HATIMA ya gharama za tozo ya miamala ya simu kupungua au kubaki kama zilivyo itafahamika leo Jumanne tarehe 31 Agosti 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Tozo hizo zilizoanza kukatwa tarehe 15 Julai 2021, ziliibua malalamiko kwa wananchi jambo lililomfanya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuagiza kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa malalamiko ya wananchi.
Rais Samia alimwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Tehama), Dk. Faustine Ndugulile kushughulikia suala hilo, ili licha ya kukusanya tozo hizo na kuzipeleka katika miradi ya maendeleo, wananchi wasiumie.
Jumamosi, iliyopita tarehe 29 Agosti 2021, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa alisema, taarifa ya mapitio kuhusu suala hilo umekamilika na kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Msigwa alisema, tozo hiyo ipo kwa mujibu wa sheria hivyo hata kushughulikia suala hilo, inahitaji umakini ili kutovunja sheria iliyopo ambayo ilipitishwa na Bunge.
“…kwa hiyo taarifa itatolewa tarehe 31 Agosti 2021 ya namna gani serikali ilivyolishughulikia,” alisema Msigwa.
Wakati Serikali ikijiandaa kutoa taarifa yake, tayari kuna kesi zimefunguliwa wadau mbalimbali Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga tozo hizo kwamba zinamuumiza mwananchi.

Mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma, Frank James akizungumza na MwanaHALISI Online amesema “mimi matarajio yangu ni serikali imeona yenyewe malalamiko ya wananchi, bila shaka itapunguza kwani makato yamekuwa yanaumiza sana.”
“Fikiria unayetuma unakatwa na anayepokea anakatwa. Yaani kwenye elfu ishirini mnaweza kukatwa kama elfu tatu hivi, sasa hii si ni kilo kabisa ya sukari? Ngoja tusubiri kuona serikali inakujaje,” amesema.
Kwa upande wake, Mkazi wa Kigoma, Nasra Abdallah amesema, yeye anasubiri kuona hali itakavyokuwa “lakini serikali ikicheza na tozo hizi, mwaka 2025 katika uchaguzi mkuu, itajifunza kitu.”
yahya