyo mwaka 2021, ndipo Mwenyezi Mungu alipoamua kumpa jukumu la juu zaidi la kuiongoza Tanzania na sasa wanawake wote na watanzania kwa ujumla wanafurahia matunda ya mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania kutokana na utulivu wa kidemokrasia, amani na kasi ya utekelezaji wa majukumu yake unavyoendelea kumbeba kiasi cha kupewa udaktari wa heshima na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

TULIA ACKSON

Baada ya kushinda kiti cha Spika wa Bunge Januari 21, 2022, ndipo dunia ilizidi kumtambua Dk. Tulia Ackson kwani alifungua ukurasa mwingine katika maisha ya kisiasa yasiyo ya kawaida ya mbunge huyo wa Mbeya Mjini katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Spika Dk. Tulia Ackson

Mwanamama huyo aliyebobea kwenye masuala ya sheria, alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya kuingizwa kwenye siasa katika uteuzi wa Rais wa mstaafu Dk. Jakaya Kikwete 2014, kisha Dk. John Magufuli mwaka, mwaka 2020 aligombea ubunge mara ya kwanza na kushinda kisha kuonesha ujasiri wake katika mambo mbalimbali ikiwamo kuanzisha Taasisi ya Tulia (Tulia Trust Fund) ambayo mbali na kuwawezesha wanawake kiuchumi, pia imekuwa ikiendesha Tamasha kubwa la Tulia Traditional Dances Festival pamoja na Mbeya Tulia marathon.

RUTH ZAIPUNA

Ukitaja mafanikio ya Benki ya NMB ambayo mwaka jana imefanikiwa kushinda tuzo 18 za kitaifa na kimataifa kutokana na huduma bora walizozitoa kwa wateja wake, huwezi kuacha kumtaja Ruth Zaipuna.

Afisa Mtendaji Mkuu – NMB, Ruth Zaipuna NMB

Agosti 18, 2020 Zaipuna aliandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu Benki hiyo ilipobinafsishwa ambapo kwa nyakati zote nafasi za juu zilishikwa na wageni kabla ya Zaipuna kupewa nafasi ya kukaimu katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu lakini akafanikisha NMB kupata faida kubwa ya Sh bilioni 93.

HELEN KIJO BISIMBA

Ukizungumzia nyanja ya uanaharakati katika masuala utetezi wa haki za binadamu, huwezi kuacha kumtaja Dk. Kijo-Bisimba (68) ambaye amekuwa Kinara wa harakati za haki za binadamu nchini Tanzania.

Dk. Helen Kijo Bisimba

Dk. Bisimba ambaye alikuwa mwalimu huyo wa somo la kiingereza na Kiswahili katika taasisi ya elimu ya watu wazima kabla ya kusomea sheria, amekuwa kama mlinzi wa haki za binadamu kwa muda mrefu pia amekua mwenye ushawishi mkubwa na kuwa chachu ya vijana wengi wachanga kuingia katika uwanja wa sheria kwa sababu yake.

Dk. Hellen Kijo Bisimba ametumikia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu toka mwaka 1995 mpaka alipostaafu mwaka 2018, lakini pia mmoja wa wanawake wachache wenye Shahada ya Uzamivu (PHD).

ASHA BARAKA

Katika tasnia ya sanaa na burudani, jina la Asha Baraka si geni masikioni mwa watanzania kwani amekuwa mwanamke wa mfano wa kuigwa kwa ujasiri alionao tangu alipoanza kazi mwaka 1980 ambapo aliajiriwa katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) jijini Dar es Salaam katika Idara ya mauzo na masoko kabla ya kiujuzulu mwaka 2010 na kujikita kwenye siasa na biashara.

Mama huyu mwenye ana vipaji lukuki, licha ya majukumu yake ya kazi, pia alikuwa  akijishughulisha kibiashara kwa kuongoza kundi la vijana waisopungua 45, katika bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’

Mzaliwa huyo wa Uvinza Kigoma, pia ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET), iliyoanzishwa mwaka 2000 lakini pia ina chuo au Academy ya kuendeleza vipaji vya vijana, inayoitwa Twanga Pepeta   Acade.

FATMA FERNANDES

Ukizungumzia wanawake wabunifu katika nyanja ya teknolojia lakini pia wenye ujasiri wa kujikita kwenye nyanja ya biashara na uchumi, mmoja wao ni Fatma Fernandes ambaye uthubutu wake umechagizwa na taaluma ya Uhusiano na Utawala wa Kimataifa.

Fatma ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya masuala ya teknolojia ya Quincewood Group Limited, yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, kwa takribani miaka 10 sasa imefanikiwa kutoa huduma ambazo ni suluhu ya changamoto mbalimbali kwa njia ya mitandao ya simu katika taasisi mbalimbali ikiwamo za sekta za umma, binafsi.

Fatma amewagusa wanawake katika maeneo matatu muhimu ya kilimo, wanawake, elimu na afya kwani katika kilimo ndiye mwanamke wa kwanza kuleta mageuzi ya kiteknolojia kupitia kampuni ya Quincewood ambayo inawapatia wakulima suluhisho la kuepuka kutumia mbegu feki kwani kampuni hiyo imekuja na teknolojia ya uhakiki wa mbegu kwa njia rahisi ya simu za mkononi kwa kutumia program ya T-Hakiki.

Aidha, mwasisi huyo pia wa kampuni ya masuala ya mawasiliano Abel & Fernandes, amefanikiwa kuifikia jamii kwa nyanja mbalimbali kupitia kampuni zinazofanya kazi na kampuni yake katika kutekeleza mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) mbali na kuzalisha ajira.

Pia kila mwaka amekuwa akiungana na kampuni nyingine kutoa huduma za matibabu bure kwa wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu ili kuboresha afya za watanzania lakini kwa upande wa elimu, tayari amefungua shule ya kimataifa ya watoto (Monti Kids Tanzania) ambayo sasa inatoa suluhu kwa wazazi kuwapatia elimu bora watoto wao huku shule hiyo ikizalisha ajira kwa watu wa kada mbalimbali.

PENDO NJAU (MALKIA WA ULINGO)

Pendo Njau ni mwamuzi wa masumbwi kinara kwa sasa nchini Tanzania akiwa na rekodi ya kuchezesha mapambano makubwa zaidi nchini Tanzania siku za karibuni.

Pendo Njau

Safari yake katika masumbwi kuanzia mwaka 2008-2009, haikuwa rahisi kama mwanamke tangu awali jamii ilimshangaa kwani walio wengi waliamini mchezo huo ni wa wahuni tu lakini katika uchezaji ngumi alifanikiwa kutwaa mataji mawili makubwa.

OPPA CLEMENT

Oppa Clement

Oppa ni mchezaji wa kandanda au mpira wa miguu anayeichezea klabu ya wanawake ya Simba Queens ya Tanzania na timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake Twiga Stars. Amekuwa mwanamke mwenye mvuto kwa wenzie kucheza mpira wa miguu kwani mbali na kuwa kinara wa mabao kwenye ligi hiyo sasa amesajili nchini Uturiki  katika klabu ya Besiktas.

ANNA HENGA

Mwanamke huyu wa shoka ambaye amechukua mikoba ya Dk. Bisimba LHRC, anasema siku 365 za mwaka zote ni za wanawake kwa sababu wanafanya kazi usiku na mchana, mchana ni mkulima, mfanyakazi, na mfanyabiashara ilihali jioni na usiku ni mlezi wa watoto na familia kwa ujumla yaani kila siku wapo kazini.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga

Anasema anachojivunia katika utetezi wa haki za binadamu ni kuwapa msaada wa kisheria zaidi ya wanawake 200 kila siku nchi nzima kupitia vijana wake.

“Kauli mbiu yam waka huu inayohusiana na masuala ya kidijitali, imeendana na LHRC kwani tumetengeneza app maalumu ambayo mtu yeyote anaweza kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu hasa ikizingatiwa wanawake wengi wanamiliki simu hivyo wanaweza kupiga siku kutoa taarifa,” anasema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!