August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hawa hawatomsahau JPM abadani

Mabanda yanayotumika na wakazi wa Bonde la Msimbazi kama makazi baada ya kubomolewa nyumba zao

Spread the love

HUENDA watamsamehe lakini kamwe hawawezi kumsahau Rais John Magufuli katika maisha yao kutokana na kutendwa, anaandika Faki Sosi.

Walikuwa na matumaini naye lakini baada ya kugusa mtima wao, kwa hakika wamebaki na makovu, manung’uniko na visirani ndani ya nyoyo zao.

Hawa ni wale walitumbuliwa pia kuvunjiwa nyumba zao walizokuwa wakiishi kabla ya utawala wa awamu ya tano.

Miongoni mwa Watanzania wenye vihoro na utawala wa Rais Magufuli ni waliokuwa wakazi wa Bonde la Mkwajuni, jijini Dar es Salaam waliobomelewa makazi yao tarehe 17 Disemba Mwaka 2015.

Wakazi hawa wahakuamini kile kilichotokea tarehe hiyo huku wengine wakiangua vilio na baadhi hata kupoteza maisha kutokana na mshtuko wa tukio la kuvamiwa kwenye makazi yao na kubomolewa pasipo kuwepo mjadala.

Kazi ya kuwang’oa eneo hilo ilifanywa na Halmashuri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Baraza la Taifa  Kuhifadhi na Kusimamia Mazingira (NEMC) kwa msaada wa karibu wa Jeshi la Polisi.

Tarehe 19 Aprili 2016, familia ya Wilson Kabwe, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam ilipata pigo la kutumbuliwa kwa baba wa familia hiyo (Wilson Kabwe).

Familia hiyo bila shaka haitamtazama Rais Magufuli kwa jicho la wema hasa kuzingatia namna baba yao (Wilson) alivyotimuliwa mbele ya kadamnasi siku ya uzinduzi wa Daraja la Kigamboni.

Terehe 20 Mei 2016 familia hiyo ilipata pigo zaidi baada ya Kabwe kufariki dunia jambo linalodaiwa kuhusishwa na mshtuko wa kutumbuliwa.

Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alionja maumivu ya utawala wa Rais Magufuli.

Tarehe 20 Mei mwaka huu ipo kwenye kumbukumbu yake daima, ndio siku alipotimuliwa na Rais Magufuli kwa madai ya kulewa na kuingia bungeni.

Bernard Mchomvu, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato (TRA) naye anaongeza orodha ya watu walioonja machungu ya utawala wa awamu ya tano.

Ilikuwa tarehe 20 Novemba mwaka 2016 ambapo alipata taarifa ya kuondolewa kwenye ‘kiti chake cha ufalme’.

Tarehe 20 Aprili mwaka 2016 Rais Magufuli alipeleka majonzi kwa Juliet Kairuki, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Kosa lake kuu na lililoibua mjadala kitaifa ni madai ya Rais Magufuli kwamba, amekuwa akifanya kazi bila kupokea mshahara wa serikali tangu aajiriwe.

Muosha huoshwa, hii kauli ilitumika pale Rais Magufuli alipomtumbua Ombeni Sefue ambaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Ombeni alikuwa akitumika kutoa taarifa za wale waliotumbuliwa na mkuu wa nchi. Ombeni alifikwa na kadhia hiyo tarehe 6 Machi 2016 akiwa Ikulu.

Tarehe 11 Aprili 2016, Anna Kilango Malecela, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Shinyanga alipoteza ajira yake mara baada Rais Magufuli kumtimua.

Madai ya Ikulu ni kwamba, Kilango alitoa taarifa isiyo sahihi kwamba, kwenye mkoa huo ambao yeye alikuwa mkuu wa mkoa hakukuwa na watumishi hewa jambo ambalo lilibainika kuwa taarifa yake haikuwa na ukweli.

Tarehe 17 Desemba 2016 Rais Magufuli alipeleka tena machungu katika familia ya Malecela.

Wakati huu alimtumbua Dk. Mwele Malecela, aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu (NIMR).

Kilichoonekana kuikera Ikulu ni kutoa matokeo ya utafiti yaliyoonesha kuwepo kwa virusi vya ZIKA jambo lililoelezwa kwamba, linaweza kuathiri nchi hususani kwenye masuala ya utalii.

Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nayo iliguswa. Tarehe 15 Februari mwaka 2016 Herry Mchunga, Mkurugenzi wa Manunuzi wa MSD  na wakurugenzi wengine watatu walitmbuliwa.

Ha walitumbuliwa wakiwa katika shuguli za ufungaji vitanda kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa madai ya kufanya ubadharifu wa fedha zilizodaiwa kufikia Sh.1.5 bilioni na kukeuka sheria za utumishi wa umma.

Baadhi ya watumishi wengine wanaobaki na kumbukumbu hasi ya mwaka 2016 ni pamoja na Henry Mchunga, Mkurugenzi wa Ugavi; Misanga Muja, Mkurugenzi Shughuli za Kanda ambaye pia alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa MSD kwa miaka mitatu; Cosmas Mwaifwani na Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Joseph Tesha.

 

error: Content is protected !!