May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Halmashauri zatakiwa kuongeza ukusanyaji mapato kupunguza utegemezi

Spread the love

 

SERIKALI imeziasa Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kutenga asilimia 40 ya mapato yao kukamilisha miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao. Anaripoti Danson Kaijage – Arusha … (endelea)

Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 20 Januari, 2022 Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dk. Festo Dugange wakati alipokutana na uongozi wa Halmashauri na Wilaya ya Monduli katika kikao cha pamoja.

Dk. Dugange amesema halmashauri hazina budi kuongeza wigo wa mapato yao na kukamilisha miradi yao ya maendeleo yenye tija badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.

Ameitaja baadhi ya miradi yenye tija ambayo itahitaji fedha za asilimia 40 zilizotengwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa ni pamoja na maboma ya zahanati, nyumba za watumishi, madarasa ya shule za msingi na matundu ya vyoo.

“Kwa hiyo ni lazima tukusanye kwa ufanisi kisha asilimia 40 tunatenga ili iende kuimarisha miundombinu hiyo lakini ni lazima uchague miradi michache ambayo fedha ile itakamilisha,” amesema.

Katika hatua nyingine Dk. Dugange ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kwa kutenga shilingi milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto katika zahanati ya Nafco.

Zahanati hiyo iliyopo katika kijiji cha Nafco, Kata ya Loksale, Tarafa ya Kisongo inatarajiwa kupandisha hadhi na kuwa kituo cha afya.

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Ngakoka Ludwig amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri yake ilipanga kupeleka shilingi milioni 245 lakini mpaka sasa wamepeleka fedha kwenye miradi ya nyumba tatu za watumishi.

Amesema nyumba hizo zipo kwenye zahanati tatu za Matinda, Meserani na Meserani Bwawani ambapo kila zahanati imepewa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba moja ya mtumishi.

error: Content is protected !!