Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Halmashauri zisimamie miradi shirikishi ya misitu
Habari Mchanganyiko

Halmashauri zisimamie miradi shirikishi ya misitu

Spread the love

 

HALMASHAURI za Wilaya zenye vijiji vinavyotekeleza miradi ya usimamizi shirikishi wa misitu na biashara endelevu ya mazao ya misitu nchini zimetakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye ripoti za wanavijiji ili kuondoa changamoto ya mapungufu katika usimamizi wa fedha za shughuli za usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii (USMJ) na kuendeleza uhifadhi. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Ofisa sera na majadilino kutoka Mtandao wa usimamizi shirikishi wa misitu ya Jamii Tanzania (MJUMITA) Elida Fundi alisema hayo jana kwenye mkutano wa Kikosi kazi cha wadau wa shughuli za misitu Tanzania (TFWG) uliofanyika mkoani hapa ambapo alisema licha ya juhudi zinazoendelea kufanywa na wadau hao kuhakikisha wanavijiji wananufaika na mazao ya misitu lakini wapo baadhi ya viongozi wanaokiuka maelekezo ya kuweka fedha benki na kuanza kuzitumia kabla hawajaziingiza kwenye akaunti husika jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kifedha.

Alisema MJUMITA imekuwa ikishirikiana na wadau wengine wa misitu kupitia TFWG ili kusaidia vijiji kuwekeza katika USMJ na biashara endelevu ya mazao ya misitu jambo lililosaidia baadhi ya vijiji kuwezesha hadi kupata faida ya zaidi ya shilingi mil 100 na kuzifanyia shughuli mbalimbali za maendeleo ya vijiji.

Alisema katika kuhakikisha wanawajengea uwezo viongozi wa vijiji hivyo wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya, idara ya misitu na idara ya ukaguzi ambao huwaunganisha na wananchi na kufanya ukaguzi wa hesabu za vijiji na kuhakikisha wanafuata kanuni na taratibu za kisheria za matumizi ya fedha za serikali lakini wanavijiji hao hubadilisha utartaibu muda mfupi tu viongozi hao wanapoondoka.

Alisema amelazimika kusema hilo kwa sababu wamebaini kuanzishwa kwa desturi  kukabidhi fedha kienyeji kwa uongozi wa vijiji bila kupeleka benki hali ambayo haina matokeo mazuri baadae sababu wanavijiji hawataona umuhimu wa USMJ na hivyo kuacha kusimamia na kulinda misitu jambo ambalo sio lengo lao.

“tunatamani kuona kwamba vijiji vingine vilivyoanzisha utaratibu huo waendelee kusaidiwa na Halmashauri za wilaya na ofisi ya ukaguzi jambo litakalopunguza  mapungufu yaliyopo ya masuala ya utawala bora katika maeneo yao” alisema Fundi.

“Matumizi mabaya ya fedha yanatokea kwenye fedha ambazo zilipaswa kulipwa benki, na mtu anakuja kulipa kwenye halmashauri ya kijiji, na mtu akishika mkononi, mara nyingi binadamu tulivyo na hulka, hela haitaenda benki na itabaki mikononi, haipaswi, isiliwe pesa mbichi, iwekwe benki na itumike kwa kupitishwa kwenye Halmashauri ya kijiji, pamoja na mikutano mikuu ya hadhara ya kijiji” alisema.

Hivyo aliishauri Halmashauri ifanye ukaguzi angalau mara moja kwa kila mwaka kwa kupitia vijiji vinavyovuna mazao ya misitu jambo litakalosaidia vijiji kuwa na uelewe muda wote na kuendeleza shughuli za usimamizi shirikishi wa misitu na mazao ya misitu na kupata fedha wanayoitegemea hata pale mashirika yanayosimamia yatakapokwisha muda wake wa kufanya kazi katika maeneo hayo.

Naye Afisa Misitu mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa amewashauri wadau wa misitu kuona umuhimu wa kuwepo na ubia katika kusimamia misitu ya vijiji sababu nguvu ya vijiji katika kusimamia misitu bado ni ndogo ikiwemo kwenye masuala ya kifedha.

Hivyo alisema Serikali kuu, wakala wa misitu (TFS), Halmashauri na wanavijiji hawana budi kushirikiana jambo litakalofanya misitu kuonekana kuwa na faida kwa Serikali, Halmashauri na vijiji husika lakini vinginevyo hali haitakuwa nzuri hasa katika utunzaji misitu kuendana na wakati huu wa kuhimiza jamii kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!