January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatushangai kukimbiwa – Nape

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hakishangai wala kuhuzunika na wimbi la wanachama wake kuhama chama katika wakati huu kinapokabiliwa na ushindani mkali kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwamba suala la wanachama kuhama na kuhamia vyama vya upinzani ni jambo la kawaida na CCM haishangai.

“Kwa wale wanaohama CCM na kwenda Ukawa wanatakiwa kutambua kwamba hata walioanzisha vyama vya upinzani walitoka CCM. Wanaendeleza utaratibu wa kawaida. Kuondoka kwao sio jambo la ajabu, wengi wao wanaondoka kwa matatizo yao binafsi,” amesema Nape, katika kauli inayoashiria kama vile viongozi wakuu wa chama hicho hawaguswi na wimbi la makada kukitenga chama.

Nape ametoa kauli hiyo ndani ya mazingira yanayoonesha kukibomoa chama hicho kilichoko madarakani kwa miaka yote tangu jamhuri ilipojitawala baada ya uhuru. CCM ni zao la TANU na ASP, vyama vilivyoshiriki kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.

Makumi kwa makumi ya makada wake, wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu kama wenyeviti wa mikoa, jumuiya ya vijana, na wabunge wanaomaliza muda, wamekuwa wakitoka CCM na kuhamia kambi ya upinzani na hasa vyama vinavyoshirikiana katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

UKAWA, umoja ulioanzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba, umefanikiwa kusimamisha mgombea mmoja wa kiti cha urais wa jamhuri ambaye ni Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa shinikizo la bunge Februari 2008 na kiongozi aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Lowassa alihama CCM tarehe 25 Julai siku chache baada ya kulalamika kukatwa jina lake katika waombaji wa uteuzi wa kugombea urais kupitia CCM katika vikao vya juu vilivyofanyika mjini Dodoma. Alihamia Chadema na moja kwa moja kutunukiwa dhamana hiyo ya kuwakilisha UKAWA katika uchaguzi. Tangu hapo, amesababisha wanachama wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono alipokuwa CCM kumfuata.

Wenyeviti watatu wa mikoa wamejiengua CCM na kila mmoja kutoa malalamiko ya kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa taratibu ndani ya chama hicho vikiandamana na vitendo vya matumizi makubwa ya fedha katika kutafuta uongozi. Wenyeviti hao ni Mgana Msindai (Singida) ambaye aliwahi kuwa mbunge jimbo la Singida, Onesmo ole Nangole (Arusha), Khamis Mgeja (Shinyanga) na Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

Viongozi wa ngazi ya juu wa CCM waliojitokeza mapema kujiuzulu, walikuwa ni wabunge James Lembeli (Kahama), Esther Bulaya (Viti Maalum) na Goodluck Ole Medeye wa Arumeru Magharibi, pamoja na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Isaac Joseph, ambao kama hao wenyeviti, nao pia walihamia Chadema.

Lowassa alihama CCM na kujiunga Chadema baada ya jina lake kuondolewa kwenye hatua ya awali ya mchakato wa kupitisha wagombea wa urais bila kufuata utaratibu uliowekwa na chama hicho. Mchakato ambao umewagawa wanachama wa chama hicho.

Kabla ya kuondoka kwa Lowassa ndani ya CCM, wabunge Esther Bulaya (viti maalum) na mbunge wa Kahama James Lembeli waliondoka ndani ya chama hicho na kujiunga na Chadema huku wakifuatwa na mamia ya makada wa CCM.

Kada mwingine aliyeihama CCM katika wabunge ni Said Nkumba (Sikonge) ambaye wakati wa Bunge Maalum la Katiba alianzisha kundi lililoitwa Tanzania Kwanza, kwa lengo la kukabiliana na mkakati wa UKAWA wa kuitetea Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Nkumba anakumbukwa kwa kauli zake kali dhidi ya wajumbe wa UKAWA.

Kauli aliyoitoa Nape ya chama hicho kutopatwa hofu ya kukumbwa na wimbi la wanachama wake kuhama, imekuwa ikitolewa mara kwa mara na viongozi wa chama hicho ambao wanayoyasema yanatofautiana na yanayoelezwa na walio chini yao.

Sauti kubwa ya viongozi wa CCM inasikika ikilaumu makada hao kwamba wameondoka kwa kujali maslahi yao, na akitolea mfano wa Mgeja, aliyejiondoa Jumatano, Nape alisema kiongozi huyo ameamua kuondoka CCM kwa sababu binti yake aliyekuwa anawania kuteuliwa kugombea ubunge wa Viti Maalum, kushindwa kura za maoni.

“Pamoja na mambo mengine mengi, kwanza alitabiriwa kuondoka muda mrefu kumfuata rafiki yake Edward Lowassa, kilichokuwa kinamkalisha ndani ya CCM ni mwanaye wa kike aliyekuwa amegombea ubunge wa viti maalum akadhani atapita, bahati mbaya yule binti akapata kura chache sana.

“Ndugu Mgeja akajaribu kutumia uenyekiti wake wa Mkoa wa Shinyanga kumshawishi Katibu Mkuu wa CCM achakachue kura ili kumpitisha binti yake. Alipokataliwa, akaambiwa haiwezekani lazima ufuate utaratibu, Mgeja akatoka na hasira zake kwenda kuhama chama. Sasa hili ni suala binafsi sana,” alisema.

Mgeja ambaye hakupatikana kuzungumzia tuhuma alizozitoa Nape, alitoka CCM saa chache baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama kilichojadili na kupitisha majina ya wagombea ubunge. Mgeja alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu hiyo.

Katika hatua nyingine, Nape amesema kwamba taarifa zinazosambaa kwenye vyombo vya habari nchini kwamba mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ameahidi kuwapa walimu kote nchini kompyuta mpakato pamoja na Sh. 50 milioni kila kijiji iwapo watamchagua kuwa rais, hazina ukweli.

Amesema mgombea huyo hajawahi kutoa ahadi hiyo na kwamba hizo ni taarifa “zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo si za kweli.”

error: Content is protected !!