October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatuna uhaba wa mahindi – Serikali

Mahindi yakiwa shambani

Spread the love

SERIKALI imeeleza kutoridhishwa na upandaji wa bei ya mahindi, ikieleza kutokuwepo kwa uhaba wa bidhaa hiyo nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea),                                           

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 19 Novemba 2019 na Prof. Siza Tumbo Hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wakati akifungua mkutano wa kupokea tafiti kuhusu kuimarisha usalama wa chakula ndani na nje ya nchi.

Utafiti huo unatekelezwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Afrika (AGRA) na Wizara ya Kilimo.

Prof. Tumbo amesema, bei ya mahindi kwa sasa imepanda hadi kufikia Sh. 107,000, ambapo mwaka jana muda kama huu, bei ya gunia la mahindi lilikuwa ni sh. 65,000.

“Tunatakiwa kuangalia bei ya mahindi imeishapanda sana na mmesikia kidogo watu wameanza kuliongelea hili, bei imefika Sh.107,000 hizi ni  takwimu zetu rasmi ukifananisha na mwaka jana bei ilikuwa  sh.65,000  kipindi kama hichi.

“Kwa hiyo, sasa hivi bei imeishapanda hatujui, bei ya juu huwa inafikiwa Februari, hatujui mwakani itafikaje. Hatuwezi kukwepa mahindi kwasababu ni zao linalopendwa sana, bado tumefungua mipaka na chakula kinaenda ndani na nje,” amesema Prof.Tumbo.

Amesema, kwa sasa ukuaji wa uchumi kwenye kilimo ni asilimia 5.3 lengo likiwa ni kufikia asilimia 6.

“Ndio maana kelele hazipo kwenye usalama wa chakula, sasa hivi zipo kwenye biashara. Kuna wakati mwingine tunajisahau kujisifu tunabaki kwenye lawama, tunasahau kujisifu kwamba tuna usalama wa chakula, tunalalamika haturuhusiwi kuuza chakula nje ya nchi,” alisema na kwamba Tanzania ina chakula zaidi ya tani milioni 2.5.

Aidha, Prof.Tumbo amesema, katika kipindi cha Julai hadi Septemba, Tanzania imesafisha mihogo tani 5000 huku wanunuaji wakubwa ikiwa ni Burundi.

Vivian Kazi, Mkuu wa Idara ya Ushauri Elekezi kutoka Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), amesema wamefanya kazi nyingi za kitafiti zikiwemo kutoa ushauri katika kupitia sera mbalimbali za nchi.

Amesema, ESRF kwa kushirikiana na Agra pamoja na Wizara ya Kilimo, imekuwa ikitekeleza mradi wa kuimarisha usalama pamoja na biashara ya chakula ndani na nje ya nchi kuanzia Novemba 2018.

error: Content is protected !!