July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hamburg yaisaidia Kinondoni mradi bil 3.5

Spread the love

MANISPAA ya Kinondoni kwa ushirikiano na Manispaa ya Jiji la Hamburg, nchini Ujerumani ziko katika hatua za mwisho za ujenzi wa mradi mkubwa kwa ajili ya kukusanya taka zinazooza na kuzizalisha kuwa mbolea ambao utagharimu Euro Mil. 1.6 ambazo ni sawa na Sh. 3.5 bilioni utakapokuwa umekamilika na kuanza kazi ifikapo Juni 2016. Anaandika Josephat Isango … (endelea).

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake Meya Jacob amesema kuwa baada ya mradi kukamilika kutakuwa na uhakika wa kukusanya na kuzoa nusu ya taka zote zinazozalishwa kwa siku katika manispaa hiyo ambazo kwa sasa zinakadiriwa kuwa tani 2,026.

Meya huyo pia alitumia fura hiyo kumtambulisha Mwakilishi wa Jiji la Hamburg ambaye atakuwa Mtaalam Mshauri wa Mradi huo, Dkt. Florian Koelsch.

Meya ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo utakaoanza na kuweka mitambo yake (compost plant) itakayokuwa ikibadilisha taka zinazooza kuwa mbolea, utaanza mwezi mmoja ujao katika eneo la Mabwepande, jijini Dar es Salaam,

Aliongeza kuwa mradi huo unaanza kutekelezwa siku chache baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, akiongeza kuwa manispaa hizo mbili ambazo ziko katika ushirikiano zilipeana majukumu ya kufanya ambapo Jiji la Hamburg walikubali kufadhili ujenzi na usimamizi kwa mwaka mmoja utakapokuwa umekamilika na Manispaa ya Kinondoni ilipewa jukumu la kutafuta ardhi ya kujenga mitambo hiyo.

“Tayari tumepata ardhi takriban ekari 20 katika Kata ya Mabwepande. Kazi ya ujenzi itaanza mwezi mmoja ujao kwa maana ya kufunga mitambo, inakadiriwa ndani ya mwaka mmoja hadi Juni mwakani mradi utakuwa tayari unaanza kazi. Kwa upande wetu kwa kweli tuko tayari,” amesema Meya Jacob.

Meya amewahakikishia wananchi wa Kinondoni kuwa yeye pamoja na baraza la madiwani analoliongoza kwa kushirikiana na watendaji, wamejipanga kikamilifu kuwatumikia wananchi kwa kuzifanyia kazi kero mbalimbali, likiwemo suala la kuhakikisha manispaa inakuwa safi kimazingira.

“Tumejipanga ipasavyo…tunataka uchafu uwe mahali panapostahili ama kwa kuzalishwa kuwa mbolea ua kuchomwa moto. Nashukuru tangu nimeingia tunaendelea kupata uungwaji mkono wa wadau mbalimbali. Kuna mpango mwingine wa kuwa na dampo la kuchoma taka, dampo tanuru. Ukikamilika pia tutawataarifu,” ameongeza Meya Jacob.

Amesema kuwa kwa sasa Manispaa ya Kinondoni inazalisha taka takriban tani 2,026 kila siku kutokana na shughuli za mtu mmoja mmoja (majumbani) na katika taasisi kv; masoko, shule n.k, ambapo kwa sasa manispaa hiyo ina uwezo wa kukusanya na kuzoa robo ya taka hizo huku changamoto ya kumaliza kero hiyo ikiwa bado ni kubwa ndiyo maana kupitia uongozi wake wanabuni miradi mbalimbali kupata suluhisho la uhakika kusafisha manispaa hiyo.

Kwa upande Dkt. Koelsch amesema kuwa Jiji la Hamburg litafurahi iwapo mradi huo utaanza haraka iwezekanavyo kabla mwaka wa fedha wa bajeti ya Ujerumani haujaisha.

Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya ushirikiano wa pande zote hizo mbili ambao anatarajiwa utaendelea kuimarishwa kwa manufaa na maslahi ya wananchi wa nchi zote mbili.

error: Content is protected !!