January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatma mapingamizi ya kina Mbowe Ijumaa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, imepanga Ijumaa tarehe 17 Desemba 2021, kutoa uamuzi wa mapingamizi ya utetezi, dhidi ya kupokelewa hati ya ukamataji mali ya mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassan. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika kesi ya ugaidi inayowakabili washtakiwa wanne, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freemam Mbowe

Siku hiyo imepangwa leo Jumatano, tarehe 15 Desemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya kupokea hoja za pande zote mbili, dhidi ya mapingamizi hayo.

“Naomba niwapangie kutoa uamuzi kesho kutwa siku ya Ijumaa, tarehe 17 Desemba 2021,” amesema Jaji Tiganga.

Mapingamizi hayo yaliibuka mahakamani hapo, baada ya shahidi wa nane wa Jamhuri, Mkuu wa Upelelezi wilayani Arumeru, Arusha, SP Jumanne Malangahe, kuiomba ipokee kama sehemu ya ushahidi wake.

Baada ya kutoa ombi hilo, mawakili wa utetezi wakiongozwa na wakili wa mshtakiwa huyo, Nashon Nkungu, waliweka mapingamizi likiwemo lililodai nyaraka hiyo haina uhusiano huku lingine likidai haina uwezo wa kupokelewa kwa kuwa imechukuliwa kwa sheria ambayo haipo.

Pingamizi lingine lilidai, shahidi aliyeomba kuitoa nyaraka hiyo, ameshindwa kuithibitisha kama ndiyo yenyewe aliyoiandika tarehe 10 Agosti 2020, baada ya kukagua nyumbani kwa Hassan, maeneo ya Yombo Kilakala, Temeke jijini Dar es Salaam.

Pingamizi lingine lilidai, shahidi huyo hajaonesha mlolongo wa  utunzwaji kielelezo hicho hadi kilipomfikia mahakamani hapo (Chain of Custody), wakati anatoa ushahidi.

Lingine lilidai shahidi huyo aliingiza kinyemelea taarifa ambazo hazijasainiwa na mshtakiwa pamoja na mashahidi walioshuhudia zoezi la upekuzi huo.

Hata hivyo, Mawakili wa Jamhuri wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, waliiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali mapingamizi hayo, wakidai hayana mashiko kisheria.

Kuhusu pingamizi la SP Malangahe kutothibitisha hati hiyo ya ukamataji mali, walidai , shahidi wao aliithibitisha mahakama hiyo kuwa nyaraka hiyo ndiyo aliyoifanyia kazi wakati anakagua nyumbani kwa Hassan.

Mawakili hao walidai nyaraka hiyo ina uhusiano na uwezo wa kupokelewa, kwa kuwa imeandaliwa kwa sheria iliyotungwa na Bunge.

error: Content is protected !!