December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Haramu kwa haramu Z’bar

Spread the love

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inasaka wateja wa kushiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi mwaka huu ili kukivusha Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Faki Sosi.

Haramu huende kwa haramu, ndivyo inaweza kuwa tafsiri ya kile kinachoendelea visiwani Zanzibar kwa sasa.

Uchaguzi wa marudio umeitishwa kinyume cha sheria na unaendeshwa kinyeme cha sheria. Taratibu na kanuni zote zimezikwa na sasa ni ‘bora liende.’

Sheria ya uchaguzi ipo wazi kuwa, hakuna mgombea binafsi na kwamba ni lazima kwa mgombea yeyote kuwa ni mwanachama wa chama fulani.

Licha ya Khamis Idd Lila aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar kutimuliwa kwa madai ya kununuliwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kushiriki uchaguzi wa marudio, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inambeba na kumpa ulinzi kama mgombea.

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo hivi karibuni alizungumza na waandishi wa habari akieleza msimamo wa chama hicho kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Si Lila pekee anayebebwa na ZEC, Hamad Rashidi aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) ambaye amesimamishwa uanachama na chama chake, ZEC inampa ulinzi kama mgombea urais halali wa uchaguzi huo.

Kwa sasa Salim Khamis Ali, Mkurugenzi wa Uchaguzi visiwani humo amekabidhi walinzi kwa Hamad na Lila ambao hawana uhalali wa kuwakilisha vyama vyao kwenye uchaguzi huo.

Ali Khatibu Ali, Mgombea wa Chama Cha Kijamii (CCK) naye amejumuishwa kwenye uchaguzi huo lakini Constantine Akitanda, mwenyekiti wa chama hicho hana taarifa.

Akitanda ni miongoni mwa viongozi wa vyama walioeleza hadharani msimamo wao wa kutojiingiza kwenye marudio ya uchaguzi yaliyotangazwa na ZEC. Tume imempa ulinzi mteja wake Ali.

Isaa Mohammedi Zonga wa Chama cha Sauti ya Umma) naye amepewa ulinzi na ZEC licha ya chama hicho kueleza kwamba hakitashiriki uchaguzi huo.

Wiki mbili zilizopita viongozi wa SAU walijitokeza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakieleza kugomea marudio ya uchaguzi yaliyotangazwa na ZEC kwa madai ya kutokuwepo uhalali wa kufanya hivyo.

Vyama visivyo na mgogoro katika marejeo ya uchaguzi huo ni CCM kinachowakilishwa na Dk. Ali Mohammedi Shei; Juma Ali Khatibu akikiwakilisha Tadea; Soud Said Soud akiiwakilisha APF na Hafidh Hassan Seleiman wa TLP. Vyama ambavyo vimegomea uchaguzi huo mpaka sasa ni 10.

Hata hivyo, zipo taarifa kuwa CCM inawasaka viongozi wa NRA ili kuwarubuni na hatimaye kukubali kushiriki uchaguzi huo.

“Ni kweli harakati hizo zipo na wanaohusika wameanza kazi hiyo ili wafanikiwe haraka kabla ya kupinduka kwa mwezi huu,” anasema mtoa taarifa aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.

Mtandao huu wiki hii uliripoti kuwepo kwa taarifa ya CCM kusambaza fedha kwa vyama vya upinzani vilivyo na mgogoro wa kushiriki ama kutoshiriki uchaguzi huo ili kuvirubuni kushiriki.

error: Content is protected !!