Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hatma ya Zitto Kabwe kesho
Habari za SiasaTangulizi

Hatma ya Zitto Kabwe kesho

Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalando
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kesho Ijumaa, tarehe 29 Mei, inatarajia kusoma hukumu ya kesi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Hukumu hiyo ya kesi namba 327/2018 ya uchochezi, inatarajiwa kuvuta hisia za watu mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania, itatolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Kesi hiyo iliyofunguliwa tarehe 2 Novemba 2018 na Jamhuri, itahitimishwa kesho kwa Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, ama kutupwa gerezani, kupigwa faini, kufungwa au kuachiwa huru.

Katika shauri hilo, upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi 15, huku Zitto akiwasilisha mashahidi nane.

Kesi ilisikilizwa kwa takribani mwaka mmoja na nusu. Ilishuhudia mchuano mkali wa mawakili wa pande zote mbili hasa wakati wa kupinga hoja na vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa.

Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga; huku Zitto akitetewa na mawakili watatu wakiongozwa na Jebra Kambole.

Mawakili wengine waliomtetea Zitto, ni Frank Mwakibolwa na Bonifacia Mapunda.

Upande wa serikali uliwasilisha vielelezo vya nyaraka na video iliyodaiwa kurekodiwa na askari mpelelezi kwenye mkutano wa Zitto na wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Oktoba 2018.

Video hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo tarehe 4 Desemba 2019, na Sajenti wa Polisi, James na kupokelewa baada ya mabishano kati ya upande wa utetezi uliotaka video hiyo kutopokelewa kwa kuwa sheria ya kieletroniki fungu namba 18 (2) (a).

Hatimaye Hakimu Shaidi alipokea ushahidi huo na video hiyo ilioneshwa mahakamani hapo.

Aidha, upande wa mashtaka, uliwaleta mahakamani mashahidi waliodai walilichukia jeshi la Polisi baada ya kumsikiliza Zitto. Mashahidi walieleza namna askari wa jeshi hilo walivyoua raia.

John Malulu, Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Polisi wa Kinondoni, ni miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri waliofika mahakamani kwenye kesi hiyo.

Katika ushahidi wake, Malulu aliiambia Mahakama kuwa aliwaona vijana wakizungumzia hotuba ya Zitto kwenye maeneo ya Manzese na Kimara, Dar es Salaam ambapo katika ushahidi wake alieleza aliwaona watu hao wamekasirika na kulichukia Jeshi la Polisi.

Zitto Kabwe

Tarehe 18 Februari 2020, Mahakama ilimkuta Zitto ana kesi ya kujibu, ndipo alipoanza kujitetea kuanzia tarehe 17, 18 na 19 Machi 2020.

Zitto alianza kujitetea mwenyewe kama shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi baadaye mashahidi saba.

Baadhi ya mashahidi wa utetezi walitoka kwenye kijiji cha Mpeta, Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma walioieleza mahakama wameshuhudia mapambano ya wananchi na askari yaliyopelekea mauaji ya wananchi na askari.

Awali, shauri hilo lilipotajwa siku ya tarehe 29 Aprili 2020, wakati upande wa utetezi ulipokuja kwa ajili ya kuwasilisha hoja zao za majumuisho huku upande wa jamhuri kuona hakuna haja ya kufanya hivyo.

Wakati huo huo Wakili Kweka, alidai shauri lilitajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya hukumu ambapo mshtakiwa (Zitto) hakuwepo na hakuna taarifa kuhusu kushindwa kufika kwake mahakamani.

Hakimu Shaidi alisema kuwa hati ya kukamatwa kwa Zitto itolewe na kuahirisha shauri hilo mpaka tarehe 29 Mei kwa ajili ya kutoa hukumu.

Katika kesi hiyo inadaiwa tarehe 28 Oktoba 2018, Zitto aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, akiwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Mshtakiwa anadaiwa alitamka kuwa “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua’’

Katika mashtaka ya pili ilidaiwa tarehe 28 Oktoba 2018, mwaka juzi maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’ lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya.

“Taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kiheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa.’’

Ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema “tumekuwa tukifuatilia kwa kia yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!