August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatimaye Dk. Dau apata kazi mpya

Spread the love

SUBIRA yavuta heri. Hatimaye Dk. Ramadhani Dau aliyekuwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kabla ya kung’olewa na Rais John Magufuli, amepewa kazi mpya, anaandika Charles William.

Dk. Dau ameapishwa leo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Aziz Ponary Mlima ambaye kwa sasa ni Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Februari Mwaka huu, ikiwa ni miezi minne tu tangu Rais Magufuli kuingia madarakani, Dk. Dau aliondolewa katika nafasi yake NSSF huku akiahidiwa kupangiwa kazi nyingine. Amekaa na kusubiri kwa miezi saba na sasa amepewa kazi hiyo mpya.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu Februari mwaka huu, ilisema Dk. Dau, Dk. Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe wametuliwa kuwa mabalozi katika nchi zitakazotangazwa hapo baadaye, hata hivyo ni Dau pekee ambaye alikuwa akisubiri kupangiwa nchi ya kwenda.

19 April mwaka huu, Mathias Chikawe aliapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, huku tarehe 5 Mei mwaka huu Dk. Migiro  akiapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza. Dk. Dau aliendelea kusubiri na hali ikiwa tete katika NSSF, taasisi aliyokuwa akiiongoza.

15 Julai mwaka huu, wakurugenzi sita wa NSSF waliokuwa wakifanya kazi chini ya Dk. Dau waliondolewa kwenye nafasi zao kutokana na kujihusisha na ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.

Wengi waliamini hatua hiyo ilikuwa inazidi kumuweka pabaya Dk. Dau kwani ubadhirifu na matumizi mabaya waliyotuhumiwa kuyafanya wakurugenzi wa idara mbalimbali za NSSF, yaifanyika wakati yeye akiwa Mkurugenzi Mkuu akiwa na jukumu la kuwasimamia.

Hata hivyo kuapishwa leo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, kunathibitisha kuwa Dk. Dau bado yupo salama chini ya serikali ya Rais Magufuli. Bado anahitajika na amepewa majukumu mapya ya kuliwakilisha taifa. Amekuwa kama Nabii Daniel aliyetupwa katika shimo la Simba wenye njaa na akanusurika!

error: Content is protected !!