July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatma ya Geita, Polisi Tabora Machi 20

Spread the love

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itatoa maamuzi ya upangaji wa matokeo unaozikabiri timu za Geita Gold Mine na Polisi Tabora, anaandika Regina Mkonde.

Jamal Malinzi, ambaye Rais wa TFF, amesema kesi hiyo wameikabidhi Kamati ya Nidhamu na mpaka Machi 20 watatoa maamuzi.

Malinzi ameyasema hayo wakati akisaini mkataba endelevu wa mpango wa maendeleo ya mpira wa miguu wa wanawake nchini leo, katika ofisi za TFF zilizopo jijini Dar es Salaam.

“Kumetokea malalamiko mengi juu ya upangaji wa matokeo uliofanywa na mechi mbili za mwisho zilizochezwa na timu za Geita na Polisi Tabora,” amesema Malinzi.

Malinzi amesema kuwa, Shirikisho halitakaa kimya juu ya tuhuma hizo, na kwamba kuna kanuni zinazoendesha ligi na mamlaka zake ambazo zinapinga upangaji wa matokeo.

“Katika mchezo wa mpira wa miguu, kupanga matokeo ni kosa kama ilivyo makosa mengine, na mhusika anaweza akapata adhabu ya kifungo cha maisha, kama ni timu itashushwa daraja,” amesema.

Malinzi amesema, Kamati ya Nidhamu ya TFF inafuata kanuni za nidhamu na sheria na kwamba, Shirikisho limefungua mashitaka ambapo maamuzi yake yatatolewa Machi 20 mwaka huu.

“Taratibu za kisheria zimeanza kufuatwa, ushahidi na vilelezo vimeshaandaliwa na wanaotuhumiwa wameandikiwa barua za kushitakiwa,” amesema.

Geita FC na Polisi Tabora zinashutumiwa kupanga matokeo kwenye mechi zake za mwisho za ligi hiyo, ambapo zilicheza siku moja na wakati unaofanana.

Timu ya Polisi Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya Oljoro Arusha, wakati Geita baada ya kusikia Polisi Tabora ina matokeo mazuri, iliongeza goli moja na kuwa na mabao 8-0 zidi ya JKT Kanembwa.

Geita ilifanya hivyo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupanda daraja na kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

TFF imesaini mkataba na wadhamini wa mpango huo ambao ni Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Association, ikiwa na lengo la kuinua vipaji vya wasichana na kufufua soka la wanawake nchini.

error: Content is protected !!