August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatma mkataba TICTS Septemba

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema hatma ya mkataba Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makasha (TICTS)  itajulikana mwezi Septemba mwaka huu. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea). 

Kauli ya Waziri Mbarawa inakuja baada ya wadau wa sekta za biashara, usafirishaji na vyama vya siasa wakiishauri Serikali kutoipa mkataba mpya TICTS kwa madai yakushindwa kujiendesha kwa ufanisi na kusababisha msongamano wa makasha bandarini.

Katika siku za hivi karibuni Chama cha ACT-Wazalendo kiliishauri Serikali kutoipa  TICTS mkataba mpya wa kuendesha eneo la makasha la Bandari ya Dar es Salaam kikidai kuwa kampuni hiyo imeshindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka, na kuwekeza kwenye miundombinu ya bandari.

Waziri Mbarawa amesema hayo leo tarehe 4 Agosti, 2022 wakati akielezea waandishi wa habari kuhusu namna wizara yake ilivyojipanga kutekeleza Bajeti ya 2022/2023 katika sekta zake za ujenzi na uchukuzi.

“TICTS inafanya kazi kisheria, kuna mkataba kati ya Serikali na TICTS yenyewe, mkataba wenyewe utamalizika mwezi wa tisa, kwenye mkataba kuna mambo mengi yaliongolewa na kwa sasa kuna mazungumzo yanaendelea baina ya Serikali na mwekezaji huyo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa

Sasa kama tutaongeza au hatuongezi, hapa sio mahali pake, siku ikifika tutawaita tutawaambia kwanini tumeongeza au hatujaongeza,” alisema.

Prof. Mbarawa alisema kitu ambacho kimetokea kwenye mkataba huo ni kuwepo kwa vigezo, ambapo vipo ambavyo ametekeleza na vingine hajatekeleza.

Alisema kuhusu magari kuchelewa kutoka hana uhakika kuwa ni moja ya kigezo, huku akisema anachofahamu kuhusu kuchelewa kutoka ni uwepo wa mizani ambayo ilikuwa inapima magari.

Waziri alisema pia uchunguzi wao ulibaini kuwa foleni ya magari ilikuwa ikisababishwa na madereva kwenda kusubiria kuingia bandarini wakiwa katika eneo la bandari jambo ambalo wamelizuia kwa sasa.

“Wapo watu walikuwa wanaenda bandari na kuhifadhi magari na wengine wanalala jambo ambalo tumezuia kwa sasa na matokeo yanaonekana kuwa mazuri,” alisema.

error: Content is protected !!