July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hassanali aanza safari ya kumng’oa Zungu Ilala

Spread the love

MGOMBEA Ubunge katika Jimbo la Ilala kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Muslim Hassanali amezindua rasmi kampeni zake katika jimbo hilo la mkoani Dar es Salaam. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hassanali ambae pia amepania kuziangusha ngome za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumuondoa mbunge aliyejichimbia kwa vipindi viwili, Mussa Zungu, katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kuwapatia wananchi wa Ilala maendeleo wenye kiu nayo.

Hassanali ambaye amezindua kampeni zake leo kwenye viwanja vya Karume Sokoni amewaahidi wakazi wa jmbo kuwa tayari kwa ajili ya kupokea mabadiliko kutoka katika muungano unaoundwa na vyama vinne – Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

UKAWA unaundwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama Cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), ambapo amesema kwa kupitia muungano huwa viongozi wa chini watakuwa na nguvu ya kuleta maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kupanda jukwaani kuwahutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza katika viwanja hivyo Hassanali amesema muda wa mabadiliko kwa wakazi wa Ilala ni sasa hivyo CCM ijiandae kung’oka madarakani.

“Mmewapa CCM dola kwa miaka 54 sasa walichokifanya hamna miaka yote hiyo, ni zamu yetu wananchi naombeni mtupe sisi dola mwaka huu na kuahidi ndani ya miaka mitano tu mtaona mabadilko. Watanzania wasubiri neema mwaka huu,” amesema Hassanali.

Amesema umuhimu wa kuiondoa CCM unakuja kwa kuwa chama hicho kimelea na kulinda mfumo wa uongozi uliokwamisha maendeleo ya haraka ya wananchi, jimboni Ilala na nchi nzima. Amesema mfumo huo unakandamiza haki za wananchi na unachelewesha huduma za jamii zenye ufanisi

Hassanali ametaja baadhi ya maeneo ya kushughulika nayo atakapokuwa mbunge kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya barabara jimboni, ukosefu wa ajira kwa vijana, mitaji ya biashara ndogo, elimu duni.

Amesema kuna mfumo wa ubaguzi kwa wafanyabiashara akijitaja mwenyewe kuwa ingawa amezaliwa jimboni Ilala anachukuliwa kama Mtanzania mwenye asili ya India.

Katika hafla ya uzinduzi wa kampeni yake, pia walihudhuria viongozi wa dini, viongozi wa waendesha bodaboda, machinga, soko la Karume.

Hassanali amekuwa mdhamini wa Chadema kwa miaka 13 mfululizo na kugombea nafasi ya ubunge kwenye maeneo matatu tofauti.

error: Content is protected !!