June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hatima ya Assange kesho

Spread the love

JULIAN Assange, Mmiliki wa mtandao wa kihabari maarufu duniani wa WikiLeaks, amesema atakuwa hana chaguo isipokuwa kusalimu amri iwapo Umoja wa Mataifa utaamua kuwa amezuiliwa ubalozini Ecuador jijini London kihalali. Anaandika Jabir Idrissa.

“Iwapo UN itaamua kesho kuwa nimeshindwa kesi dhidi ya mamlaka ya Uingereza na Sweden, nitaondoka ubalozini (kesho) Ijumaa ili niwe huru kukamatwa na polisi wa Uingereza kwa kuwa haitakuwa na maana tena kukata rufaa,” amesema.

“La nikishinda na serikali hizi mbili zinazoshirikiana kunizuia zikikutwa zimechukuwa hatua isivyo halali dhidi yangu, basi nitatarajia kukabidhiwa pasipoti yangu na kufutwa kwa amri za kutakiwa kukamatwa,” ameongeza.

Jopo la wanasheria wanaoshughulikia masuala ya kuwekwa kizuizini, linatarajiwa kutoa uamuzi wake Ijumaa hivyo kumaliza mgogoro wa miaka mitatu kati ya Assange na mamlaka za Uingereza na Sweden, zinazomtaka kwa ajili ya kushitakiwa mahakamani kwa tuhuma za ubakaji na kufanya ujasusi.

Assange, 44, ambaye ni raia wa Australia, aliomba hifadhi ya kisiasa kwenye ubalozi wa Ecuador nchini Uingereza mwaka 2012 katika jitihada zake za kukwepa kusalimishwa kwa mamlaka ya Sweden anakodaiwa alihusika na ubakaji. Amekanusha tuhuma hizo.

Polisi wa Uingereza wameshasema watamkamata akiondoka ubalozini Ecuador.

Mwendesha Mashitaka wa Sweden amesema uamuzi wa jopo la Umoja wa Mataifa hautakuwa na nguvu ya kisheria kuhusu uchunguzi unaoendelea dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Assange, ambaye alikamatwa mara ya kwanza mwaka 2010 jijini London, amesema pasipoti yake italazimika kurudishwa na amri ya kumkamata ifutwe iwapo uamuzi utakuwa upande wake.

Alikamatwa kwa utaratibu wa kisheria wa Jumuiya ya Ulaya amri iliyotolewa na Sweden anakotuhumiwa kwa makosa ya ubakaji na udhalilishaji.

Mwaka 2012 akiwa amedhaminiwa, aliomba hifadhi akiwa Ubalozi wa Ecuador eneo la Knightsbridge, Uingereza baada ya Mahakama ya Juu ya Uingereza kuamuru akamatwe na kupelekwa anakotakiwa.

Mwendesha Mashitaka nchini Sweden alimuondolea Assange mashitaka ya udhalilishaji lakini bado anakabiliwa na tuhuma za kubaka. Mwaka 2014 Assange alilalamika Umoja wa Mataifa kwamba anawekwa kizuizini isivyo halali kwa kuwekwa katika mazingira ya kutoweza kuondoka Ubalozini kwa kuwa atakamatwa.

Katika malalamiko yake alidai ananyimwa uhuru wake katika mazingira mabaya na kwa muda usiokubalika.

Maamuzi muhimu yanayosubiriwa ni kuhusu kwamba Assange anahitaji fursa ya kupata hifadhi ya kisiasa, kwa kuwa hajashitakiwa, na hakuna mabadiliko ya sheria ya Uingereza tangu alipojichimbia Ubalozini.

Mtandao wake wa Wikileaks ulieleza mapema kwamba unasubiri uthibitisho wa uamuzi wa UN.

Makao makuu ya mamlaka ya Serikali ya Uingereza imesema uamuzi wa jopo utakosa nguvu ya kisheria wakati amri ya kumkamata itakuwa na nguvu.

“Tumekuwa na uhakika kwamba Assange hajazuiwa kinyama na Uingereza isipokuwa yeye mwenyewe anajitahidi kukwepa kukamatwa kwa kuamua kujichimbia Ubalozini Ecuador.

“Uingereza ingali na jukumu la kisheria la kumkamata na kumsafirisha nchini Sweden,” imesema taarifa ya serikali ya Uingereza.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden imesema inafahamu kwamba uamuzi wa UN unatofautiana na wa serikali ya Sweden.”

Ikasema utaratibu wa kisheria kuhusu tuhuma zinazomkabili Assange utashughulikiwa na mahakama na waendesha mashitaka wa Sweden.

Wakili wake, Per Samuelsson, amesema serikali ya Sweden itakuwa inatenda sivyo kuendelea kuchunguza iwapo jopo litaamua hana tatizo.

Assange amekuwa akiamini kuwa akikamatwa atapelekwa Marekani na kushitakiwa kwa tuhuma za ujasusi baada ya kuchapisha siri za Marekani kwenye mtandao wa intaneti. Marekani imekuwa ikishinikiza akamatwe na kupelekwa huko kushitakiwa.

Oktoba mwaka jana kikosi cha upelelezi cha Uingereza, Scotland Yard, kilisema hakitaweka lindo tena nje ya Ubalozi wa Ecuador katika mpango uliogharimu Pauni 12 milioni. Lakini kimesema “kuna njia mbalimbali za siri na dhahiri za kumkamata.”

error: Content is protected !!