July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hashim Rungwe: Rais Samia amewakosea Watanzania

Hashim Rungwe, Mwenyekiti wa Chaumma

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amewakosea Watanzania, kufuatia msimamo wake wa kuweka kando mchakato wa upatikanaji Katiba mpya. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Rungwe ameyasema hayo leo Jumanne, tarehe 6 Julai 2021, akizungumza na wanahabari ofisini kwake, Makumbusho mkoani Dar es Salam, kuhusu kauli Rais Samia ya kutofufua mchakato huo uliokwama 2015, ili asimamishe uchumi wa nchi.

“Tunastahili kutendewa haki, wananchi waastahili kupata haki kutoka kwa Serikali yao, akianza kudai anataka kupewa nafasi ina maana anaikanyaga Katiba. Hakuna hata sehemu moja ambayo imeandikwa kwa bahati mbaya, hili jambo ni muhimu kwa hiyo anatakiwa atekeleze,” amesema Rungwe.

Rais Samia alitoa kauli hiyo akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini, mwishoni mwa Juni 2021, ambapo aliomba apewe muda wa kusimamisha uchumi wa nchi. Kisha ataanza kushughulikia mchakato wa upatikanaji katiba mpya.

Rungwe ameipinga kauli hiyo akisema kwamba, mtangulizi wake Hayati John Magufuli alitoa sababu hiyo hiyo, wananchi walipokumbushia mchakato huo.

“Watu wa vyama vya siasa tulipiga kelele sana, kwa mtangulizi wake aliposema anataka apewe nafasi ainyooshe nchi kwamba imepinda na nafikiri ni mimi pekee ndio nilihoji nchi imepinda wapi,” amesema Rungwe.

Rais wa Tanzania,
Samia Suluhu Hassa

Mwanasiasa huyo amesema vuguvugu la kudai Katiba mpya nchini, lisimama katika uongozi wa Magufuli, baada ya wanasiasa na wanaharakati kuhamia katika mapambano ya kupinga masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Lakini baadaye mjadala ulibadilika watu wakawa wanazungumzia kuhusu ukiukwaji wa haki, mjadala wa Katiba ukasimaa. Rais Samia ametukosea sana, ametuweka kwenye jicho la unyonge sana. Sisi tunasema Mama Samia unayo mamlaka, hayo mengine ya uchumi ni ya kwako, sis tufungulie funga njia,” amesema Rungwe.

Kuhusu mikutano ya vyama vya siasa, Rungwe amemuomba Rais Samia aondoe zuio hilo lililowekwa na mtangulizi wake, Magufuli.

“Sisi tumeambiwa tusubiri na suala la kujaribu hatuwezi kufanya, kwa sababu kujaribu ni hatari. Kwanza tulishazuiwa kufanya nikutano na mlango bado haujafunguliwa, hivyo hata vyombo vya ulinzi na usalama vinajua haturuhusiwi, tutaumizwa bure. Hatuna nguvu kama walizonazo hao waliosema watafanya mikutano bila kauli ya rais,” amesema Rungwe.

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiendelea na vikao vya bunge hilo

Mchakato wa Katiba mpya ulianza 2011 chini ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83 /2011 ilitungwa pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Mchakato huo uliishia Aprili 2015, katika maandalizi ya wananchi kuipigia kura Katiba pendekezwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), kuahirisha zoezi hilo kutokana na uandikishaji daftari la wapiga kura kutokamilika.

Magufuli aliyefariki dunia akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, aliukwepa mchakato huo akisema kwamba anataka kuinyoosha nchi.

error: Content is protected !!