September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Hati ya mashtaka katika kesi ya Mbowe na wenzake yarekebishwa

Spread the love

 

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi Na. 16/2021, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema na wenzake, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, umerekebisha hati ya mashtaka iliyotumika kufungua kesi hiyo yenye mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 10 Septemba 2021 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, mbele ya Jaji Mustapha Siyani, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa katika hatua za awali.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

Wakili Kidando amesema, wamefanya marekebisho katika hati hiyo baada ya mahakama hiyo kuulekeza upande wa mashtaka kuifanyia marekebisho katika shtaka la kwanza, nne na la sita.

“Jaji kesi hii ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa katika hatua ya awali, tuko tayari kuendelea kusikiliza na tulishawasilisha hati ya mashtaka yenye marekebisho mahakamani na kwa mawakili wa utetezi,” amesema Wakili Kidando.

Baada ya Wakili Kidando kuyasema hayo, Jaji Siyani alielekeza upande wa mashtaka kuwasomea upya washtakiwa mashtaka.

Washtakiwa hao wameyakana mashtaka yote waliyosomewa na kesi hiyo kuendelea kusikilizwa.

Mashtaka yaliyoagizwa kufanyiwa marekebisho ni shtaka la kwanza, ambalo ni la kula njama za kutenda vitendo vya ugaidi, linalowakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, maeneo ya mikoa ya Arusha, Morogoro na Dar es Salaam.

Shtaka la nne la kushiriki vikao vya kutenda kosa la ugaidi linalowakabili wote, wanalodaiwa kutenda kati ya tarehe 1 Mei hadi 5 Agosti 2020, kwenye Hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro.

Huku la sita likiwa ni la kumiliki mali, ambayo ilikuwa itumike katika kosa la ugaidi, linalomkabili Bwire peke yake.

Hati hiyo ya mashtaka imerekebishwa baada ya upande wa utetezi kuiwekea mapingamizi, ikidai kwamba ni batili, hatua iliyopelekea mahakama hiyo mbele ya Jaji Elinaza Luvanda, kabla ya kujitoa katika usikilizwaji wa kesi hiyo, kuuamuru upande wa mashtaka kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka.

Katika mapingamizi hayo, upande wa utetezi ulidai mashtaka yaliyokuwemo katika hati hiyo yamejirudia rudia.

error: Content is protected !!