Spread the love

 

JESHI la Polisi Mkoani wa Arusha, linamsaka mfanyakazi wa ndani (jina linahifadhiwa), akituhumiwa kuua mwajiri wake, Janerose Dewasi (66) mkazi wa Njiro Block D jijini hapa, baada ya kukutwa ameuawa nyumbani kwake kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Tukio hilo ni mwendelezo wa tukio kama hilo lilitokea siku chache zilizopita, baada ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite, Ruth Mmassy (40), kudaiwa kuuawa na mtoto wake eneo hilo hilo la Njiro na mwili wake kutumbukizwa kwenye chemba ya majitaka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Justine Masejo, jana alithibitisha kutokea tukio hilo na kueleza wanamsaka mfanyakazi wa ndani ambaye alikuwa anaishi na marehemu huyo na alitoweka baada ya tukio.

Kamanda Masejo alisema mwili wa mwanamke huyo aliyekuwa anaishi na mfanyakazi wa ndani kwenye nyumba yake, alionekana kupigwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso, huku akibainisha kuwa Polisi inamsaka mfanyakazi huyo wa ndani anayedaiwa kutoroka muda mfupi kabla ya kugundulika kwa tukio hilo.

“Uchunguzi wa awali, umebaini marehemu alikuwa anaishi na mtumishi wa kazi za ndani, ambaye alianza kazi wiki moja iliyopita ila alitoweka ghafla baada ya tukio hilo,” alisema.

Alifafanua mfanyakazi huyo alitoweka muda mfupi kabla ya kugundulika tukio hilo.

Kamanda alitoa mwito kwa wenye nyumba kuwa makini na wafanyakazi wa ndani wanaowapa kazi kwa kujua historia zao.

Mmoja wa majirani, Tedy Minja alisema mtuhumiwa huyo alikuwa hajulikani sana mtaani, kwani alianza kazi muda si mrefu na alikuwa akishinda ndani bila kutoka.

Kamanda Masejo aliwasihi viongozi wa dini kuendelea kutoa maombi kwa jamii ili kujitenga na matendo maovu.

Mauaji ya Ruth yaligundulika tarehe 24 Desemba, baada ya polisi kufika nyumbani kufanya upekuzi na kubaini mwili ukiwa ndani ya chemba ya choo.

Ruth alikuwa mfanyabiashara maarufu wa madini Arusha na Manyara ambaye inadaiwa aliuawa 11 Desemba 2021lakini mwili wake uligundulika wiki mbili baadaye – Desemba 24.

Kifo cha Ruth kilibainika baada ya binti yake aitwaye Patricia Mmasi (19), anayesoma China, kuingiwa shaka akiwa China kwani kila alipompigia simu mama yake, hakumpata.

“Huyu binti alikuwa anarejea nchini kutoka masomoni China. Alikuwa akipiga simu mara kwa mara kwa mama yake, lakini simu ilikuwa haipatikani.

“Alipofika nchini, alimwuliza kaka yake, yuko wapi mama? Majibu ya kaka yake, ndiyo yalimpa shaka, akalazimika kuwaambia ndugu na baadaye wakaripoti Polisi,” alieleza mtoa taarifa wa gazeti hili ambaye ni mmoja wa wanafamilia.

Marehemu Ruth alizikwa kijijini Mikungani, Arumeru, baada ya mwili wake kushindwa kufunuliwa ili kutolewa heshima za mwisho kutokana na kuharibika huku mwanawe Patrick Mmassy akiendelea kushikiliwa na Polisi kwa uchunguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *