October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Halmashauri ya Chadema yaenda kujifunza kwa CCM

Soko Kuu la Dodoma

Spread the love

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Dodoma ambayo inaongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi amesema wameamua kufanya ziara katika halmashauri inayongozwa na CCM kwani katika suala la maendeleo wanatakiwa kuweka pembeni itikadi zao kwani wanajenga nyumba moja.

Meya, Mwashilindi amesema lengo la ziara hiyo ya mafunzo ni kujifunza jinsi ya ukusanyaji wa mapato pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa na yakati, ambayo Dodoma wamefanya vizuri.

“Tumekuja kujifunza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kati masuala ya usafi pamoja na kubadilishana uzoefu.

“Halmashauri ya Jiji la Mbeya linaongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jiji la Dodoma linaongozwa na CCM lakini katika mambo ya maendeleo lazima tutambue kuwa tunajenga nyumba moja kwa faida ya wananchi tunaowaongoza,” alisema Meya Mwashilindi.

Naye Afisa Utumishi wa Jiji la Dodoma, Bartazar Ngowi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema Jiji la Dodoma wamepokea wageni wa Baraza la Madiwani kutoka Jiji la Mbeya kwa nia ya kujifunza namna gani Dodoma inaweza kukusanya mapato na kutekeleza miradi mikubwa.

“Tumepata ugeni kutoka Mbeya nia ikiwa kubadilishana ujuzi na utendaji kazi, kutembelea miradi pamoja na kujifunza ni kwa namna gani Jiji la Dodoma linaweza kukusanya mapato na kuwa na bajeti kubwa,” alieleza Ngowi.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Fedha katika Jiji la Dodoma, Alfred Mlowe amewapa siri za kwanini Jiji la Dodoma wanafanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

Mlowe amesema kuwa kinacholifanya Jiji la Dodoma kuweza kukusanya mapato kwa kiwango kikubwa ni ushirikishwaji kati ya idara na idara, kitengo kwa kitengo, jambo lingine ambalo linalifanya Jiji la Dodoma kupaa kimapato ni kuhakikisha kila idara inafanya kazi ya ukusanyaji mapato kwa uaminifu na ushirikiano.

Katika maelezo yake Mkuu wa Idara ya Fedha, Mlowe alisema katika Jiji la Dodoma hakuna pesa ambayo inakusanywa kwa mfumo wa kutumia makaratasi (analog) bali fedha zote zinakusanywa kwa mfumo wa eletloniki.

error: Content is protected !!