January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hassanali: Nitavunja ngome ya Zungu

Spread the love

MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Ilala (Chadema), Musilim Hassanali amesema, atavunja ngome ya mgombea wa CCM, Mussa Zungu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Anafafanua, maeneo yote ambayo Zungu anaamini amejiimarisha, ataingia na kukomba wanachama wapya kwa kuwa, chama chake kimechokwa.

Akizungumza na mwandishi wa MwanahalisiOnline baada ya kurejesha fomu ya kugombea ubunge katika Ofisi za Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Hassanali amesema, akiingia madarakani jimbo hilo litapata taswira mpya inayoakisi maendeleo.

Hassanali amekuwa mdhamini wa Chadema kwa miaka 13 mfululizo na kugombea nafasi ya ubunge kwenye maeneo matatu tofauti. Ni mfanyabiashara maarufu nchini.

Amesema ana kazi kubwa ya kurekebisha madudu yaliyofanywa na CCM kwa kipindi cha miaka 54 tangu Uhuru.

“Yaani nashidwa hata kusema nitaanza na kipi maana katika idara zote CCM hakuna kipya wala kizuri walichokifanya, nitakuwa na kazi ya kuboresha kila sekta ili wananchi wangu wa Ilala wapate maisha bora na kuondokana na umaskini,” amesema Hassanali.

Katika maboresho hayo amesema, kuna mambo ambayo atayapa kipaumbele katika kuleta maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, ajira kwa vijana wakiwemo wafanyabiashara wadogowadogo pamoja na kukomesha suala la ukabila.

Vipaumbele vingine ni kuwapatia fursa mamalishe, msongamano wa magari bila sababu na kufuta sheria kandamizi ambazo ziliwekwa na CCM ili kuwanyima fursa za maendeleo vijana. Kuhusu kuwepo kwa ubaguzi wakati wa kuandika wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) hasa jamii ya wahindi amesema, CCM imesahau ilikotoka na kwamba, wawekezaji wazawa na wasio wazawa ndio waliosaidia kuikomboa nchi hii.

“Nikifanikiwa kuchaguliwa, nitakomesha ukabila kwani wawekezaji ndio wanasaidia vijana wengi nchini kwa mfano wahindi ukiwafukuza unawaumiza Watanzania wengi. Nchi yetu sio masikini bali sera haziwapi fursa wananchi.

“Nikiwa Mbunge wa Ilala nitahakikisha nawasaidia vijana hasa hawa wamachinga ambao kila siku wanahangaishwa na hawana sehemu malumu ya biashara. Nitahakikisha tabu hiyo inaisha kwa kuwapatia eneo nzuri,” amesema.

Hata hivyo amesema hana chuki na Zungu lakini anaichukia CCM hivyo amewaomba wakazi wa jimbo hilo kuungana ili kumwangamiza mdudu CCM.

 

error: Content is protected !!