June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Hamadi Rashid ajihalalisha ADC

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid akifafanua jambo

Spread the love

HAMADI Rashid Mohammed-Mbunge wa Wawi, aliye katika mgogoro na Chama chake cha Wananchi (CUF) kwa zaidi ya miaka miwili sasa, leo ametangaza rasmi bungeni kugombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC). Anaandika Edson Kamukara …(endelea).

Hamad na wenzake 10 walivuliwa uanachama wa CUF kwa tuhuma za kukivuruga chama miaka michache iliyopita, lakini akafungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga uamuzi huo. Tangu wakati huo ameendelea kubakia bungeni kwa kinga ya mahakama ambayo haijatoa hukumu.

Muda mfupi baada ya Hamad kutimuliwa, anadaiwa kuanzisha chama kipya cha ADC kupitia “washirika wake”, jambo ambalo hajawai kulikanusha na badala yake amekuwa akijitambulisha kama mlezi wa chama hicho hadi alipojihalalisha rasmi leo.

Akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Hamad baada ya kugusia maeneo kadhaa ya ushauri kwa Serikali kusimamia uchumi wa nchi, ndipo akatangaza kung’atuka ubunge akisema hatagombea tena.

“Mheshimiwa Spika huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Mimi nimekuwemo humu bungeni tangu mwaka 1977, wewe Spika unafahamu. Sasa ningependa kuwaaga wabunge wenzangu kwamba sitagombea ubunge tena…napumzika kazi hiyo.

“Ila ninapostaafu kazi hiyo, natafuta utumishi mwingine. Hivyo, nakusudia kugombea urais wa Zanzibar kupitia ADC,” alisema Hamad na kusababisha ukumbi wa Bunge kulipuka kwa vicheko na makofi.

error: Content is protected !!